• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 20, 2013

  AZAM YAWAKOSAKOSA WAARABU TAIFA, TATU ZAGONGA MWAMBA HUWEZI AMINI

  Kipa wa AS FAR Rabat, Ali Grouni akiwa amedaka mpira mbele ya mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Herman Tchetche katika mchezo wa kwanza, Raundi ya Tatu Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.

  Na Mahmoud Zubeiry
  AZAM FC imelazimishwa sare ya bila kufungana jioni hii na AS FAR Rabat ya Morocco katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Tatu, Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Matokeo hayo yanaifanya Azam iwe na mtihani mgumu katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo Morocco, wakitakiwa lazima kushinda au kutoa sare ya mabao ili kufuzu.
  Pamoja na sare hiyo, Azam watakumbuka sana mabao matatu ya wazi waliyokosa kupitia kwa washambuliaji wao wa pembeni, Kipre Herman Tchetche mawili na Khamis Mcha ‘Vialli’ moja,  
  Kipre aligongesha mwamba mashuti mawili katika dakika za 51 pembeni kushoto katikati  na dakika ya 90+1 mwamba wa juu katikati baada ya jitihada za kuwatoka mabeki wa AS FAR Rabat.
  Khamis Mcha naye alimtoka vizuri beki wa pembeni wa AS FAR Rabat dakika ya 52 lakini akapiga nje shuti lake.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emile Fred wa Shelisheli, aliyesaidiwa na nduguze Steve Maire na Jean Ernesta pembeni, kipindi cha kwanza Azam walionekana kucheza kwa tahadhari zaidi na kufanya mashambulizi machache.
  Lakini kipindi cha pili, walifunguka na kuanza kushambulia moja kwa moja jambo ambalo liliweka kwenye misukosuko lango la AS FAR Rabat kwa muda mrefu hadi wachezaji wa timu hiyo kuanza kufanya hila za kupoteza muda ili kupunguza kasi ya wenyeji.
  John Raphael Bocco ‘Adebayor’ naye alilitia misukosuko mara kadhaa lango la wageni kila ilipoingizwa mipira ya juu kutokea pembeni hususan kona japokuwa alikuwa chini ya ulinzi mkali leo.
  Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo/Luckson Kakolaki dk7, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Salum Abubakar, John Bocco ‘Adebayor’, Humphrey Mieno na Kahmis Mcha ‘Vialli’/Mwaikimba dk78.
  AS FAR Rabat; Ali Grouni, Mustafa Mrani, Younes Hammal, Younes Belakhdar, Yassine El Kordy, Abdelrahim Achchakir/Mostafa El yousfi dk74, Salaheddine Said, Mohamed El Bakkali, Salaheddine Aqqal/Souffiane Alloudi dk80, Mustafa Allaoui na Hicham El Fathi/Youssef Anouar dk69.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: AZAM YAWAKOSAKOSA WAARABU TAIFA, TATU ZAGONGA MWAMBA HUWEZI AMINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top