• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 27, 2013

  HAIKUWA KAZI RAHISI YANGA KUTWA UBINGWA MSIMU HUU

  Mabingwa; Wachezaji wa Yanga wakipongezana baada ya mechi yao iliyopita na JKT Ruvu

  Na Mahmoud Zubeiry
  HATIMAYE ndoto za klabu kongwe zaidi nchini, Yanga SC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2012/2013 zimetimia jana, kwa kuwa pointi zake 56 sasa haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote. 
  Yanga yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu jana, kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa ligi hiyo baina ya wenyeji Coastal Union na Azam FC ya Dar es Salaam, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Matokeo hayo yanamaanisha, Azam FC waliokuwa washindani wakuu wa Yanga SC yenye pointi 56, hawawezi tena kufikisha pointi hizo ambazo wanazo mabingwa hao wapya, kwani hata wakishinda mechi zao nyingine  mbili zilizobaki, watamaliza na pointi 54. 
  Mchezaji aliyepeleka shangwe na vigelegele Jangwani ni Danny Lyanga, ambaye aliifungia Coastal bao la kusawazisha dakika ya 72. 
  Lyanga ambaye ilibaki kidogo asajiliwe Yanga msimu huu kutoka Toto Africans, kama si kuzidiwa kete na Coastal, alifunga bao hilo katika mpira wake wa kwanza kuugusa tangu aingie kuchukua nafasi ya Suleiman Kassim ‘Selembe’ dakika ya 71.
  Alifunga bao hilo, baada ya kupokea pasi nzuri ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Pius Kisambale, ambaye ni mdogo wa kiungo wa Wana Jangwani hao, Athumani Iddi ‘Chuji’.
  Azam ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika mchezo huo, lililofungwa na beki Aggrey Morris kwa penalti dakika ya 60, baada ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Gaudence Mwaikimba kuchezewa rafu kwenye eneo la hatari  na beki Yussuf Chuma- na refa Andrew Shamba wa Pwani akaamuru pigo hilo.
  Matokeo hayo yanakuwa sawa na Coastal kulipa fadhila kwa Yanga, kwani hata wao, ubingwa wao pekee wa Ligi Kuu waliochukua mwaka 1988 ulitokana na ‘msaada’ wa wana Jangwani huo.
  Msimu huo, mshindani wa Coastal katika mbio za ubingwa alikuwa Simba SC ambaye ili kutwaa taji hilo, alihitaji kushinda mechi ya mwisho dhidi ya African Sports mjini Tanga huku akiomba Wagosi wa Kaya walale mbele ya Yanga Uwanja wa Taifa.
  Lakini Yanga wakacheza ‘kichovu’ na Athumani China akaenda kupiga penalti ‘kiviivu’ akakosa, Coastal ikishinda 2-0 na kusherehekea taji pekee la ubingwa wa Ligi Kuu, licha ya Simba pia kushinda 3-0 dhidi ya Sports Tanga. 
  Hili linakuwa taji la 24 kwa Yanga, tangu watwae kwa mara ya kwanza mwaka 1968.
  Kikosi cha ubingwa...

  SAFARI YA UBINGWA YANGA SC…
  Yanga SC imetwaa ubingwa baada ya kucheza mechi 24, ikishinda 17, sare tano na kufungwa mbili, zote ugenini dhidi ya Wakata Miwa, Kagera Sugar 1-0 na Mtibwa Sugar 3-0 Morogoro.
  Pamoja na Azam kutaka kujaribu kupambana na Yanga SC, lakini ilikuwa kazi ngumu kwani hata kama wangeshinda jana dhidi ya Coastal na mabingwa hao wapya wakafungwa mechi zao zote, bado walikuwa wanajivunia wastani mzuri mno wa mabao ya kufunga na kufungwa. 
  Azam walihitaji kufunga mabao 10 katika mechi tatu- wasifungwe hata moja na Yanga isifunge hata moja na ifungwe mechi zote, ndio wawe mabingwa kwa tofauti ya mabao. Ingewezekana, lakini lisingekuwa jambo jepesi.
  Yanga SC imetwaa ubingwa wa Bara baada ya kupitia mikononi mwa makocha wawili, Mbelgiji Tom Saintfiet aliyeanza kabla ya kutimuliwa baada ya mechi tatu, na nafasi yake kuchukuliwa na Mholanzi, Ernie Brandts.  
  Saintfiet aliiacha Yanga ina pointi nne, ndani ya mechi hizo, kutokana na sare moja, kufungwa moja na kushinda moja na kabla ya hapo, aliipa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame.
  Haikuwa rahisi; Wakati mwingine ilibidi vikao kama hivi katikati ya mchezo

