• HABARI MPYA

  Tuesday, September 24, 2013

  KINDA ALIYEIUA YANGA SC JUZI HAKUWA CHAGUO LA MAKOCHA AZAM...ALIPANGWA KWA SHINIKIZO LA WENYE TIMU

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 24, 2013 SAA 1:48 ASUBUHI
  KINDA Joseph Kimwaga aliyeifungia Azam FC bao la ushindi dakika za lala salama katika mechi dhidi ya Yanga SC juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam timu hiyo ikishinda 3-2 hakuwa chaguo la kocha Muingereza Stewart John Hall kucheza mechi hiyo, imefahamika.
  Habari kutoka ndani ya Azam FC, zimesema kwamba mchezaji huyo pamoja na kinda mwenzake, Farid Mussa waliingizwa kwenye programu za mchezo huo kwa shinikizo la Wakurugenzi wa timu, ambao wanaheshimu uwezo wao.
  Bao la ushindi; Joseph Kimwaga akifumua shuti baada ya kuwaacha mabeki wa Yanga kuifungia Azam bao la ushindi wa juzi

  Furaha; Kimwaga akifurahia baada ya mpira kutinga nyavuni
  Kufuatia Azam FC kulazimishwa sare ya 1-1 na timu dhaifu, Ashanti United katikati ya wiki iliyopita, na kuonekana kabisa wachezaji hawakucheza kwa kujituma, Wakurugenzi walimuamuru Stewart kuanza kuwatumia wachezaji wa kikosi cha pili, Azam Akademi. 
  Pamoja na Stewart kuonekana kutokuwa na imani na makinda wa Akademi, lakini alishinikizwa na akaambiwa awaweke kando wachezaji wote ambao walionekana dhahiri kucheza bila kujituma dhidi ya Ashanti United.
  Na katika mchezo wa juzi dhidi ya Yanga SC wachezaji wa kudumu wa kikosi cha kwanza cha Azam FC kama Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Khamis Mcha ‘Vialli’ hawakuwepo hata benchi, badala yake makinda Kimwaga na Farid walichukua nafasi. 
  Hakuwa chaguo lao; Makocha wa Azam kutoka kushoto, Stewart Hall na Wasaidizi wake, Kali Ongala na Ibrahim Shikanda 

  Farid alianza na kucheza vizuri wingi ya kushoto akimpita mara kadhaa Mbuyu Twite na kutia krosi nyingi maridadi kabla ya kumpisha ‘mshindi wa mechi’, Kimwaga dakika ya 72 akaenda kuwamaliza Yanga SC.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Dominic Nyamisana, aliyesaidiwa na Charles Simon na Flora Zablon wote wa Dodoma, hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ sekunde ya 34 tu, baada ya kuuwahi mpira uliorudishwa na beki Kevin Yondan kufuatia pigo la kichwa la Brian Umony na kuutumbukiza nyavuni. 
  Yanga SC inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts, ilikuja juu baada ya bao hilo na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Azam, lakini hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika hawakufanikiwa kupata bao.
  Lakini kipindi cha pili, Yanga walirudi na moto mkali na kufanikiwa kusawazisha bao dakika ya 48 kupitia kwa Mrundi, Didier Kavumbangu aliyeutokea mpira mrefu na kwenda kumchambua kipa wa Azam, Aishi Manula.  
  Mshindi wa mechi; Kimwaga akipongezwa na wenzake kwa bao zuri la ushindi juzi


  David Luhende wa Yanga SC kulia aliteswa na kijana juzi Taifa

  Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Azam na kufanikiwa kupata bao la pili, dakika ya 65 mfungaji Hamisi Kiiza aliyemalizia pasi ya Simon Msuva.
  Beki Kevin Yondan aliunawa mpira kwenye eneo la hatari dakika ya 68 na Kipre Herman Tchetche akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 69 na kufanya 2-2.
  Azam waliokoa shambulizi la hatari langoni mwao na kuanzisha shambulizi la haraka- na mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Uhai msimu uliopita, Kimwaga hakufanya makosa- hadi mwisho Azam 3-2 Yanga.
  Hata huyu noma; Farid Mussa alimpita mara kadhaa Mbuyu Twite na kutia krosi maridadi
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KINDA ALIYEIUA YANGA SC JUZI HAKUWA CHAGUO LA MAKOCHA AZAM...ALIPANGWA KWA SHINIKIZO LA WENYE TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top