• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 19, 2013

  KAPTENI HANS POPPE AMVULIA KOFIA ALHAJ KIBADENI, ASEMA SIMBA SC ITATISHA MSIMU UJAO

  Ndani ya Kinesi; Hans Poppe
  akiwa mazoezini Kinesi leo
  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JUNI 19, SAA 12:25 JIONI
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameridhishwa na kazi anayoifanya Kocha Mkuu mpya wa klabu hiyo, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na amesema ana matumaini naye sana.
  Akizungumza baada ya mazoezi ya leo jioni kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam, Milionea huyo amesema kwamba King Kibaden anafanya kazi nzuri yenye kutia matumaini. 
  “Nimefika mazoezini leo, nimeona kazi inayofanywa na Kibaden na benchi lake zima la Ufundi, kwa kweli inatia matumaini na kinachotakiwa ni sisi wana Simba wote kumpa sapoti na muda si mrefu Simba SC itarejesha heshima yake,”alisema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
  Poppe amesema uongozi umeamua kumkabidhi masuala yote ya ufundi Kibadeni na utamtekelezea mapendekezo yote atakayoyatoa katika kukamilisha programu zake.
  Poppe aliyerejea Jumapili nchini kutoka Tunisia alipokwenda kufuatilia fedha za mauzo ya mshambuliaji Mganda, Emanuel Okwi katika klabu ya Etoile du Sahel ya huko yuko katika harakati za kuhakikisha Simba inakuwa imara msimu ujao.
  Anatia matumaini; King Kibaden kazini Simba SC

  Na leo amekwenda Kinesi ili kuona maendeleo ya timu kwa ujumla na wachezaji, hususan wale wapya waliosajiliwa kutoka timu mbalimbali katika kujaribu kutathmini kikosi cha msimu ujao.
  Wachezaji wote kwa ujumla wa Simba SC wapo mazoezini, ispokuwa waliokuwa katika timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Uganda kwa mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwishoni mwa wiki. 
  Simba imepania kujiimarisha chini ya kocha mpya, mshambuliaji wake nyota wa zamani King Kibadeni baada ya kupitia msimu mbaya uliopita ikipokonywa ubingwa wa Ligi Kuu na kukosa japo nafasi ya pili ya kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho.
  Ikiwa imepania kurejesha heshima msimu ujao, Simba inaonekana kuwa makini mno katika usajili na uuundaji mzima wa kikosi cha msimu mpya.
  Tayati imekwishasajili wapya kadhaa kuboresha timu, wakiwemo kipa Andrew Ntalla, Issa Rashid, Zahor Pazi, Mganda Samuel Ssenkoom, Adeyoum Saleh Ahmed na bado inapepesa macho kusaka nyota zaidi wa kurejesha heshima yake msimu ujao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KAPTENI HANS POPPE AMVULIA KOFIA ALHAJ KIBADENI, ASEMA SIMBA SC ITATISHA MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top