• HABARI MPYA

  Alhamisi, Juni 20, 2013

  RAIS JK, SUNDERLAND NA MPANGO WA AKADEMI YA KISASA DAR, WANAZIJUA SIMBA NA YANGA? WAMUULIZE KIPINGU

  Rais Kikwete akiwa na watoto wa akademi ya Sunderland pamoja na Mwenyekiti wa klabu hiyo

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JUNI 20, 2013 SAA 4:30 ASUBUHI
  BEKI Kolo Toure alijiunga na Arsenal Februari mwaka 2002 akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast kwa ada ya uhamisho ya Pauni 150,000 baada ya kufanya majaribio ya muda mfupi sana Highburry (sasa Emirates), kufuatia Arsene Wenger kuvutiwa na mchezaji huyo alipomuona katika Fainali za Mataifa ya Afrika, bado kinda sana.
  Hata hivyo, Toure alilalizimika kusubiri hadi msimu uliofuata kucheza mechi ya kwanza  katika kikosi cha kwanza na ilikuwa ni dhidi ya Liverpool katika Ngao ya Jamii, Agosti mwaka 2002 na tangu hapo akawa mchezaji wa kutumainiwa kikosini hadi alipohamia Manchester City na sasa anaelekea kumalizia soka yake Liverpool.
  Ametokea katika akademi ya ASEC ambako wametokea nyota wengine wa Ivory Coast wanaokula maisha Ulaya akina Bonaventure Kalou, Didier Zokora, Emmanuel Eboue, Gervinho, Salomon Kalou, Romaric, Didier Ya Konan na mdogo wake, Yaya.
  Akademi ya ASEC inatambulika kama lulu katika soka ya Afrika, ambayo ilianzishwa na Roger Ouegnin na Jean-Marc Guillou mwaka 1993 katika viwanja vya mazoezi vya ASEC na tangu hapo imezalisha nyota wengi wa kimataifa. 
  Utaratibu wa hapo, wanafunzi wanakuwa wanapewa elimu pamoja na kufundishwa michezo, wakifundishwa masomo ya Hesabu, Historia, Jiografia, Fizikia, Kifaransa, Kiingereza na Kispanyola. 
  Yussuf Bakhresa akizungumza na beki wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Rigobert Song ambaye kwa sasa ni Meneja wa timu hiyo. watu aina hii ndiyo wanaweza kuisaidia akademi ya Azam kufikisha wachezaji Ulaya. 

  Wanasoma na kufanya mazoezi mara mbili kwa siku pamoja na kucheza mechi kila Jumamosi na wanaangaliwa kwa makini juu ya mwenendo wao mzima pamoja na afya.
  Hiki ni kitu ambacho Watanzania wenye mitazamo ya mbali, kama Iddi Kipingu walikiona mapema na wakaona wanahitaji kuwa na kitu kama hicho nyumbani.
  Miaka michache baadaye tangu kuanzishwa kwa akademi ya ASEC, Tanzania nao wakapata akademi moja nzuri sana ambayo ilikuwa na mwanzo mzuri, hiyo ni sekondari ya Makongo, enzi zile chini ya Iddi Kipingu.
  Kipingu alikuwa ana timu yake ya wataalamu waliokuwa wanazunguka sehemu mbalimbali nchini kusaka vijana wenye vipaji na kuwaingiza katika shule hiyo inayomilikiwa na Jeshi kuwaendeleza kimichezo na elimu pia na ndani ya muda mfupi, ikawa tegemeo la taifa katika kuzalisha wachezaji wa timu za taifa.
  Ikafikia hadi wachezaji wakawa wanajisingizia; “Mimi natokea Makongo” wakijua ndiyo njia rahisi ya kupata timu.
  Kipingu aliiboresha zaidi Makongo akaajiri hadi walimu marufu wa kigeni, kama Mkongo Tambwe Leya na Mnigeria Ernest Mokake, wote sasa marehemu ambao hakika walifanya kazi nzuri sana.
  Shule nyingine za Jeshi kama Jitegemee na Lugalo nazo zikaiga mfumo wa Makongo na kwa hakika tulifanikikwa kuzalisha vipaji vingi miaka ya katikati, lakini mambo mawili makubwa yalitukwamisha uongozi mbovu wa soka na kukosekana kwa mwendelezo mzuri.
  Viongozi wa soka ya nchi hii walishindwa kumpa sapoti Kipingu na mradi ule, badala yake wakataka kuitumia shule hiyo kama bwalo la kuzalisha wachezaji wa kuchezea timu zao, Simba na Yanga.
  Marehemu Talib Talib, alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na wakati huo kiongozi wa timu ya jeshi la Magereza mwaka 1998- akachukua vijana kibao wa Makongo waliokuwa katika timu ya taifa ya Vijana na kuwapeleka katika timu ya jeshi hilo, Prisons ya Mbeya.
  Aliwasaidia ajira jeshini, lakini hiyo haikuwa dira ya Kipingu- bali ilikuwa ni kufuata nyayo za ASEC kuhakikisha anakuwa na vijana wanaocheza Ulaya, ili baadaye waje kuisaidia timu ya taifa.
  Abedi Pele akiwa na vijana wa akademi ya Azam Chamazi

