• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 30, 2013

  UONGOZI AZAM FC WAFIKIRIA KUIPELEKA TIMU HISPANIA, LAKINI...

  Msafara wa Azam FC ukitoka nje ya Uwanja wa Ndege wa Casablanca jana, tayari kwa safari ya Rabat 

  Na Mahmoud Zubeiry, Rabat
  UONGOZI wa Azam FC unafikiria kwenda Hispania kuwatembeza wachezaji wake ambako ni jirani na Morocco, ilipo sasa timu hiyo, lakini kwa kuwa hawakujiandaa kwa hilo, unahofia kukwamishwa na mambo kadhaa.
  Katibu wa Azam, Nassor Idrisa ameiambia BIN ZUBEIRY mjini hapa kwamba, wangeweza kuwapeleka wachezaji Hispania kutalii, lakini kwa kuwa hawajajiandaa kwa hilo, wanahofia baadhi ya mambo yatawakwamisha.
  “Mimi nina uzoefu wa haya mambo, tulikwenda na wachezaji wa timu B Sweden mwaka 2010, watano walitutoroka. Sasa unapotaka kufanya ziara kama hizi, lazima muwe mmejiandaa vya kutosha, ili yakitokea ya kutokea mnakua mnajua mnaanzia wapi,”alisema Nassor.
  Azam FC imetua jana Morocco ikitokea Dar es Salaam kupitia Dubai na itakuwa hapa kwa wiki nzima kabla ya mchezo wa marudiano dhidi ya wenyeji FAR Rabat katika mchezo wa Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi wiki hii.
  Ukuta; Mabeki wa kati wa Azam FC, Joackins Atudo na David Mwantika kulia


  Kulia Abubakar maarufu Clouds, kushoto Kipre Balou na katikati ni mrembo aliyemlaki kwa mashamsham mchezaji huyo baada ya kuwasili Casabalnca

  Hoi bin taaban; John Bocco ukipenda muite Adebayor kushoto na Himid Mao, wakiwa wameketi Uwanja wa ndege wa Casablanca kusubiri usafiri wa kuelekea Rabat jana

  Azam imetua hapa baada ya safari ndefu ya takriban saa 14 angani na saa mbili na ushei barabarani- saa tano kutoka Dar es Salaam hadi Dubai na saa tisa kutoka Dubai hadi Cassablanca- kisha saa mbili kwa barabara hadi Rabat.  
  Kutoka Morocco hadi Hispania ni umbali wa maili tisa tu na kuna boti ziendazo kasi zinazotumia dakika 30 kuvuka hadi nchi hiyo. Kuna miji miwili Hispania, Melilla na Ceuta upande wa pwani ya Mediterranean imepakana na Morocco.
  Rabat, walikofikia Azam ni mji wa tatu kwa ukubwa Morocco ambao unakadiriwa kuwa na watu wasiopungua Milioni 1 na umepakana na Bahari ya Atlantic katika mdomo wa Mto Bou Regreg.
  Kikosi cha Azam kilichofikia katika hoteli ya Golden Tulip, kinatarajiwa kuanza mazoezi leo mjini hapa kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi.
  Ikumbukwe, Azam inahitaji sare yoyote ya mabao au kushinda kabisa ili kufuzu kwenye michuano hiyo, baada ya awali kutoa sare ya bila kufungana mjini Dar es Salaam.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: UONGOZI AZAM FC WAFIKIRIA KUIPELEKA TIMU HISPANIA, LAKINI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top