• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 28, 2013

  BARTHEZ ALIBARIKI USAJILI WA DIDA YANGA BAADA YA PENDEKEZO LA KOCHA, ASEMA BIN KLEB

  Kifaa kipya Jangwani; Deo Munishi 'Dida' ametua kwa baraka za Barthez
  Na Prince Akbar, IMEWEKWA JUNI 28, 2013 SAA 2:30 ASUBUHI
  MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kwamba wamemsajili Deogratius Munishi ‘Dida’ kwa sababu ni kipa aliyependekezwa na kocha wao, Mholanzi Ernie Brandts na pia kipa wao namba moja kwa sasa, Ally Mustafa ‘Barthez’ akabariki usajili huo.   
  Akizugumza na BIN ZUBEIRY asubuhi ya leo, Bin Kleb amesema kwamba kocha Brandts alipendekeza Dida ndiye asajiliwe kuwa kipa wa pili katika klabu hiyo, baada ya Barthez, ambaye ndiye Yanga One kwa sasa.
  “Lakini kabla ya kumsainisha, tuliomba maoni ya watu mbalimbali akiwemo kipa wetu namba moja wa sasa, naye akatoa baraka zake kwamba Dida ndiye anayefaa,”alisema.
  Bin Kleb amesema kulikuwa kuna baadhi ya maoni yakipendekeza Juma Kaseja aliyetemwa Simba SC asajiliwe Yanga SC, lakini baada ya uongozi kujadili ukaona ni bora kufuata mapendekezo ya mwalimu kwa kumsajili Dida.
  Tumemsaini Dida; Bin Kleb
   akizungumza na simu

  “Kulikuwa kuna majina ya makipa watatu, kati yao, wawili wote wamekwishawahi kudakia Yanga, Kaseja na Benjamin Haule, lakini katika majumuisho, Dida akawa ameshinda mchakato nasi tukamsainisha Mkataba wa miaka miwili jana mchana,”alisema. 
  Kleb amesema Dida anachukua nafasi ya Said Mohamed ambaye ameachwa baada ya kumaliza Mkataba wake wa miaka miwili tangu asajiliwe kutoka Majimaji ya Songea.
  “Dida ni kipa mzuri, ana uzoefu wa kutosha. Ni kipa ambaye amekuwa akikubalika mbele ya makocha wengi wa timu ya taifa hapa nchini, tumeona atatufaa na tumempa Mkataba wa Miaka miwili,”alisema Kleb.
  Dida atakwenda kuwa kipa wa pili Yanga SC, baada ya Ally Mustafa ‘Barthez’ waliyekuwa naye Simba SC.
  Magazeti yalianza kutabiri kwamba, baada ya Kaseja kumaliza miaka yake tisa ya kuitumikia Simba SC angekwenda kuungana tena na Barthez Yanga, ila usajili huu wa Dida, unafuta uwezekano huo.
  Kaseja sasa kuna uwezekano akatua Azam FC, ambayo ina kipa mzoefu mmoja tu, Mwadini Ally ambaye naye dhahiri hafikii uwezo wa Tanzania One huyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: BARTHEZ ALIBARIKI USAJILI WA DIDA YANGA BAADA YA PENDEKEZO LA KOCHA, ASEMA BIN KLEB Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top