• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 19, 2013

  DIHILE AWAWEKEA NADHIRI YANGA SC, ASEMA JUMAPILI HAWATOKI TAIFA

  Shaaban Dihile aliyedaka mpira juu

  Na Princess Asia
  KIPA wa JKT Ruvu, Shaaban Dihile amesema kwamba Yanga SC watawahakikishia kubaki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Dihile amesema kwamba wataifunga Yanga SC Jumapili na kufikisha pointi 26, ambazo zitawafanya wawe salama na kujiondoa kwenye hatari ya kushuka Daraja.
  “Tunawajua Yanga, tena vizuri sana. Siku hiyo Taifa patachimbika, lazima tuwafunge watake wasitake, na watu watashangaa siku hiyo, tutapiga mpira wa hatari sana,”alisema.
  Dihile alisema JKT Ruvu ni timu nzuri tu ila kuyumba kwao msimu huu kumetokana na sababu mbalimbali ambazo tayari zimekwishashughulikiwa na hali imekuwa shwari tena.
  “Sasa hivi tupo kambini tunajifua vikali sana. Kila mchezaji anaitazama hiyo mechi kama ya ukombozi kwetu na hakutakuwa na mzaha hata kidogo siku hiyo. Tutapiga ile soka ya kijeshi haswa,”alisema Dihile.
  JKT Ruvu ina pointi 23 kwa sasa ikiwa katika nafasi ya 11 na inapambana kutoka kwenye orodha ya timu tatu za kushuka Daraja.
  Hivi karibuni, timu hiyo ilibadilisha uongozi na benchi la ufundi, kocha Charles Kilinda aliyekaa na timu hiyo kwa misimu mitatu akiondolewa na sasa Kocha Msaidizi, Azishi Kondo ameshika mikoba. 
  Kwa upande wa Yanga, inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 53, baada ya kucheza mechi 23 ikiwa inahitaji pointi sita katika mechi zake tatu zilizobaki kujihakikishia ubingwa.
  Baada ya JKT Ruvu, Yanga itacheza na Coastal Union Mei 1 na Simba SC Mei 18.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: DIHILE AWAWEKEA NADHIRI YANGA SC, ASEMA JUMAPILI HAWATOKI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top