• HABARI MPYA

    Saturday, April 20, 2013

    SAMATTA NA ULIMWENGU MZIGONI BONDENI LEO AZAM IKIWAKARIBISHA WAMOROCCO TAIFA


    Na Prince Akbar
    WAKATI Azam FC itakuwa ikimenyana na AS FAR Rabat ya Morocco katika mchezo wa kwanza Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika, wachezaji wawili wa Tanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanatarajiwa kuiongoza TP Mazembe ya DRC katika mchezo wa kwanza wa hatua hiyo, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Orlando Pirates nchini Afrika Kusini.
    Wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobaki kwenye michuano ya Afrika, watashuka dimbani, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni kupepetana na Waarabu hao.
    Kikosi cha Azam FC

    Azam FC ina fursa nzuri ya kufanya vizuri kwenye mechi hiyo itakayochezeshwa na refa Emile Fred kutoka Shelisheli kutokana na maandalizi iliyofanya na itakuwa vyema Watanzania wakijitokeza kwa wingi uwanjani kuiunga mkono timu hiyo.
    Makocha wasaidizi wa timu zote mbili, Kalimangonga Ongala wa Azam na Lahcen Ouadani wa AS FAR Rabat walizungumza na Waandishi wa habari jana kuhusu mechi hiyo, na kusema wamejiandaa kuibuka na ushindi.
    Kocha Ongala alisema wamepata DVD za mechi tatu za mwisho za AS FAR Rabat, moja ikiwa dhidi ya timu ya Al Nasir ya Libya ambayo waliitoa katika Raundi ya Pili na nyingine mbili za ligi ya Morocco ambazo wamezifanyia kazi kuhakikisha wanashinda leo.
    Naye Ouadani alisema hawaifahamu vizuri Azam, lakini wanaujua mpira wa Tanzania baada ya kuangalia mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) iliyochezwa jijini Dar es Salaam Machi 24 mwaka huu na Stars kushinda mabao 3-1.
    Baadhi ya wachezaji ambao Azam inatarajia kuwatumia kwenye mechi ya leo ni pamoja na Aishi Manula, Mwadini Ally, Khamis Mcha, John Bocco na Salum Abubakar ambao pia wamo kwenye kikosi cha sasa cha Taifa Stars kilicho chini ya kocha Kim Poulsen.
    Samatta na Ulimwengu kushoto

    Lakini pia, Azam inajivunia wachezaji wake mahiri wa kigeni, Kipre Balou na pacha wake, Kipre Tchetche kutoka Ivory Coast, Wakenya Joackins Atudo na Humphrey Mieno na Mganda, Brian Umony. 
    AS FAR Rabat ina wachezaji sita kwenye timu ya Taifa ya Morocco. Wachezaji hao ni mabeki Younes Bellakhdar, Abderrahim Achchakir, Younnes Hammal, na viungo Salaheddine Said, Salaheddine Aqqal na Youssef Kaddioui.
    Mabingwa wa Afrika mwaka 1995, Pirates wao watakuwa na kazi nzito mjini Johannesburg mbele ya akina Samatta na Ulimwengu ambao timu yao, Mazembe imewahi kutwaa mara nne ubingwa wa Afrika
    Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kuzikutanisha timu hizo tangu mwaka 2002 na Pirates ikatolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya Mazembe kushinda 3-1 ugenini na kufuzu hatua ya makundi, ambako walikwenda hadi Nusu Fainali walipotolewa na Zamalek ya Misri.
    Tangu wakati huo, makali ya Mazembe yameongezeka na kuweza kutwaa mataji mawili ndani ya miaka minne na kuweka historia ya kutwaa Medali ya Fedha katika Klabu Bingwa ya Dunia mwaka 2010.
    Pirates ndiyo kwanza inajaribu kurudi tangu walipofika Nusu Fainali mwaka 2006.
    Beki mkongwe wa Pirates na Nahodha, Lucky Lekgwathi amesema rekodi nzuri ya Mazembe siku za karibuni inaufanya mchezo huo uwe mgumu.
    Mazembe ina majeruhi mmoja, mshambuliaji Mzambia Given Singuluma na kwa maana hiyo, kocha Lamine Ndiaye atawategemea Samatta mwenye mabao mawili hadi sasa katika mashindano haya na Ulimwengu.
    Mchezaji wa Mazembe anayetakiwa na Pirates, Rainford Kalaba ataongoza safu ya kiungo baada ya kufanya mambo adimu katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Mochudi Centre Chiefs ya Botswana wiki mbili zilizopita.
    Wachezaji wa Pirates waliokuwa majeruhi baada ya mechi za mwishoni mwa wiki iliyopita, Andile Jali, Oupa Manyisa, Siyabonga Sangweni, Thabo Matlaba pamoja na Sifiso Myeni wote wanatarajiwa kuwa tayari kwa mchezo huo.
    Mshindi wa jumla atafuzu kutinga hatua ya makundi ambayo itaanza Julai 19 na atakayefungwa, ataangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, mechi za kwanza zikichezwa kati ya Mei 17 na 19. Mungu ibariki Azam, wabariki Samatta na Ulimwengu. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SAMATTA NA ULIMWENGU MZIGONI BONDENI LEO AZAM IKIWAKARIBISHA WAMOROCCO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top