• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 26, 2013

  JUMA KASEJA ATEMWA 'KIROHO MBAYA' SIMBA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JUNI 26, 2013 SAA 1:00 ASUBUHI
  MLINDA mlango nambari moja Tanzania, Juma Kaseja Juma amehitimisha miaka yake tisa ya kuitumikia klabu ya Simba SC baada ya klabu hiyo kuamua kutomuongezea Mkataba, baada ya Mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu.  
  Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya Simba SC, zimesema kwamba Kaseja anaachwa baada ya kuitumikia kwa mafanikio makubwa klabu hiyo tangu mwaka 2003 aliposajiliwa kutoka Moro United, eti kwa sababu hakubaliki kwa sasa na wapenzi wa timu hiyo.
  Hata hivyo, jambo la kusikitisha tu ni kwamba hakuna sababu za msingi za kuachwa kwa mlinda mlango huyo, zaidi tu ya kuonekana wamemchoka baada ya kuwa naye kwa muda mrefu.
  Ameachwa; Nahodha wa Simba SC, Juma Kaseja ameachwa 'kiroho mbaya' 

  Kaseja anaachwa Simba SC akiwa bado kipa namba moja wa timu ya taifa, Taifa Stars na anayekubalika mbele ya makocha wengi, hususan wa kigeni.   
  Lakini pia, staili inayotumika kumuacha Kaseja ni sikitisho lingine, kwani anaachwa ‘kiroho mbaya’ licha ya kuitumikia klabu kwa muda mrefu na kwa mafanikio makubwa.
  Juma alistahili kuagwa kwa heshima Simba SC hata kama anatungika glavu zake au anahamia klabu nyingine, kwani kwa vyovyote tayari ameingia kwenye orodha ya magwiji wakubwa wa klabu hiyo.
  Hadi anaachwa, Juma Kaseja amedaka mechi 25 dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga SC tangu ajiunge na Simba mwaka 2003 akirithi mikoba ya aliyekuwa Simba One, Mwameja Mohamed aliyestaafu rasmi mwaka 2002. 
  Kwa kuwa Mwameja alikuwa Tanzania One pia, haikuchukua muda, Kaseja naye akawa Tanzania One, akirithi mikoba ya Manyika Peter, aliyekuwa kipa wa Yanga. Makipa wote hawa watatu, Mwameja, Manyika na Kaseja watakumbukwa kwa mahiri wa kuokoa mikwaju ya penalti. 
  Mechi ya kwanza ya watani Kaseja kucheza ilikuwa Aprili 20, mwaka 2003 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ambayo Yanga ilishinda 3-0, mabao yake yakifungwa na Kudra Omary dakika ya 30, Heri Morris dakika ya 32 na Salum Athumani dakika ya 47.
  Hii ilikuwa mechi maalum ya kirafiki, iliyoandaliwa na promota Dika Sharp kwa kushirikiana na Prime Time Promotions, ambayo ilipewa jina ‘Big Match’
  Mechi ya pili ikafuatia Septemba 28, mwaka 2003, katika Ligi Kuu ambayo iliisha kwa sare ya 2-2, mabao ya Simba yakifungwa na Emmanuel Gabriel dakika ya 27 na 36, wakati ya Yanga yalifungwa na Kudra Omary dakika ya 42 na Heri Morris dakika ya 55.
  Alikuwa Mshauri wa Kiemba asihame Simba; Juma Kaseja alikuwa mshauri wa Amri Kiemba wakati amemaliza Mkataba wake na alimuambia abaki Msimbazi nyota yake ilipong'ara

