• HABARI MPYA

    Monday, June 24, 2013

    NYOTA WA ZAMANI TAIFA STARS AFARIKI DUNIA AKIWA NA UMRI WA MIAKA 84

    Stars ya enzi za Mathias Kissa (Picha kwa hisani ya Uhuru)
    Na Boniface Wambura, IMEWEKWA JUNI 24, 2013 SAA 11:30 JIONI
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema lipokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Cosmopolitan na Taifa Stars, Mathias Kissa (84) kilichotokea leo alfajiri (Juni 24 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
    Taarifa ya TFF imesema kwamba, msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani enzi zake, Kissa akiwa na timu ya Tabora alitamba katika michuano ya Kombe la Taifa wakati huo ikiitwa Sunlight Cup. Alikuwa akicheza katika nafasi ya ulinzi.
    Baadaye alijiunga na Cosmoplitan ya Dar es Salaam, na pia kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ambapo enzi zake akiwa na wachezaji kama Yunge Mwanansali wakiiwakilisha Tanganyika na baadaye Tanzania Bara walitamba katika michuano ya Kombe la Chalenji wakati huo ikiitwa Gossage, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
    Kissa ambaye alipata tuzo ya mchezaji bora wa karne kwa upande wa Tanzania, tuzo inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) alikuwa ndiye mchezaji msomi kupita wote wakati akichezea timu ya Taifa akiwa amehitimu elimu ya Darasa la Kumi.
    Kwa mujibu wa binti yake, Erica, marehemu ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi (stroke) alioupata miaka mitano iliyopita, na kisukari. Baadaye alipata kidonda ambacho ndicho kilichosababisha kifo chake.
    Msiba uko nyumbani kwa marahemu, Masaki, Mtaa wa Ruvu karibu na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) na mazishi yatafanyika keshokutwa, Jumatano (Juni 26 mwaka huu) kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
    TFF imesema inatoa pole kwa familia ya marehemu Kisa, Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Cosmopolitan na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Kisa mahali pema peponi. Amina
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NYOTA WA ZAMANI TAIFA STARS AFARIKI DUNIA AKIWA NA UMRI WA MIAKA 84 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top