• HABARI MPYA

    Sunday, September 22, 2013

    MANJI ASITARAJIE ‘UBWETE’, YANGA NI ILE ILE NA WATU WALE WALE

    IMEWEKWA SEPTEMBA 22, 2013 SAA 3:29 ASUBUHI
    MOJA kati ya misimu mitamu na ya kukumbukwa ya Ligi Kuu ya Bara ni wa mwaka 2003, wakati huo ligi inaanzia kwenye hatua ya makundi, baadaye inachezwa hatua ya mwisho ya Nane Bora.  
    Ulikuwa mfumo mzuri, kwa sababu baada ya kuchuja ‘pumba’ zile timu ngangari zinakutana katika hatua ya mwisho ya kusaka bingwa.
    Katika msimu huo, kuelekea mechi za mwisho Yanga SC ilikuwa inachuana kileleni na Mtibwa Sugar, zote zikiwa na pointi 23, Jangwani wakiwa kileleni kwa wastani wa mabao mawili zaidi, wakati mahasimu wao, Simba SC walikuwa nafasi ya tatu na pointi zao 22.

    Mbio za ubingwa hapa, wazi zilikuwa za Yanga SC na Mtibwa- na Simba SC walikwishakata tamaa hata ya nafasi ya pili, unajua kwa sababu gani?
    Yanga SC ilikuwa inamaliza na Prisons ambayo ilikuwa inachukuliwa kama haitatoa upinzani na Mtibwa Sugar ilikuwa inamaliza na Twiga SC ya Kinondoni, ambayo ilichukuliwa kama dhaifu.
    Simba SC ilikuwa inamaliza na moja ya timu ngumu wakati huo, AFC ya Arusha Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiamini hata ikishinda haiwezi kutwaa ubingwa, kwa kuwa ilizipa nafasi kubwa Yanga na Mtibwa kushinda mechi zao za mwisho.
    Nini kilitokea katika mechi za mwisho Novemba 26, mwaka 2003? Prisons iliitandika Yanga SC 3-2 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Twiga SC ikaichapa Mtibwa Sugar 3-2 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wakati ushindi wa mabao 2-0 wa Simba SC dhidi ya AFC ulitosha kabisa kuimaliza ligi tofauti na ilivyotarajiwa, Wekundu wa Msimbazi wakitwaa taji kwa pointi moja zaidi dhidi ya Prisons iliyoshika nafasi ya pili kutoka ya tano. Yanga ilishuka nafasi ya tatu na Mtibwa nafasi ya nne.
    Kwa nini nimekumbusha msimu huo wa Ligi Kuu. Nitawaambia. Yanga SC ilikuwa Mbeya kwa mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya wenyeji wa mkoa huo, Mbeya City na Prisons na kuambulia sare katika mechi zote, ya kufungana bao 1-1.
    Baada ya matokeo hayo, ameanza kusakwa mchawi Yanga SC, wachezaji wakituhumiwa kutojituma na pia eti kuna mgawanyiko ndani ya uongozi, ndivyo vinasababisha hali hiyo.
    Kama Yanga SC wana matatizo yao ndani ya uongozi, na wanayajua vyema wakayatatua kwa mustakabali mzuri wa klabu yao, lakini sina hakika sana kama ni sahihi kuanza kuchimbua vitu kwa sababu ya matokeo ya Mbeya.
    Kwa timu ngeni katika Ligi Kuu, inaweza kuwa na fikra hizo, lakini kwa wazoefu wa Ligi Kuu kama Yanga SC wanapaswa kutambua kama Mbeya ni moja ya mikoa migumu kuvuna pointi kwa urahisi, kwa sababu mara nyingi wanazalisha timu za ushindani.
    Hiyo ni tangu ya enzi za Tukuyu Stars waliokuwa hadi mabingwa wa Bara mwaka 1986 na baadaye Mecco, kabla ya hizi Prisons na Mbeya City. 
    Prisons iliteleza katika mechi mbili za mwanzoni msimu huu, lakini baada ya hapo imetoa sare moja ugenini na Coastal Unio mjini Tanga na nyingine na Yanga Jumatano.
    Mbeya City imeonyesha ni timu nzuri baada ya kwenda kutoa sare hadi ugenini, Manungu mbele ya Mtibwa Sugar na jana Taifa dhidi ya Simba SC. Najua, Yanga SC watakuwa wanahesabu idadi ya mechi za ugenini za wapinzani wao, Simba SC na kulinganisha na wao juu ya  matokeo.
    Simba SC katika mechi zake mbili za ugenini, imevuna pointi nne, moja Tabora kwa sare ya 2-2 na Rhino Rangers na nyingine Arusha kwa ushindi wa 1-0 na JKT Oljoro, wakati wao wamevuna mbili tu Mbeya. Simba SC haijafika Mbeya. Arusha ni Arusha na Mbeya ni habari nyingine.
    Simba SC wameonjeshwa tu jana Taifa Mbeya ikoje, lakini na wao watakwenda huko. Ni mapema mno Yanga SC kuanza kuweweseka, ligi bado mbichi na Mbeya ni kugumu kihistoria- tangu Kenneth Pius Mkapa bado Nahodha wa Yanga kabla ya Ally Mayay Tembele ‘Meja’ na Freddy Mbuna Swale.
    Jambo la msingi, kocha Mholanzi, Ernie Brandts na Wasaidizi wake wafanyie kazi mapungufu ya timu yao baada ya sare tatu mfululizo badala ya kuanza kufukua fukua mambo, ambayo yanaweza kuleta matatizo zaidi katika klabu hiyo.
    Siku zote, ukiwa kiongozi wa Simba au Yanga tarajia tu lazima kutakuwa na watu nje ni wapinzani wako na hawataki ufanikiwe- na hizo ndizo changamoto zenyewe za uongozi, kama huwezi kukabiliana nazo, bado hufai.
    Alhaj Ismail Aden Rage pale Simba SC kila siku yupo kwenye mapambano na wapinzani na bado anaendelea na majukumu yake ya kuongoza klabu. Vivyo hivyo, Mwenyekiti wa Yanga SC, Alhaj Yussuf Mehboob Manji asitarajie ‘ubwete’ katika kuiongoza klabu hiyo. 
    Yanga SC ni ile ile ya tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere (marehemu) na watu wake ni wale wale na kwa kiasi kikubwa tabia na desturi ni zile zile. Upinzani nadra kukosekana, hivyo apambane tu kuonyesha uwezo na umahiri wake katika kukabiliana na mambo, ili kudhihirisha yeye ni kiongozi kweli.
    Wale maelfu wanaomiminika uwanjani, shida yao ni kushangilia ushindi tu na mwisho wa msimu mataji. Hilo ni deni analo. Siku njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MANJI ASITARAJIE ‘UBWETE’, YANGA NI ILE ILE NA WATU WALE WALE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top