• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 23, 2013

  KAVUMBANGU SASA FITI, AANZA TENA KAZI JANGWANI KESHO

  Usafiri kuelekea nje ya Uwanja; Kavumbangu akitolewa kwa machela baada ya kuumia dhidi ya Oljoro

  Na Mahmoud Zubeiry
  MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Mrundi Didier Kavumbangu aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu, anatarajiwa kuanza mazoezi kesho baada ya kupona, ili kujiandaa na mechi mbili za mwisho za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Mrundi huyo aliumia katika mechi dhidi ya JKT Oljoro, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 13, mwaka huu timu yake ikishinda 3-0 na tangu hapo amekosa mechi mbili dhidi ya JKT Mgambo Tanga 1-1 na JKT Ruvu Dar es Salaam Yanga ikishinda 3-0.
  Lakini baada ya matibabu, Kavumbangu aliye katika msimu wake wa kwanza Yanga SC anatarajiwa kuanza mazoezi kesho. Mbali na Kavumbangu, mchezaji mwingine majeruhi Yanga, beki Juma Abdul naye anatarajiwa kuanza mazoezi Ijumaa.
  Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu, Yanga iliwapa wachezaji wake mapumziko ya siku mbili jana na leo na kesho wanarudi kazini.
  Kumbuka, Yanga SC ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 56 na inaweza kutangaza ubingwa katika mchezo wake ujao dhidi ya Coastal Union, Mei 1, mwaka huu Uwanja wa Taifa, ikishinda. Lakini Yanga wanaweza pia kusherehekea ubingwa nje ya Uwanja iwapo Azam FC itafungwa au kutoa sare na Coastal Union Tanga Ijumaa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KAVUMBANGU SASA FITI, AANZA TENA KAZI JANGWANI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top