• HABARI MPYA

    Friday, April 26, 2013

    YANGA BINGWA 2012/2013 BAADA YA AZAM KUTOA SARE 1-1 NA COASTAL MKWAKWANI LEO

    Yanga SC; Mabingwa 2012/2013

    Na Prince Akbar, Tanga
    YANGA bingwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2012/2013. Habari ndiyo hiyo. Yanga ya Dar es Salaam imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu jioni hii, kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa ligi hiyo baina ya wenyeji Coastal Union na Azam FC ya Dar es Salaam, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.
    Matokeo hayo yanamaanisha, Azam FC waliokuwa washindani wakuu wa Yanga SC yenye pointi 56, hawawezi tena kufikisha pointi hizo ambazo wanazo mabingwa hao wapya, kwani hata wakishinda mechi zao nyingine  mbili zilizobaki, watamaliza na pointi 54. 
    Mchezaji aliyepeleka shangwe na vigelegele Jangwani leo ni Danny Lyanga, ambaye aliifungia Coastal bao la kusawazisha dakika ya 72. 
    Lyanga ambaye ilibaki kidogo asajiliwe Yanga msimu huu kutoka Toto Africans, kama si kuzidiwa kete na Coastal, alifunga bao hilo katika mpira wake wa kwanza kuugusa tangu aingie kuchukua nafasi ya Suleiman Kassim ‘Selembe’ dakika ya 71.
    Alifunga bao hilo, baada ya kupokea pasi nzuri ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Pius Kisambale, ambaye ni mdogo wa kiungo wa Wana Jangwani hao, Athumani Iddi ‘Chuji’.
    Azam ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika mchezo wa leo, lililofungwa na beki Aggrey Morris kwa penalti dakika ya 60, baada ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Gaudence Mwaikimba kuchezewa rafu kwenye eneo la hatari  na beki Yussuf Chuma- na refa Andrew Shamba wa Pwani akaamuru pigo hilo.
    Baada ya bao hilo, Coastal walionekana kufanya jitihada za wazi kusawazisha na ndipo Lyanga aliyetokea benchi akawapa ubingwa Yanga.
    Matokeo haya yanakuwa sawa na Coastal kulipa fadhila kwa Yanga, kwani hata wao, ubingwa wao pekee wa Ligi Kuu waliochukua mwaka 1988 ulitokana na ‘msaada’ wa wana Jangwani huo.
    Msimu huo, mshindani wa Coastal katika mbio za ubingwa alikuwa Simba SC ambaye ili kutwaa taji hilo, alihitaji kushinda mechi ya mwisho dhidi ya African Sports mjini Tanga huku akiomba Wagosi wa Kaya walale mbele ya Yanga Uwanja wa Taifa.
    Lakini Yanga wakacheza ‘kichovu’ na Athumani China akaenda kupiga penalti ‘kiviivu’ akakosa, Coastal ikishinda 2-0 na kusherehekea taji pekee la ubingwa wa Ligi Kuu, licha ya Simba pia kushinda 3-0 dhidi ya Sports Tanga. 
    Hili linakuwa taji la 24 kwa Yanga, tangu watwae kwa mara ya kwanza mwaka 1968.
    Coastal Wamelipa fadhila za 1988

      MSIMAMO WA VPL HADI SASA...
                                        P W D L GF GA GD Pts
    1 Yanga SC        24 17 5 2 44 13 31 56
    2 Azam FC          24 14 5 5 42 20 22 48
    3 Kagera Sugar   23 11 7 5 25 18 7 40
    4 Simba SC         22 9 9 4 32 21 11 36
    5 Mtibwa Sugar   24 9 9 6 27 23 4 36
    6 Coastal Union   24 8 10 6 24 21 3 34
    7 Ruvu Shooting  22 8 6 8 21 21 0 30
    8 JKT Oljoro 24 7 7 10 22 27 -5 28
    9 Prisons            24 6 8 10 14 21 -7 26
    10 JKT Ruvu 24 7 5 12 20 37 -17 26
    11 Mgambo JKT   23 7 4 12 16 23 -7 25
    12 Toto African     25 4 10 11 22 34 -12 22
    13 Polisi Moro      23 3 10 10 12 22 -10 19
    14 African Lyon 24 5 4 15 16 36 -20 19

    Aidha, huu unakuwa msimu wa pili mfululizo, Azam wanaukosakosa ubingwa wa Ligi Kuu, baada ya msimu uliopita pia kuzidiwa kete na Simba SC. 
    Kikosi cha Coastal Union leo kilikuwa; Shaaban Kado, Hamad Khamis, Othman Tamim, Philip Mugenzi, Yussuf Chuma, Abdi Banda, Joseph Mahundi, Razack Khalfan, Pius Kisambale/Mohamed Soud dk85, Suleiman Kassim ‘Selembe’/Danny Lyanga dk71 na Twaha Shekuwe. 
    Azam FC; Mwadini Ally, Himid Mao, Erasto Nyoni, David Mwantika, Aggrey Morris, Jabir Aziz/Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’ dk75, Brian Umony/Seif Abdallah Karihe dk68, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba/Abdi Kassim ‘Babbi’ dk82, Humphrey Mieno na John Bocco ‘Adebayor’.

    ORODHA MABINGWA WA JUMLA LIGI KUU:
    1965 : Sunderland (Dar es Salaam) 
    1966 : Sunderland (Dar es Salaam) 
    1967 : Cosmopolitans (Dar es Salaam) 
    1968 : Yanga 
    1969 : Yanga 
    1970 : Yanga 
    1971 : Yanga 
    1972 : Yanga 
    1973 : Simba 
    1974 : Yanga 
    1975 : Mseto SC (Morogoro) 
    1976 : Simba 
    1977 : Simba 
    1978 : Simba 
    1979 : Simba 
    1980 : Simba 
    1981 : Yanga 
    1982 : Pan African 
    1983 : Yanga 
    1984 : Simba 
    1985 : Yanga 
    1986 : Tukuyu Stars (Mbeya) 
    1987 : Yanga 
    1988 : Coastal Union (Dar es Salaam) 
    1989 : Yanga 
    1990 : Simba  
    1991 : Yanga 
    1992 : Yanga 
    1993 : Yanga 
    1994 : Simba 
    1995 : Simba 
    1996 : Yanga 
    1997 : Yanga 
    1998 : Yanga 
    1999 : Mtibwa Sugar (Morogoro) 
    2000 : Mtibwa Sugar (Morogoro)  
    2001 : Simba 
    2002 : Yanga 
    2003 : Simba 
    2004 : Simba 
    2005 : Yanga 
    2006 : Yanga 
    2007 : Simba (Ligi Ndogo) 
    2008 : Yanga 
    2009:  Yanga  
    2010: Simba SC
    2011: Yanga SC
    2012: Simba SC
    2013: Yanga SC
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA BINGWA 2012/2013 BAADA YA AZAM KUTOA SARE 1-1 NA COASTAL MKWAKWANI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top