• HABARI MPYA

    Friday, April 19, 2013

    SIMBA SC YAUSAJILI TFF MKATABA WAKE MPYA NA MRISHO NGASSA, ILA...

    Mkataba mpya watinga TFF; Ngassa
    ana msimu mmoja zaidi Msimbazi

    Na Mahmoud Zubeiry
    SIMBA SC imeupeleka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mkataba wake mpya na mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa, ambao unaonyesha ataitumikia klabu hiyo na msimu ujao pia.
    Chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba SC, kimesema; “Tumeupeleka mkataba ambao Ngassa alisaini na sisi na TFF wamegonga muhuri wa kuupokea,”.
    Kikifafanua, chanzo hicho kimesema; “Sisi tuliununua mkataba wa Ngassa uliokuwa umebaki Azam FC kwa shilingi Milioni 25, kwa hivyo, haki za mchezaji huyo zote zikahamia kwetu,”.
    “Lakini alipokuja kwetu, tukazungumza naye, akasaini mkataba wa msimu mmoja zaidi kutoka ule mkataba wake uliobaki Azam FC na tulimpa shilingi Milioni 30. Fedha taslimu Milioni 12 na gari aina ya verosa yenye thamani ya Sh. Milioni 18, akasaini kila sehemu na kuweka dole gumba,”kilisema chanzo hicho.   
    Hata hivyo, chanzo hicho kimesema kwa sasa Mrisho amekuwa akilalamika kwa uongozi wa Simba kwamba alidhani alipewa Milioni 12 na Verosa ili akubali kuja Simba.
    Ikumbukwe awali Ngassa aligoma kupelekwa kwa mkopo Simba SC, hadi alipofanya mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo na kufikia makubaliano ndipo akajiunga na klabu hiyo.
    Lakini chanzo hicho kimesema kwa sasa Mrisho anataka kufanya tena mazungumzo na Simba SC kwa ajili ya kusaini rasmi mkataba mwingine. “Sisi bado tunajiuliza, huyu mtu alikwishasaini na sasa anasema alidhani alipewa fedha na gari ili akubali kuja Simba SC. Inawezekana kwa sababu wachezaji wetu wana  matatizo, wakishaona fedha wao wanasaini tu bila hata kuisoma mikataba,”.
    “Bado tunatafakari, tunaweza kurudi naye mezani, ili aitumikie klabu kwa moyo bila kinyongo, au tu tukaamua autumikie mkataba ambao tayari tumekwishausajili na TFF,”kilisema chanzo.
    Siku zote, Mrisho mwenyewe amekuwa akisistiza hakusaini mkataba mwingine Simba SC akitokea Azam, bali anajua alikuja kumalizia mkataba wake wa klabu yake ya zamani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC YAUSAJILI TFF MKATABA WAKE MPYA NA MRISHO NGASSA, ILA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top