• HABARI MPYA

  Jumapili, Juni 23, 2013

  JUNI NDIYO HII INAYOYOMA, MBONA HATUONI KITU JANGWANI, KULIKONI MANJI!

  IMEWEKWA JUNI 23, 2013 SAA 1:00 ASUBUHI
  MARA tu baada ya kuingia madarakani, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage alitoa ahadi ya kuijengea Uwanja wa kisasa klabu eneo la Bunju na kiwanja kwa ajili ya mradi huo tayari kipo, kimelipiwa.
  Rage alisema ameingia Mkataba na kampuni ya Waturuki kujenga Uwanja huo na akamtambulisha hadi mwakilishi wa kampuni hiyo mbele ya Waandishi wa habari na kuonyesha ramani nzuri sana.
  Miaka imekatika hakuna cha Uwanja wala nini na zaidi imegundulika Simba SC haina kiwanja na kwa kuwa wanachama na wapenzi wa klabu hiyo wamezoea propaganda za viongozi wao na zaidi wanajali matokeo ya uwanjani, basi wameamua kujiridhisha walipigwa changa la macho na Mwenyekiti wao.

  Mwishoni mwa mwaka jana, Mwenyekiti wa Yanga naye, Alhaj Yussuf Mehboob Manji alitoa ahadi ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa, ulipo Uwanja wa sasa wa klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
  Mwaka huu, awali Manji alitangaza kufikia makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing Constructions Engineering Group iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja huo mpya wa Yanga.
  Baadaye, miezi miwili iliyopita kampuni hiyo iliwasilisha ramani za viwanja kadhaa, Yanga SC iachague moja, ili zoezi la ujenzi wa Uwanja huo lianze.
  Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ujenzi huo wa Uwanja utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 hadi 40,000 umepangwa kuanza rasmi mwezi ujao.
  Wakati Manji anatoa ahadi hiyo Desemba mwaka jana kwamba ujenzi utaanza Juni, ilikuwa muda kidogo- lakini leo naandika makala haya ni siku 23 ya Juni na hadi sasa Kaunda ipo kama alivyoiona kwa mara ya mwisho, marehemu Rashid Ngozoma Matunda kabla ya kifo chake.
  Kuanzia Juni 1, macho ya watu hususan wapenzi wa Yanga yamekuwa yakimulika pale Jangwani kuangalia kama zoezi la ujenzi limeanza, lakini hadi leo bado.
  Ukweli ni kwamba, watu wengi hawana imani na ahadi hiyo kama itatekelezwa kutokana na ukweli halisi wa gharama za ujenzi wa Uwanja na hali ya kiuchumi ya klabu.
  Yanga haina uwezo kifedha kama klabu kujenga Uwanja- labda ipewe mkopo, na ni nani au taasisi gani itakayoipa mkopo mkubwa wa kuweza kujenga Uwanja wa klabu hiyo? Hilo ndilo swali.
  Ni swali tu, inawezekana Yanga wana mipango yao na inakwenda vizuri, pengine bila shaka magari ya vifaa vya ujenzi yamekwishaanza kuelekea Jangwani.
  Manji ni tajiri, mpenzi na mwanachama wa Yanga. Anaweza kutoa fedha yake ya mfukoni kuijengea Uwanja Yanga? Na ana kiwango cha fedha za kutosha kutoa kugharamia ujenzi na asiyumbe kiuchumi? Hayo ni maswali ambayo pengine wengi wengine wanajiuliza hivi sasa.
  Hakuna asiyejua kama Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa, mmiliki wa Azam FC ni tajiri, lakini mwisho wa siku tumeuona Uwanja alioujenga kwa ajili ya timu yake pale Chamazi. 
  Yanga wanataka kujenga Uwanja wa hadhi zaidi ya huo wa Chamazi. Hapo ndipo ulipolalia wasiwasi wa wengi juu ya zoezi hilo. Lakini inawezekana ukawa ni wasiwasi tu, Yanga SC na Manji wana mpango kamili ambao sasa unaelekea katika hatua za utekelezaji wake tu.   
  Ikumbukwe pia, Manji alitangaza mpango wa kulikarabati na jengo dogo la klabu hiyo, liliopo Mtaa wa Mafia na kuwa jengo la kitegauchumi la klabu, akaunda Kamati chini ya Mwenyekiti, Ridhiwani Kikwete kusimamia zoezi hilo.
  Hadithi za ujenzi wa Uwanja mpya Yanga SC, ukarabati wa jengo la Mafia sasa ni maarufu masikioni mwa wengi, zikisimuliwa na wasimulizi tofauti kuanzia enzi za akina Tarimba Abass wanaongoza klabu hiyo.
  Na zimeendelea hata wakati wa uongozi uliopita wa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga, lakini suala la utekelezaji wake ndilo limekuwa gumu.
  Kuna sababu za kumuamini Manji, kwa sababu kila ukiitazama Yanga ya leo, bila ya yeye ngumu kupata picha ingekuwaje.
  Manji aliingia Yanga mwaka 2006 baada ya jitihada zilizofanywa na wanachama wa klabu hiyo akina Theonist Rutashoborwa (sasa marehemu), Mzee wa Mpunga, Mawakili Lugaziya na Matunda na baadhi ya Waandishi wa Habari za michezo wenye mapenzi na klabu hiyo, kuanzisha harambee ya Saidia Yanga, kufuatia hali mbaya ya kiuchumi kukithiri ndani ya klabu hiyo, chini ya uongozi wa Francis Kifukwe.
  Katika kutafuta misaada ya kuibeba timu wakati huo ipo kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame ndipo wakampata Manji naye kwa mapenzi yake, akasema; “Nitaubeba mzigo wote”, na kweli hadi leo, amekuwa akiilea Yanga tangu kama mfadhili hadi sasa Mwenyekiti.
  Hadi sasa, Manji ameingia kwenye historia Yanga kama miongoni mwa watu muhimu kuwahi kutokea kwenye klabu hiyo, bila hata ya ahadi ya Uwanja. Bila shaka hata wana Yanga pia na Watanzania wengi wanamuamini na kumuheshimu Manji.
  Na kwa sababu hiyo, ipo haja ya kuepuka ahadi yake kufananishwa na ya Rage. Juni ndiyo hii inayoyoma, mbona hatuoni kitu Jangwani? Wikiendi njema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: JUNI NDIYO HII INAYOYOMA, MBONA HATUONI KITU JANGWANI, KULIKONI MANJI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top