• HABARI MPYA

  Jumapili, Juni 30, 2013

  WACHEZAJI TAIFA STARS CHUPUCHUPU KUTAPELIWA KWA TAMAA YA KUCHEZA ULAYA

  Mngetapeliwa; Kutoka kulia, Athumani Iddi 'Chuji',Amri Kiemba na Nadir Haroub 'Cananvaro', wachezaji wa Taifa Stars wanaocheza nyumbani, ambao wote wana kiu ya kucheza Ulaya
  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JUNI 30, 2013 SAA 2:31 ASUBUHI
  UTAPELI umedunda! Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeshitukia utapeliwa uliotakwa kufanywa na watu wanaojifanya mawakala wa wachezaji kwa gia ya kutaka kuwatafutia wachezaji nchini timu za kuchezea Ulaya.
  Wiki iliyopita, TFF ilitoa taarifa za klabu ya Thai Port Football ya Thailand kutafuta wachezaji nchini Tanzania kwa ajili ya kucheza soka nchini humo na katika nchi nyingine barani Ulaya.
  Taarifa hiyo ya TFF ilisema, kupitia kwa wakala wake, klabu hiyo imetuma taarifa TFF ikitaka wachezaji wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 28 kwa ajili ya kuwafanyia majaribio ambapo watakaofuzu watacheza nchini humo na katika klabu nyingine za Ulaya ambazo wana ushirikiano nazo.
  Taarifa hiyo iliwataka wachezaji wenye nia ya kufanya majaribio kutuma taarifa za wasifu wao (CV) kwa klabu hiyo kwa njia ya emaili, wawe na pasi ya kusafiria pamoja na pasi ya mchezaji (player passport).
  Eti baadaye wakala atapitia vitu hivyo, na kwa wachezaji atakaowahitaji atawatumia tiketi za ndege na viza kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio nchini humo, na watakaofanikiwa kabla ya kusaini nao mikataba watawasiliana na klabu zao nchini (kwa wale wenye klabu).
  Katika mahojiano na BIN ZUBEIRY juzi ofisini kwake, Ilala, Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kwamba wametilia shaka dili hilo baada ya uchunguzi wa awali walioufanya.
  “Tuliwasiliana na FA (chama cha soka) cha Thailand, wakasema hiyo klabu ipo, lakini haina mpango huo. Zile anuania walizotumia jamaa ni za klabu ile. Na namba za simu ukipiga wanapokea mnazungumza, lakini kumbe wao waliingilia mfumo wa mawasiliano wa ile klabu na kuuteka ili kuutumia kutapeli.
  “Kwa hivyo tumesitisha hilo zoezi kwanza, ili tuendelee na uchunguzi zaidi, ila wachezaji walikwishajitokeza na kutuma maombi, ila tunasikitika mmoja tu ndiye alikamilisha taratibu zote,”alisema Wambura.
  Wambura alisema kilichowatia wasiwasi TFF hadi kuamua kufanya uchunguzi ni masharti yaliyotolewa, yakimtaka mwombaji nafasi kwanza alipe ada ya kujisajili, ambayo ni dola za Kimarekani 486 (zaidi ya Sh. 700,000 za Tanzania) 486 na baadaye tena atatakiwa kulipa dola 1,000 (zaidi ya Sh. Milioni 1,600,000) ndipo anatumiwa tiketi. 
  “Ina maana mtu angetoa kiasi cha dola 2,000 (zaidi ya Sh. Milioni 3, 200,000) kwanza ndio atumiwe tiketi na hatudhani kama angetumiwa tiketi. Na kwa uzoefu wetu juu ya masuala haya namna ambavyo wachezaji wanaletewa mialiko ya kwenda nje, hii ilitutia shaka mapema,”alisema.
  Matokeo ya hivi karibuni ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mechi za Kundi C kuwanai tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia yanaonyesha soka ya nchini imekuwa, lakini wachezaji wanaangushwa na uzoefu wa kutocheza Ulaya.
  Na wachezaji wa Tanzania sasa wana hamu ya kucheza Ulaya ili kunufaika kimaslahi na pia kukuza viwango vyao- inaonekana wajanja wanataka kutumia udhaifu huu kutapeli vijana nchini hivi sasa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: WACHEZAJI TAIFA STARS CHUPUCHUPU KUTAPELIWA KWA TAMAA YA KUCHEZA ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top