VIGOGO wa Hispania, Real Madrid wametangaza katika tovuti yao kuingia Mkataba wa miaka mitatu na kocha Mtaliano, Carlo Ancelotti ambaye atatambulishwa kwa Waandishi wa Habari Jumatano.
Real Madrid imethibitisha Carlo Ancelotti ataondoka Paris Saint-Germain kuja kurithi mikoba ya Jose Mourinho aliyeondoka mapema mwezi huu.Madrid iliamua mara moja kumchukua Ancelotti, kufuatia Mourinho kutimkia Chelsea, lakini PSG awali iligoma kumuachia kocha huyo mwenye umri wa miaka 54.Hata hivyo, wamekubali sasa kumruhusu Ancelotti kuondoka baada ya kumteua Laurent Blanc kurithi mikoba yake, ambaye wamemtangaza leo.
"Real Madrid itamtambulisha Carlo Ancelotti kama kocha wao mpya kwa misimu mitatu ijayo, Jumatano ya Juni 26,"imesema taarifa ya klabu hiyo katika tovuti yao.
"Shughuli itafanyika Santiago Bernabeu katika Royal Box saa 7:00 mchana.  Kisha Carlo Ancelotti atakuwepo mapema."
Ancelotti amekuwa kocha wa PSG tangu Desemba 2011 na ameiongoza timu hiyo kutwaa taji lao la tatu laLigue 1 kihistoria kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 19.
Awali alizifundisha kwa mafanikio Chelsea na AC Milan, wakati pia alifundisha Juventus, Parma na Reggiana katika hatua zake za mwanzoni za ukocha.