• HABARI MPYA

  Jumapili, Septemba 29, 2013

  SIMBA SC YAZIDI KUTISHA LIGI KUU, HUYO TAMBWE AISEE BALAA, AZAM SARE MBEYA, ASHANTI YAIKATALIA MTIBWA CHAMAZI

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 29, 2013 SAA 4:30 ASUBUHI
  SIMBA imezidi kujitanua kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Azam FC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Prisons mjini Mbeya. 
  Uwanja wa Taifa, hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Mrundi Amisi Tambwe dakika ya 24 kwa penalti, baada ya beki Jamal Said wa JKT Ruvu kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
  Hata hivyo, wachezaji wa JKT Ruvu walimzonga mshika kibendera nambari moja, John Kanyenye wa Mbeya aliyetoa penalti hiyo kabla ya kutulia na kuruhusu mkwaju upigwe- na Tambwe akaenda kufunga bao lake la saba katika Ligi Kuu msimu huu ndani ya mechi sita.
  Mabao saba mechi sita; Wachezaji wa Simba SC wakimpongeza Tambwe baada ya kufunga bao la kwanza jioni ya leo

  Simba SC ndiyo waliotawala zaidi mchezo kipindi cha kwanza ingawa na JKT Ruvu walikuwa wakishambulia mara kadhaa, lakini ngome ya Wekundu wa Msimbazi ikiongozwa na kipa mrefu zaidi katika Ligi Kuu, Abbel Dhaira ilikuwa imara hii leo.
  Simba SC ilipata pigo dakika ya 30, baada ya kiungo wake mahiri, Amri Kiemba kuumia goti na kutoka  nje, nafasi yake ikichukuliwa na Ramadhani Singano ‘Messi’.  
  Kipindi cha pili, Simba SC walikianza kwa kasi na kufanikiwa bao la pili dakika nne tu tangu kuanza kwa ngwe hiyo ya lala salama kupitia kwa Ramadhani Singano ‘Messi’.
  Messi alifunga bao hilo baada ya kuuwahi mpira uliorudishwa na mabeki wa Ruvu kufuatia Amisi Tambwe kuunganisha krosi maridadi ya Abdulhalim Humud ‘Gaucho’.
  Baada ya bao hilo, JKT waliongeza kidogo kasi ya mashambulizi yao, lakini hawakuwa na mipango mwafaka ya kuipenya ngome ya Simba SC.
  Mawinga wa JKT walikuwa wakitia krosi za juu langoni mwa Simba wakati washambuliaji wao ni wafupi na kipa wa Wekundu wa Msimbazi, Abbel Dhaira pamoja na mabeki wake, Kaze Gilbet na Joseph Owino ni warefu.
  Kwa matokeo hayo, Simba SC inatimiza pointi 14 baada ya kucheza mechi sita na kujiimarisha kileleni mwa ligi hiyo. 
  Wchezaji wa JKT Ruu wakimzonga refa Anthony Kayombo baada ya kuwapa SImba SC penalti iliyozaa bao la kwanza

  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, Haruna Shamte, Adeyoum Seif, Kaze Gilbert, Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Amri Kiemba/Ramadhani Singano dk29, Said Ndemla, Betram Mombeki/Miraj Madenge dk63, Amisi Tambwe na Haroun Chanongo/Marcel Kaheza dk56. 
  JKT Ruvu; Shaaban Dihile, Damas Makwaya, Stanley Nkomola, Omar Mtaki, Jamal Said, Nashon Naftali, Alhaj Zege, Emanuel Swita/Richard Msenya dk58, Bakari Kondo/Paul Ndauka dk78, Salum Machaku na Emanuel Pius.
  Katika mechi nyingine, Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Azam FC imetoka sare ya 1-1 na Prisons, bao la Azam likifungwa na Kipre Tchetche dakika ya 49 na la Prisons lilifungwa na Peter Michael dakka ya 36 na Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Ashanti United imetoka sare ya 2-2 na Mtibwa Sugar. Mabao ya Ashanti yalifungwa na Paul Maone na Tumba Swedi, wakati ya Mtibwa yalifungwa na Shaaban Kisiga ‘Malone’.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA SC YAZIDI KUTISHA LIGI KUU, HUYO TAMBWE AISEE BALAA, AZAM SARE MBEYA, ASHANTI YAIKATALIA MTIBWA CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top