• HABARI MPYA

  Alhamisi, Juni 27, 2013

  YANGA SC KUCHEZA NA KCC YA UGANDA KATIKA ZIARA YA KOMBE KANDA YA ZIWA

  Mwali anapelekwa Mwanza
  Na Prince Akbar, IMEWEKWA JUNI 27, 2013 SAA 5:12 ASUBUHI
  MSHAMBULIAJI nyota Tanzania, Mrisho Ngassa aliyerejea Yanga SC majira haya ya joto akitokea kwa wapinzani wa jadi, Simba SC, zote za Dar es Salaam ataanza rasmi kuichezea timu hiyo Juni 6, mwaka huu mjini Mwanza.
  Mabingwa hao wa Tanzania Bara na Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC watacheza na KCC ya Uganda badala ya Rayon Sport ya Rwanda Julai 6 na 7, mwaka huu katika sehemu ya ziara yake ya kulitembeza Kombe lake la ubingwa wa Ligi Kuu mikoa ya kanda ya Ziwa, ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
  TBL imekuwa ikiidhamini Yanga SC kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager tangu mwaka 2008 sawa na wapinzani wao wa jadi, Simba SC na ndiyo wamedhamini ziara hiyo.
  Akizungumza na Waadishi wa Habari leo asubuhi, makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto amesema kwamba timu itaondoka Julai 5 Dar es Salaam, siku mbili tu baada ya kuanza mazoezi Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam kuelekea Mwanza tayari kwa mchezo wa kwanza dhidi ya wapinzani wao hao, Uwanja wa CCM Kirumba, Julai 6.
  Kizuguto amesema Julai 7, timu hizo zitarudiana kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na baada ya hapo, mabingwa hao mara tano wa Kombe la Kagame (Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati), Yanga SC wataelekea mjini Tabora, kucheza mechi nyingine na wenyeji, Rhino FC waliopanda Ligi Kuu msimu huu Julai 11, mwaka huu Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.
  Katika ziara hizo, Yanga watatembeza Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu, walilolitwaa kwa mara ya 24 msimu huu kwenye mitaa mbalimbali kushangilia na mashabiki wao. 
  Yanga SC imeshindwa kwenda Sudan kutetea Kombe lake la Kagame mwaka huu, kutokana hofu ya machafuko yanayoendelea nchini humo na hii inakuwa mara ya pili kihistoria klabu hiyo kugoma kwenda kutetea taji hilo, baada ya awali mwaka 2000 kukataa kwenda Rwanda, hadi walipwe fedha zao za zawadi kwa kutwaa taji la mwaka uliotangulia 1999 mjini Kampala, Uganda.
  Yanga SC, imekuwa na mafanikio makubwa tangu ianze kudhaminiwa na TBL, ikitwaa jumla ya mataji sita katika kipindi hicho, yakiwemo mawili ya Kagame, 2011 na 2012 na manne ya Ligi Kuu Bara, 2008, 2009, 2011 na 2013.
  Katika kipindi hicho, hadhi ya klabu ya Yanga imepanda kutoka klabu isiyo na gari hata moja, hadi sasa kuwa mabasi matatu ya viwango tofauti, dogo aina ya Hiece, kubwa aina ya Coaster na kubwa zaidi aina ya Yutong kwa ajili ya safari za nje ya Jiji, ambayo yote wamepewa na wadhamini wao hao wakuu.
  Kwa ujumla udhamini wa TBL umeleta ahueni kubwa ndani ya Yanga katika suala la uendeshaji wa timu, kutoka kwenye kushindwa kulipa mishahara ya makocha na wachezaji, hadi sasa kuwa na uhakika wa kufanya yote hayo sambamba na kusajili wachezaji ‘babu kubwa’ barani, kama Haruna Niyonzima, raia wa Rwanda. Mkataba wa awali baina ya Yanga na TBL, ulisainiwa Agosti 18, mwaka 2008 katika hoteli ya Movenpick, mjini Dar es Salaam, ukiwa na thamani ya Sh bilioni 3 za Kitanzania na kwa miaka mitatu, ikiwa kila mwaka inapata Sh Bilioni 1, kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa timu 
  Agosti 2, mwaka 2011, TBL ilisaini Mkataba wa udhamini na Yanga wa miaka minne sawa na kwa watani wao pia, Simba SC.
  Katika mkataba huo mpya, uliotiwa saini kwenye hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es Salaam, TBL iliongeza dau la fedha za mishahara kwa wachezaji kutoka Sh. Milioni 16 hadi Milioni 25 kwa mwezi, ikaongeza basi moja kubwa, Yutong lenye uwezo wa kubeba abiria 54 na fedha kwa ajili ya kugharamia mikutano ya wanachama ya kila mwaka Sh. Milioni 20 kugharamia tamasha la mwaka la klabu na vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh. Milioni 35 kila msimu.
  Yanga pia inapewa bonasi ya Sh. Milioni 25 ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara au Milioni 15, ikishika nafasi ya pili katika Mkataba huo wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 5 tangu Agosti 8, mwaka huu hadi Julai 31, mwaka 2016.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA SC KUCHEZA NA KCC YA UGANDA KATIKA ZIARA YA KOMBE KANDA YA ZIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top