• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 19, 2013

  YANGA WASITARAJIE MTEREMKO KWETU, ASEMA PIUS KISAMBALE WA COASTAL UNION

  Pius Kisambale kulia

  Na Prince Akbar
  MSHAMBULIAJI wa Coastal Union, Pius Kisambale ameitahadharisha timu yake ya zamani, Yanga SC isitarajie mteremko katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya timu hizo Mei 1, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kisambale ameiambia BIN ZUBEIRY jana mjini Tanga kwamba, Yanga wamepanga kutangaza ubingwa ndani ya mechi zao mbili zijazo (JKT Ruvu na Coastal), lakini wanajidanganya.
  “Mimi nasema wanajidanganya, kusema kwamba wataifunga JKT na baadaye sisi (Coastal) ili watangaze ubingwa. Labda wawafunge JKT, lakini sio sisi. Tutawakazia vibaya sana,”alisema Pius. 
  Pius alisema binafsi yeye amepania kucheza soka ya kiwango cha juu ili kuwaonyesha Yanga SC walikosea kumuacha na pia kulinda heshima ya timu yake, Coastal.
  “Kwanza sisi wachezaji wengi wa Coastal tunaupenda sana ule Uwanja (Taifa), tena kwa mfumo wetu wa uchezaji, panatufaa sana na Yanga watashangaa siku hiyo,”alisema.
  Coastal iko salama, ikiwa haina wasiwasi wa kushuka Daraja kwa pointi zake 33 ilizovuna katika mechi 23, lakini haina nafasi ya kuwamo ndani ya mbili bora. 
  Yanga, inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 53, baada ya kucheza mechi 23 ikiwa inahitaji pointi sita katika mechi zake tatu zilizobaki dhidi ya JKT Ruvu Jumapili, Coastal Union Mei 1 na Simba SC Mei 18, ili kujihakikishia ubingwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA WASITARAJIE MTEREMKO KWETU, ASEMA PIUS KISAMBALE WA COASTAL UNION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top