• HABARI MPYA

    Thursday, April 18, 2013

    STEWART HALL WA AZAM APAMBANISHWA NA KOCHA WA FAR RABAT KABLA YA MECHI KESHO

    Stewart Hall

    Na Prince Akbar
    MAKOCHA wa timu za Azam, Stewart John Hall na AS FAR Rabat ya Morocco, Abderazzak Khairi watakutana na waandishi wa habari kesho (Aprili 19 mwaka huu) kuzungumzia mechi yao itakayofanyika Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mkutano huo ambao pia utawahusisha manahodha wa timu hizo mbili utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zilizoko Uwanja wa Karume, Barabara ya Uhuru na Shaurimoyo.
    Timu hizo zitakutana katika mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho itakayoanza saa 10:00 jioni, kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye Morocco.
    AS FAR Rabat waliwasili jana Dar es Salaam  na kufanya vya hapa na pale.
    Kwanza walikuwa ni watu wenye wasiwasi tangu wanatua Uwanja wa Ndege na wasiowaamini wenyeji wao, wakitaka zaidi kujiongoza wenyewe na baadaye sasa wakakataa hoteli waliyokodiwa na wenyeji wao, Sapphire Court.
    Pamoja na kuambiwa hoteli hiyo imepitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na timu zote zilizocheza na Azam katika mashindano hayo, zilifikia hapo, Al Nasir ya Sudan Kusini na Barack Young Controllers II ya Liberia, lakini wakagoma.
    Wenyeji wakawaambia kama hawataki hoteli hiyo watajilipia popote watakapokwenda na Waarabu hao nao wakaonyesha jeuri ya fedha kwa kujipangia New Africa Hotel. Kaazi kweli kweli.
    Lakini hizi ni dalili mbaya kwa Waarabu hao kugomea hoteli na visa vyote walivyofanya, kuna hatari Azam wakafanyiwa visa zaidi watakapokwena Morocco kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
    Mshindi wa jumla katika mechi mbili za timu hizo, ataingia kwenye droo ya kucheza na timu zilizotolewa katika Ligi ya Mabingwa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. 
    Azam FC ilifanikiwa kuingia Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, baada ya kuifunga jumla ya mabao 2-1 Barack Young Contollers II ya Liberia.
    Ilianza kwa kushinda 2-1 mjini Monrovia kabla ya kulazimishwa sare ya bila kufungana Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: STEWART HALL WA AZAM APAMBANISHWA NA KOCHA WA FAR RABAT KABLA YA MECHI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top