• HABARI MPYA

    Friday, April 12, 2013

    AGGREY MORRIS, NYONI NA WENZAO WOTE WALIOSIMAMISHWA WAINGIA KAMBINI AZAM KUJIANDAA KUUA MNYAMA JUMAPILI

    Erasto Nyoni kulia na Aggrey Morris kushoto, wakiwa Chamazi jana

    Na Mahmoud Zubeiry
    WACHEZAJI wanne wa Azam FC waliokuwa wamesimamishwa tangu Novemba mwaka jana, kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Said Mourad, Erasto Nyoni na Aggrey Morris jana wameingia kambini katika hosteli za klabu hiyo, Azam Complex, Chamazi kujiandaa na mechi dhidi ya Simba SC keshokutwa.
    Azam FC, imewarejesha kundini wachezaji wake hao iliyowasimamisha kwa tuhuma za kuihujumu timu hiyo katika mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC, ambayo Wekundu wa Msimbazi walishinda mabao 3-1, baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kukamilisha uchunguzi wao na kubaini hawakuhusika.
    Katibu wa Azam, Nassor Idirsa aliiambia BIN ZUBEIRY jana Chamazi kwamba, wachezaji wote wameitikia wito wa kurejea kwenye timu na tayari wameingia kambini kwa ajili ya mchezo wa Jumapili.
    BIN ZUBEIRY iliwashuhudia wachezaji hao wakiwa Chamazi jana. Pamoja na kusimamishwa, Nyoni na Morris waliendelea kuitwa Taifa Stars na kuendelea kufanya vizuri, licha ya kutocheza mechi za ushindani.
    Dida na Mourad, wao walikuwa wakifanya mazoezi tu kwenye maskani zao na kucheza mechi za ‘ndondo’ ili kujiweka fiti wakisubiria hatima zao.
    Azam FC ilipunguza ‘gepu’ la pointi inazozidiwa na vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC hadi kubaki tatu, kufuatia ushindi wa mabao 3-1 jioni ya leo dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
    Yanga ina pointi 49 kileleni, Azam inafuatia ikiwa na 46, Kagera Sugar yenye 37 ni ya tatu na Simba ambao ni mabingwa watetezi, wanashika nafasi ya nne kwa pointi zao 35.
    Mabao ya Azam katika mchezo wa leo, yalitiwa kimiani na Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya tisa na Kipre Herman Tchetche dakika za 28 na 61, wakati la Lyon lilifungwa na Adam Kingwande dakika ya 36.
    Pamoja na kufungwa, Lyon ilionyesha upinzani kwa Azam FC na kufanya mchezo uwe mtamu.
    Kipigo hicho kinazidi kuiweka Lyon katika hatari ya kushuka daraja, ikibaki na pointi zake 19, baada ya kucheza mechi 23 na sasa ni miujiza tu itakayoifanya timu hiyo iendelee kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
    Azam itashuka tena dimbani Jumapili, kumenyana na mabingwa watetezi Simba SC katika mfululizo wa ligi hiyo, wakati kesho Yanga itacheza JKT Oljoro Uwanja wa Taifa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AGGREY MORRIS, NYONI NA WENZAO WOTE WALIOSIMAMISHWA WAINGIA KAMBINI AZAM KUJIANDAA KUUA MNYAMA JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top