• HABARI MPYA

    Tuesday, April 30, 2013

    MBERWA KUCHEZESHA YANGA NA COASTAL KESHO TAIFA

    Yanga SC

    Na Boniface Wambura
    REFA Simon Mberwa kutoka Pwani, atachezesha mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Yanga Sc na Coastal Union ya Tanga.
    Katika mechi hiyo namba 172, Mberwa atasaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara refa wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam na Kamisaa David Lugenge kutoka Iringa.
    Viingilio katik mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo.
    Katika michezo mingine ya ligi hiyo, mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu, Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa African Lyon katika mechi namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. 
    Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
    Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons na Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili Oljoro JKT kutoka Arusha.
    Tayari Yanga SC wamejihakikishia ubingwa wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 56, ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MBERWA KUCHEZESHA YANGA NA COASTAL KESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top