• HABARI MPYA

  Alhamisi, Juni 20, 2013

  OLOYA AOTA MBAWA SIMBA SC, HASIRA ZA HANS POPPE SASA KUSAJILI WAKALI WENGINE WAWILI WA KIGENI

  Labda baadaye; Oloya kwa sasa anaendelea kucheza Vietnam amesema atakuja Simba SC Oktoba
  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JUNI 20, 2013 SAA 10:30 JIONI
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Moses Oloya ameahidi kujiunga na Simba SC kuanzia Oktoba mwaka huu, baada ya kumaliza wake wa sasa na klabu ya Saigon Xuan Thanh ya Vietnam.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba amekwishafanya mazungumzo na Mganda huyo na wamefikia makubaliano juu ya kila kitu kuhusu usajili wake, lakini ameomba amalize kwanza Mkataba wake aje akiwa mchezaji huru.
  Analeta mashine mpya; Hans Poppe amesema anasajili wageni wengine wawili tishio

  “Tumekubaliana kila kitu na hadi jana baada ya kuvuma habari amesanini Yanga nimempigia simu na nimezungumza naye amesema hajasaini anarejea Vietnam na atakuja kusaini kwetu kama tulivyokubaliana,”alisema Hans Poppe. 
  Mjumbe huyo wa Kamati ya Utendaji pia S.S.C., amesema kwamba baada ya kuona uwezekano wa kumsaini kwa sasa mchezaji huyo aliyezaliwa miaka 20 iliyopita ni mgumu, wameamua kusaka mshambuliaji mwingine wa kigeni badala yake, lakini mwenye uwezo kama wake.
  Poppe amesema pamoja na mshambuliaji, pia wanasaka beki mwingine wa kati wa kigeni mwenye uwezo mkubwa.
  “Tutasaini hao wawili wengine twende nao hadi baada ya mzunguko wa kwanza tuone. Maana tutakuwa na wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni, kwani tayari tunao Abbel Dhaira, Mussa Mudde na Samuel Ssenkoom (wote Waganda), hivyo tukiongeza wawili watakuwa watano,”alisema.
  Alipoulizwa kuhusu nafasi ya Oloya, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema; “Ni kipindi kirefu sana hadi dirisha dogo, kuna kuuza watu hapa katikati au hata kuacha, kama mtu unaona hana msaada kwa timu, unamuengua unaweka Oloya aje kuwapa raha wana Simba,”alisema.
  Simba ikimpata Oloya aliyekwenda Vietnam akitokea KCC ya kwao, aliyoichezea tangu mwaka 2009 hadi 2010, itakuwa imelamba dume.
  Oloya ni mchezaji mzuri kuliko Emmanuel Okwi ambaye Simba SC imemuuza Etoile du Sahel ya Tunisia na Januari mwaka huu, Yanga SC na Azam zote zilijaribu kutaka kumsajili bila mafanikio Desemba mwaka jana.
  Mwishowe Azam ikaona bora kumsajili Mganda mwingine, Brian Umony, wakati Yanga ilibanwa na nafasi ya idadi ya wachezaji wa kigeni, lakini ikamuweka kwenye orodha ya wachezaji inayoweza kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: OLOYA AOTA MBAWA SIMBA SC, HASIRA ZA HANS POPPE SASA KUSAJILI WAKALI WENGINE WAWILI WA KIGENI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top