  Inafahamika hakufukuzwa kwa sababu ya uwezo, bali tofauti zake na uongozi- ndizo zilimpandiaha ndege kuondoka nchini. 
  Huwezi kumuengua Sainfiet katika pongezi za ubingwa huu, kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa msingi wa ujenzi wa kikosi imara na kutengeneza pia mpangilio wa timu, ambao Brandts aliendelea nao.
  Brandts alikuwa kocha wa APR ya Rwanda katika Kombe la Kagame Julai mwaka jana ikifungwa mara mbili na kikosi cha Saintifet- kwa maana hiyo aliiona Yanga na kuijua vyema kabla hajaanza kuifundisha.
  Brandts ametoa sare nne zaidi na kufungwa mechi moja nyingine, akishinda 16 kati ya 21 za Ligi Kuu, ambazo aliiongoza Yanga SC msimu huu hadi sasa. Imetosha Yanga kubwa bingwa.

  MECHI 24 ZILIZOIPA UBINGWA YANGA SC:
  P W D L GF GA GD Pts
  1 Yanga SC 24 17 5 2 44 13 31 56

  15/09/12 Yanga 0-0 Prisons (Mbeya) 
  19/09/12 Yanga 0-3 Mtibwa Sugar (Moro)
  22/09/12 Yanga 4-1 JKT Ruvu Stars
  30/09/12 Yanga 3-1 African Lyon
  03/10/12 Yanga 1-1 Simba
  08/10/12 Yanga 0-1 Kagera Sugar (Bukoba)
  11/10/12 Yanga 3-1 Toto Africans (Mwanza)
  20/10/12 Yanga 3-2 Ruvu Shooting
  24/10/12 Yanga 3-0 Polisi Morogoro
  27/10/12 Yanga 1-0 JKT Oljoro (Arusha)
  31/10/12 Yanga 3-0 JKT Mgambo
  04/11/12 Yanga 2-0 Azam
  11/11/12 Yanga 2-0 Coastal Union (Tanga)
  11/01/13 Yanga 3-1 Prisons
  02/02/13 Yanga 1-1 Mtibwa Sugar
  13/02/13 Yanga 4-0 African Lyon
  23/02/13:  Yanga 1-0 Azam
  27/02/13 Yanga 1-0 Kagera Sugar
  09/03/13 Yanga 1-0 Toto Africans
  16/03/13 Yanga  1-0  Ruvu Shooting
  30/03/13 Yanga 0-0 Polisi Morogoro
  10/04/13 Yanga 3-0 JKT Oljoro FC
  17/04/13 Yanga 1-1  JKT Mgambo (Tanga)
  21/04/13 Yanga 3-0 JKT Ruvu Stars
  MECHI ZIJAZO;
  01/05/13 Yanga Vs Coastal Union
  18/05/13 Yanga Vs Simba

  UONGOZI MPYA NA MIKAKATI YA KURUDISHA HESHIMA…
  WAKATI Yussuf Manji na akina Clement Sanga, Abdallah Bin Kleb, Mussa Katabaro na Aaron Nyanda wanaingia madarakani Yanga Julai 15, mwaka jana- klabu ilikuwa imepoteza hadhi yake.
  Imetoka kufungwa 5-0 na wapinzani wa jadi Simba SC sambamba na kuvuliwa ubingwa pamoja na kukosa hata nafasi ya kucheza michuano ya Afrika mwaka huu.
  Mikakati ya kuijenga Yanga mpya imara ilianza Juni, kwa wagombea Manji, Katabaro, Sanga, Bin Kleb kushirikiana na Seif Ahmad ‘Seif Magari’ kufanya usajili wa wachezaji na baadaye kuajiri kocha, Saintfiet.
  Mjadala; Viongozi wa Yanga wakijadiliana baada ya mechi JKT Mgambo

  Baada ya mafanikio ya Kagame, Yanga walikwenda kwa wiki moja Rwanda pamoja na kuitikia mwaliko wa rais wa nchi hiyo, Paul Kagame, lakini pia kucheza mechi za kirafiki.
  Timu iliporejea, ikaingia kwenye Ligi Kuu na kwa bahati mbaya baada ya mechi tatu Saintfiet akatofautiana na Manji na kufukuzwa. Timu ilikaa na kocha Msaidizi, Freddy Felix Minziro kwa mechi mbili tu kabla ya Brandts kuja nchini.
  Yanga ilifanikiwa kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa kileleni na Desemba ikaenda Uturuki kwa ziara ya mafunzo ya wiki mbili.
  Kwa kiasi fulani, Yanga imenufaika na ziara hiyo, kwani tangu irejee kutoka Ulaya haijapoteza mechi na imekuwa ikicheza soka ya kuvutia.
  Ilikuwa shughuli; Frank Domayo akichuana na wachezaji wa Mgambo