  Tajiri aliyeanzisha Moro United, Merey Balhabou naye akachukua nyota wengine kibao mwaka 2001 kutoka Makongo na kutoka hapo, basi ikawa shule hiyo inazalisha wachezaji wa kuchezea timu za Bara na si ndoto za Ulaya tena.
  Kabla ya kwenda Simba, Haruna Moshi akaanzia Coastal Union ya Tanga na Boniface Pawasa akaanzia CDA ya Dodoma kabla ya kutua Msimbazi.
  Vijana wakapoteza dira waliyowekewa Makongo- wakawa wanacheza kutafuta nafasi za kutua Simba au Yanga na si kwenda Ufaransa tena, ambako wachezaji wengi wa Afrika wanaanzia maisha huko.  
  Rais Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na Mwenyekiti na Mmiliki wa klabu ya Sunderland ya England nchini humo, Ellis Short na akaomba na kukubaliwa kujengewa akademi ya kisasa Dar es Salaam. 
  Klabu hiyo kwa ushirikiano na Symbion Power Tanzania Limited imekubali kujenga akademi ya soka mjini Dar es Salaam kufuatia ombi la Rais Kikwete, aliyekuwa London kwa ziara ya kikazi ya siku tatu mwishoni mwa wiki. 
  Rais JK ni mkereketwa wa michezo na alitamani sana kuona timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars japo inacheza Fainali moja za Mataifa ya Afrika akiwa Ikulu na amefanya jitihada kubwa sana- sijui atakayerithi nafasi yake kama ataendeleza juhudi hizo. 
  Lakini mpango kama huu wa akademi ni hatua moja kubwa sana ya kimaendeleo na ambayo siku moja itakuja kuinufaisha nchi. 
  Siku zote naandika, tunazalisha vijana wengi sana kutokana na mashindano ya vijana kama Copa Coca Cola, Airtel Rising Star na mengineyo, lakini tatizo wanakosa mwendelezo na hawafiki popote na siku zote tunaendelea kulia kilio kile kile.   
  Iddi Kipingu kulia akiwa na rais wa TFF, Leodegar Tenga

  Wazi akademi hii ya JK na Sunderland, ile ya Azam na ile aliyoanzisha Kipingu baada ya kutoka jeshini, ni sehemu mwafaka za kuendeleza vijana na kuzalisha wachezaji wa kucheza Ulaya baadaye.
  Lakini ili tufanikiwe lazima tuzingatie dira halisi na si kurudi kule kule, kuzalisha vijana wa kucheza Simba na Yanga- kutokana na miradi hii ambayo inagharimu fedha nyingi.
  Mwanasoka Bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele alipotembelea akademi ya Azam, kule Chamazi aliitamani sana na akasema ile ni akademi bora kuliko hata nyingi za Ulaya.
  Pele akaitabiria makubwa Azam miaka ya baadaye- kwamba itakuwa bora kuliko klabu za Ulaya na uzuri mchezaji wa Azam hawezi kwenda Simba au Yanga, hadi wenye timu yao waamue.
  Ila, wakati umefika Azam akademi iwe na Mtendaji Mkuu mwenye sifa za kimataifa ambaye atasaidia kuwatoa vijana pale Chamazi hadi Ulaya, vinginevyo utakuwa mradi usio na matunda na utafika wakati utakuwa mzigo kwa wawekezaji wenyewe. 
  Lakini pia, ile akademi inahitaji Mwalimu tena wa kiwango cha juu kuliko mwalimu wa Azam A, kwa sababu ule ndiyo msingi mkuu wa kuwalipa wawekezaji hao, kuliko chochote katika mradi ule wa Chamazi.
  Akademi ya Azam pale ilipo haitakiwi kusubiri kufikiwa, bali inahitaji kutafuta namna ya kuwafikisha vijana wake Ulaya kwa ajili ya kujitangaza kwanza na ndipo baadaye ianze kujiuza.
  Athumani Iddi 'Chuji' wa Yanga kushoto akimenyana na Amri Kiemba wa Simba SC kulia. Wote hawa wangeweza kucheza Ulaya, ila 'watafia' Simba na Yanga zao.

  Naamini sana juu ya wamiliki wa Azam, Yussuf Bakhresa mmoja wa wakurugenzi wa bodi ya kabu hiyo na wakala wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ni mweledi sana na ni mtu wa mipango, wasiwasi ni hiyo akademi inayokuja ya JK na Sunderland kama haitakuwa bwalo za kuzalisha wachezaji wa kucheza Simba na Yanga. Kama ni reli ya kati, basi kwa leo hapa ndiyo Kigoma. Siku njema waungwana. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: RAIS JK, SUNDERLAND NA MPANGO WA AKADEMI YA KISASA DAR, WANAZIJUA SIMBA NA YANGA? WAMUULIZE KIPINGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top