  Mechi ya tatu ilikuja Novemba 2, mwaka 2003 ya Ligi Kuu, marudiano ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana. 
  Mechi ya nne iliikuja Agosti 7, mwaka 2004, ilikuwa ya Ligi Kuu pia, Simba ikashinda 2-1, mabao ya Shaaban Kisiga ‘Malone’ dakika ya 64 na Ulimboka Mwakingwe dakika ya 76, wakati la Yanga lilifungwa na Pitchou Kongo dakika ya 48.
  Mechi ya tano ilikuja Septemba 18, mwaka 2004 ya Ligi Kuu pia, bao pekee la Athumani Machuppa dakika ya 82, likiipa ushindi Simba.
  Mechi ya sita ilikuja Aprili 17, 2005 na Simba ikashinda tena 2-1, Ligi Kuu Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, mabao yake yakifungwa na Nurdin Msiga dakika ya 44 na Athumani Machupa dakika ya 64, baada ya Aaron Nyanda kutangulia kuifungia Yanga dakika ya 39.
  Mechi ya saba, ilikuja Julai 2, mwaka 2005 ya fainali ya Kombe la Tusker, ilichezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Yanga ikalala 2-0, mabao ya Emmanuel Gabriel dakika ya 60 na Mussa Hassan Mgosi dakika ya 72.
  Mechi ya nane ilikuja Agosti 21, mwaka 2005 ya Ligi Kuu, ambayo Simba ilishinda 2-0, mabao yote yakitiwa kimiani na Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Nico Nyagawa katika dakika za 22 na 56 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
  Mechi ya tisa ilikuja Machi 26, mwaka 2006 ya Ligi Kuu, lakini hiyo iliisha kwa sare ya bila kufungana na mechi ya 10, ilikuja Agosti 15, mwaka 2006, Nusu Fainali ya Kombe la Tusker, ambayo iliisha kwa sare ya 1-1, Emanuel Gabriel akitangulia kuifungia Simba dakika ya 69 na Credo Mwaipopo akaisawazishia Yanga dakika ya 90. Simba ikashinda kwa penalti 7-6.
  Tanzania One; Juma Kaseja anaachwa Simba akiwa kipa namba moja Taifa Stars

