• HABARI MPYA

    Thursday, April 18, 2013

    KIIZA NA NIYONZIMA HALI MBAYA TANGA

    Niyonzima akijiandaa kuingia jana

    Na Mahmoud Zubeiry, Tanga
    KIUNGO Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima na mshambuliaji Hamisi Friday Kiiza hawakufanya mazoezi leo, baada ya kuumia kwenye mchezo wa jana Uwanja wa Mkwakwani, Tanga dhidi ya JKT Mgambo timu hizo zikitoka sare ya 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Yanga imefanya mazoezi leo asubuhi Mkwakwani na inatarajiwa kuondoka mchana kurejea Dar es Salaam kujiandaa na mchezo ujao.
    Mganda Kiiza aliumia dakika ya 44 baada ya kupigwa kiatu ndani ya 18 na beki wa Mgambo JKT na kumpisha Said Bahanuzi uwanjani, wakati Mnyarwanda Niyonzima aliingia kipindi cha pili na kugongwa puani na beki wa Mgambo.
    Niyonzima alikuwa tayari ana uvimbe kwenye pua uliomsababishia homa na akashindwa kuanza katika mechi hiyo- na kwa kugongwa huko alitonesha maumivu hata leo hakuweza kufanya mazoezi.
    Kiiza anaweza kukosa mechi ijayo na JKT Ruvu Dar es Salaam kwa sababu ameumia kifundo cha mguu, lakini Niyonzima anaweza kurudi uwanjani muda si mrefu.  
    Sare ya Yanga jana inamaanisha mbio za ubingwa bado zinaendelea kati ya Yanga SC yenye pointi 53 kileleni sasa na Azam FC yenye pointi 47.
    Kiiza akichechemea kutoka
     nje baada ya kuumia jana

    Hadi mapumziko, Mgambo walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Issa Kanduru aliyemgeuza kwenye eneo la hatari beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kabla ya kumtungua Ally Mustafa ‘Barthez’, baada ya kupokea pasi nzuri ya Salum Mlima.
    Mgambo walitawala sehemu kubwa ya mchezo wa kipindi cha kwanza na kupeleka mashambulizi mengi zaidi langoni mwa Yanga, ambayo zaidi walikuwa wakipiga mirefu kwa lengo la kushambulia moja kwa moja.
    Mchezo pia ulikuwa wa ‘kibabe’ na dakika 45 za kwanza zilimalizika kiungo Frank Domayo akiwa ana ngeu jicho la kushoto baada ya kupigwa kisukusuku na mchezaji mmoja wa Mgambo.
    Dakika 44 zilitosha kwa Hamizi Kiiza katika mchezo wa leo, baada ya kugongwa na beki mmoja wa Mgambo na kushindwa kuendelea na mchezo, akimpisha Said Bahanuzi.
    Kipindi cha pili, Yanga SC ilianza na mabadiliko, ikiwatoa Domayo aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Nurdin Bakari na baadaye Oscar Joshua akampisha Haruna Niyonzima.
    Mabadililo hayo yaliongeza uhai katika Yanga SC na kuanza kulishambulia lango la Mgambo JKT mfululizo hatimaye dakika ya 86 wakapata bao la kusawazisha, ambalo japo ilionekana amefunga Simon Msuva, lakini Nurdin Bakari alisema amefunga yeye.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIIZA NA NIYONZIMA HALI MBAYA TANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top