• HABARI MPYA

    Sunday, September 29, 2013

    MCHEZAJI BORA WA ARS ANAWEZA KUWA BORA PIA AFCON, NI MIPANGO TU NA LAZIMA TUJUE MAMILIONI YA FIFA YANATUMIKAJE TFF

    IMEWEKWA SEPTEMBA 29, 2013 SAA 1:59 ASUBUHI
    SOKA ya Tanzania wiki hii imepokea habari njema, kufuatia timu ya wasichana ya Tanzania kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya kimataifa ya Airtel Rising Stars mjini Lagos, Nigeria, baada ya kuwafunga majirani Kenya bao 1-0 katika Fainali. 
    Shukrani wake, Donisia Daniel aliyeifungia bao hilo pekee Tanzania iliyokuwa kundi moja na nchi za Sierra-Leone, Malawi na Uganda. Safari ya ubingwa kwa mabinti wa Tanzania ilianzia katika mechi za kundi lao, wakishinda moja dhidi ya Sierra-Leone 2-1, wakafungwa moja dhidi ya Uganda na kutoka sare ya 1-1 na Malawi.
    Katika Robo Fainali, mabinti wa kibongo wakashinda 4-2 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Uwanja wa Taasisi ya Michezo, kabla ya kuifumua Uganda kwa mabao 8-1 kwenye Nusu Fainali.

    Mbali na ushindi huo wa wasichana, Tanzania pia imejishindia tuzo mbalimbali ikiwemo, kutoa Mchezaji bora kwa upande wa wasichana ambaye ni Tatu Iddi, Mfungaji bora wa mashindano kwa upande wa wavulana, ambaye ni Athanas Mdam na Mfungaji bora kwa upande wa wasichana, ambaye Shelida Boniface.
    Kwa upande wa wavulana, Niger ilifanikiwa kutetea tena ubingwa baada ya kuifunga Zambia kwa mikwaju ya penalti 7-6 katika fainali ya Airtel Rising Stars kwenye Uwanja wa Agege nchini Nigeria. Wavulana ya Tanzania walishika nafasi ya nne kati ya timu zaidi ya 16 zilizoshiriki michuano hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vinne, Agege, Township, Legacy Pitch, Taasisi ya Michezo ya Taifa na Main Bowl. Mashindano ya Airtel Rising Stars yamefanyika kwa mara ya pili mwaka huu, yakiendelea kujikusanyia sifa za ubora miongoni mwa mashindano ya vijana.
    Nimeanza kwa kusema soka ya Tanzania imepokea habari njema, kwa sababu wahenga wanasema nyota njema huonekana asubuhi. Mabinti wadogo chini ya umri wa miaka 17 wanabeba ubingwa wa Afrika, wazi hao wakiendelezwa vyema tangu sasa, wanaweza kuwa bora zaidi na kuiletea sifa zaidi nchi hii.
    Sote tunafahamu, umuhimu wa kuwekeza katika soka ya vijana, kwani huko ndiyo sehemu mwafaka ya kuandalia nyota wa baadaye na kwa jumla timu bora za taifa za baadaye.
    Kwa takriban miaka 10 sasa Tanzania imekuwa na vyanzo vingi vya kuibua vipaji vya wanasoka wadogo ambao wameonyesha wanaweza kwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa  ya vijana kama hiyo ya Airtel Rising Stars na Copa Coca Cola.
    Lakini tatizo moja kubwa, hakuna mipango mizuri ya kuwaendeleza vijana wanapoibuka na matokeo yake tumekuwa tukipoteza vipaji vingi hapa katikati na kusababisha maana nzima ya kuwa na mashindano ya kuibua vipaji kutoweka.
    TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) wao wanasema hawana fedha za kusimamia mipango ya uendelezaji wa vijana- lakini sisi tunajua katika ruzuku ya kila mwaka ya dola 250,000 kutoka FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) sehemu ya fedha hizo inatakiwa itumike kwa ajili ya maendeleo ya soka ya wanawake na vijana.
    Fedha hizo kutoka FIFA maarufu kama FAP kwa mwaka huu zimeletwa dola 35,000 kwa ajili ya maendeleo ya vijana, dola 10,000 wanaume, dola 37,000 Wanawake, Ufundi dola 27,0500, Marefa dola 20,000, Tiba dola 15,000, Futsal na soka ya ufukweni dola 5,000, Utawala na Mipango dola 67,000, Miundombinu dola 15,000 na dola 18,000 kwa ajili ya mambo mengine. 
    Ikumbukwe mwaka 2011 TFF ilipokea dola 300,000 zaidi ikiwa ni pamoja na bonasi ya Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2010 na kufanya jumla ya dola 550,000 wakati mwaka 2010 TFF ilipata dola 250,000 zaidi za Kombe la Dunia na kufanya jumla ya dola 500, 000.
    Bado kuna mipira inayoingia TFF kila mwaka kutoka Adidas na tangu mwaka 2003 hadi 2010 ilipokea mipira 1000 ya ukubwa wa saizi tano, ingawa kwa ajili ya vijana wanatakiwa kuomba mipira ya saizi nne. Tangu 2011 hadi 2014 tayari mipira 500 imekwishaingia pale Karume.
    Bado kila mechi inayochezwa nchini, TFF ina mgawo wake, tena mzuri- je ni kiasi gani cha fedha ambacho kinakwenda katika mfuko wa kuendeleza vijana na wanawake? Katika moja ya makato maarufu kwenye mechi za mashindanio mbalimbali nchini, kuna fungu la Jichangie, wenyewe wanasema linakwenda kwenye mfuko wa maendeleo, ni mfuko upi?    
    Lakini kwa ujumla ni jitihada gani zinafanywa kushawishi makampuni, wafadhili na wawekezaji kwa ujumla kusaidia mfuko wa kuendeleza vijana? Lazima tujue ni nini kipaumbele cha TFF katika kuongoza soka ya nchi hii.
    Mchezaji bora wa Airtel Rising Stars anaweza kuwa mchezaji bora wa Kombe la Mataifa ya Afrika miaka mitatu au minne baadaye, iwapo itawekwa mkakati wa kumuendeleza kuanzia sasa. Nichukue fursa hii kuwapongeza mabinti walioitangaza vyema Tanzania nchini Nigeria  na kwa ujumla niwatakie wikiendi njema. Asanteni kwa kusoma. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MCHEZAJI BORA WA ARS ANAWEZA KUWA BORA PIA AFCON, NI MIPANGO TU NA LAZIMA TUJUE MAMILIONI YA FIFA YANATUMIKAJE TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top