  Mechi ya 11 ilikuja Oktoba 29, mwaka 2006, Ligi Kuu ambayo iliisha kwa sare tasa, yaani 0-0 na mechi ya 12 ilikuja Julai 8, mwaka 2007, Fainali ya Ligi Ndogo, ambayo matokeo yalikuwa 1-1 ndani ya dakika 120, Moses Odhiambo akitangulia kuifungia Simba penalti dakika ya pili, kabla ya Said Maulid ‘SMG’ kusawazisha dakika ya 55 na Simba ikashinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
  Mechi ya 13, ilikuja Oktoba 24, mwaka 2007, Ligi Kuu na ilichezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na bao pekee la Ulimboka Mwakingwe, dakika ya 14, lilipa Simba ushindi. Mechi ya 14 ilikuja Aprili 27, ya Ligi Kuu pia, mwaka 2008, ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana
  Mechi ya 15 ilikuja Oktoba 31, mwaka 2009, Kaseja akiwa tayari amerejea Simba SC na akaiongoza timu yake kipenzi kuilaza Yanga 1-0, bao pekee la Mussa Hassan Mgosi dakika ya 26 katika Ligi Kuu.
  Mechi ya 16, ilikuja Desemba 25, mwaka 2009, Nusu Fainali ya Kombe la Tusker na Yanga ilishinda 2-1, mabao ya Jerry Tegete dakika ya 67 na Shamte Ally dakika ya 120, wakati la Simba lilifungwa na Hillary ‘Ford’ Echesa dakika ya 78 kwa penalti.
  Mechi ya 17, ilikuja Aprili 18, mwaka 2010 na Yanga ilichapwa mabao 4-3, Ligi Kuu pia, mabao ya Simba yakifungwa na Uhuru Suleiman dakika ya tatu, Mussa Mgosi dakika ya 53 na 74 na Hillary Echesa dakika ya 90 na ushei, wakati ya wana Jangwani, yalifungwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ dakika ya 30, Jerry Tegete dakika ya 69 na 89.
  Mechi ya 18 ilikuja Oktoba 16, mwaka 2010, Ligi Kuu pia, Yanga ikishinda 1-0 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, bao pekee la Jerry Tegete dakika ya 70, wakati ya mechi ya 19 iliyokuja Machi 5, mwaka 2011, timu hizo zilitoka sare ya 1-1, Stefano Mwasyika akitangulia kuifungia Yanga kwa penalti dakika ya 59, kabla ya Mussa Mgosi kuisawazishia Simba dakika ya 73, ilikuwa ya Ligi Kuu pia.
  Mechi ya 20 ilikuja Julai 10, mwaka 2011, Yanga ilishinda 1-0, Fainali Kombe la Kagame, mfungaji Mghana Kenneth Asamoah dakika ya 108, wakati mechi ya 21 ilikuja Agosti 17, mwaka 2011, Simba ikishinda 2-0, mabao ya Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 15 na Felix Sunzu dakika ya 38 kwa penalti, kuwania Ngao Jamii.
  Mechi ya 22 ilikuja Oktoba 29, mwaka 2011 na Yanga ikashinda 1-0, bao pekee la Davies Mwape dakika ya 75, Ligi Kuu pia, wakati mechi ya 23 ni ile ya 5-0, Mei 6, mwaka 2012, Ligi Kuu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mabao ya Emmanuel Okwi dakika ya pili na 62, Felix Sunzu kwa penalti dakika ya 56, Juma Kaseja kwa penalti dakika ya 67 na Patrick Mafisango (marehemu) kwa penalti pia dakika ya 72. 
  Mechi ya 24 ilikuwa Oktoba 3, mwaka 2012 timu hizo zikitoka sare ya 1-1 katika Ligi Kuu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, tena Yanga wakikomboa bao kwa penalti kupitia kwa Said Rashid Bahanuzi dakika ya 65, baada ya Amri Kiemba kutangulia kufunga dakika ya tatu.   
  Mechi ya 25 na ya mwisho Kaseja kuidakia Simba dhidi ya Yanga, ilikuwa Mei 18, mwaka huu, Simba SC ikilala 2-0 mabao ya Mrundi Didier Kavumbangu dakika ya tano na Mganda Hamisi Kiiza dakika ya 62.
  Ikumbukwe mwaka 2009, Kaseja alikwenda kuichezea Yanga kwa Mkataba wa mwaka mmoja na huko akwadakia wana Jangwani hao mechi moja dhidi ya timu aliyotokea, Aprili 19, mwaka 2009, timu hizo zikitoka sare ya 2-2, mabao ya Simba yakifungwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ dakika ya 23 na Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 62, wakati ya Yanga yalifungwa na Ben Mwalala dakika ya 48 na Jerry Tegete dakika ya 90.
  Hadi anaachwa Simba SC, Kaseja ameiwezesha klabu hiyo kutwaa jumla ya mataji saba, matano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika misimu ya 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2010 na 2012 na matatu ya Tusker, mwaka 2003 na 2005 mawili la Tanzania na Kenya.
  Katika msimu wake wa kwanza, 2003 Simba SC, Kaseja ndio alifanya makubwa zaidi, kwanza akiifikisha timu hiyo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mjini Kampala, Uganda ikifungwa na SC Villa 1-0, bao pekee la Mkenya Vincent Tendwa, pasi ya kiungo Mtanzania, Shaaban Kisiga ‘Malone’.
  Wataungana tena? Juma Kaseja (kulia) alikuwa na Ally Mustafa Barthez (kushoto) Simba kwa miaka kadhaa, je sasa atamfuata Yanga SC?

  Baadaye mwaka huo akaiongoza Simba kufuzu hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa Afrika, ikiitoa timu ngumu, Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa watetezi, akifanya kazi kubwa ya kupangua mikwaju ya penalti baada ya sare ya jumla katika mechi zote mbili.  
  Je, kuachwa kwa Kaseja Simba SC ni mwisho wake kisoka, au ataibukia klabu nyingine? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: JUMA KASEJA ATEMWA 'KIROHO MBAYA' SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top