  WACHEZAJI WANASTAHILI PONGEZI…
  Mara nyingi kumekuwa na malalamiko ya timu kubwa kuhonga wapizani na marefa ili kupanga matokeo- lakini wadau wamekuwa wakijiuliza kwa nini zinafanya hivyo na wakati zinasajili wachezaji wa gharama na makocha Wazungu wanaolipwa fedha nyingi?
  Tatizo kubwa, wachezaji wa Simba na Yanga huwa wanacheza ‘kifaza’ hawataki kugusana- hivyo huwa wanajikuta katika wakati mgumu sana wanapokutana na timu ndogo zinazocheza ‘jino kwa jino’.
  Sasa kwa kuwa viongozi wanataka ushindi, wamekuwa wakipenyeza hongo kulainisha mechi- ila Yanga msimu huu wameamua kupambana nayo hiyo. Timu ilipofanya vibaya, viongozi walikuwa wanagombana na wachezaji na makocha, hawakwenda kuhonga refa wala timu pinzani.
  Mara kadhaa imetokea tafrani wakati wa mapumziko na hata baada ya mechi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo Yanga- kutokana na ama timu kucheza vibaya au matokeo mabaya. 
  Nyota mpya; Simon Msuva amekuwa chachu ya ushindi wa mechi kadhaa Yanga

  Ikafika wakati, wachezaji wa Yanga wakawa wanacheza kama wao ndiyo ‘timu ndogo’- watoto wa mjini wanasema walikuwa wanakaba hadi vivuli.
  Yanga ilitanguliwa kwa bao Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ikicheza na Mgambo JKT, lakini baada ya hapo wanaume hao walivyolitafuta bao la kusawazisha nyasi ziliwaka moto hadi likapatikana.
  Ilikuwa inaonekana kabisa wachezaji wa Yanga SC wanacheza kwa ajili ya kutaka kitu fulani, na kulikuwa kuna umoja baina ya wanaocheza na wasiocheza. Kila wanapoingia uwanjani, wachezaji wa benchi wanawaambia wenzao wanaoanza; “Jamani mapema jamani,”, wakiwahamasisha wafunge mapema.
  Alipoteza makali; Didier Kavumbangu alianza vizuri, baadaye akapoteza makali

  Hata Ulaya, vigogo kama Real Madrid, Barcelona, Man United, Bayern Munich, Juventus kuna kipindi vinapitia wakati mgumu katika ligi za kwao- vivyo hivyo kwa Yanga pia kuna wakati mgumu walipitia msimu huu.
  Wachezaji walizomewa na mashabiki kwa sababu hawafungi na ikazidi kuwachanganya zaidi wengine kiasi kwamba wanahitaji muda zaidi kurudi katika hali ya kawaida.  Hawakuchukuliwa kama Robin Van Persie alivyochukuliwa Man United baada ya kucheza mechi 10 bila kufunga bao, au namna ambavyo John Bocco ‘Adebayor’ anachukuliwa hivi sasa Azam FC licha ya kukumbwa na ukame wa mabao.
  Wamepitia mitihani mingi wachezaji wa Yanga SC hadi kutwaa taji na kwa namna yoyote wanastahili pongeza. 
  Hamisi Kiiza alikuwa moto

  BAADA YA UBINGWA?
  Yanga sasa itacheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Kwa kawaida, kila msimu unapomalizika fasheni kubwa kwa timu zetu ni usajili, tena wakati mwingine usajili usio na tija.
  Yanga SC wanapaswa kuliachia benchi la ufundi kazi ya timu. Kocha Brandts, ambaye anastahili kuendelea na kazi Jangwani ispokuwa aongezewe japo msaidizi mmoja kwa ajili ya wachezaji wa mbele, yeye na benchi lake la ufundi wanajua zaidi kuhusu timu na si Bin Kleb wala Manji. 
  Wajengewe kujiamini ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.
  Si tena kesho tusikie mara Shomary Kapombe, Mwinyi Kazimoto na Bin Kleb amuwahi kumsainisha mchezaji ambaye Simba wanamtaka hata kama hahitajiki Yanga, hiyo hapana. Si nzuri.
  Yanga SC waonyeshe ukomavu kwa kuendesha mambo yao kisayansi na kwa utaratibu. 
  Kifaa; Haruna Niyonzima alikuwa shujaa mara kadhaa hadi mashabiki wakawa wanamtunza fedha

  Kwa kiasi kikubwa wachezaji wa Yanga wamekwishazoeana na unaweza kuona hata wale wapya akina Ally Mustafa ‘Barthez’, Kevin Yondan, Simon Msuva, Frank Domayo, David Luhende, Didier Kavumbangu na Nizar Khalfan wanajisikia wapo nyumbabni tayari.
  Kikosi hiki kikiandaliwa vizuri, kinaweza kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika na si kukurupuka kwenda kusajili tu, bila kuzingatia ushauri wa kitaalamu. Hongera Yanga SC. Haikuwa kazi rahisi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: HAIKUWA KAZI RAHISI YANGA KUTWA UBINGWA MSIMU HUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top