• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 19, 2013

  YONDAN ATAKA KUONDOKA YANGA SC AKATAFUTE MAISHA MBELE

  Kevin Yondan

  Na Mahmoud Zubeiry
  BEKI wa Yanga SC, Kevin Yondan amesema kwamba kwa sasa akili yake ni kucheza Ulaya au nchi nyingine yoyote ambako atapata maslahi makubwa kuliko Tanzania.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Yondan amesema kwamba anaomba sana ajitokeze wakala wa ukweli atakayemsaidia kupata timu nje itakayompa maslahi makubwa.
  “Kweli sasa uwezo wangu umekuwa mkubwa sana, hata wachezaji wenzangu wananiambia hivyo. Hata mimi nina hamu ya kutoka sasa nikacheze soka yenye manufaa zaidi,”alisema.
  Hata hivyo, Yondan alisema kwamba tatizo bado hajatokea wakala wa maana wa kumsaidia kutimiza ndoto zake na hana shaka wakati utafika tu na mambo yatajipa.
  Yondan kwa sasa ni sentahafu chaguo la kwanza la klabu yake, Yanga SC aliyojiunga nayo msimu huu akitokea kwa mahasimu, Simba SC na timu ya taifa pia, Taifa Stars.  
  Mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta aliwahi kusema baada ya mechi kati ya Tanzania na Morocco kwamba Yondan ni mtu wa kucheza popote duniani.
  Mbwana alimwagia mno sifa beki huyo mzaliwa wa Mwanza na kusema kwamba iwapo ataongeza juhudi, siku si nyingi atafanikiwa kupata timu nje ya kumlipa vizuri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YONDAN ATAKA KUONDOKA YANGA SC AKATAFUTE MAISHA MBELE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top