• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 28, 2013

  DEGE LA ARSENAL LAWABEBA AZAM FC KUFUATA TIKETI YA KUSONGA MBELE KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA


  Na Mahmoud Zubeiry
  AZAM FC inaondoka leo jioni Dar es Salaam kwa ndege ya shirika la Emirates, wadhamini wa Arsenal ya England kwenda Rabat, Morocco kumenyana na wenyeji, FAR Rabat katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Tatu Kombe la Shirikisho Afrika.
  Msafara wa leo utahusisha wachezaji na benchi la Ufundi, baada ya juzi viongozi na wapenzi kadhaa kutangulia nchini humo, ili kuweka mazingira sawa.   
  Azam inakwenda huko, ikiwa inakabiliwa na jukumu la kutoa sare ya mabao au kushinda ili kusonga mbele, baada ya awali katika mchezo wa kwanza kulazimishwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita.
  Japokuwa hilo linachukuliwa kama jambo gumu mbele ya wengi, lakini rekodi ya timu hiyo, mali ya bilionea Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake inaonyesha linawezekana.
  Azam imekuwa ikicheza vizuri na kupata matokeo mazuri katika mechi za ugenini kwenye michuano hii, kuliko nyumbani na hata kufuzu kwake hadi hatua hii zaidi kulitokana na matokeo ya mechi za ugenini.
  Raundi ya kwanza, Azam ilianza kwa kushinda kwa taabu 3-1 Dar es Salaam dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini, sehemu kubwa ya mchezo huo matokeo yakiwa 1-1 kabla ya mabao ya dakika za jioni ya Kipre Tchetche kutengeneza ushindi huo.
  Mchezo wa marudiano, Azam ilishinda 5-0 ugenini na kufanya ushindi wa jumla wa 8-1, ikisonga mbele kibabe.
  Raundi ya Pili, ilianza kwa ushindi wa 2-1 ugenini, Liberia dhidi ya wenyeji, Barack Young Controllers II, lakini katika mchezo wa marudiano ilibanwa kwa sare ya 0-0.
  Kocha Muingereza Stewart Hall hakuipa umuhimu mechi ya Ligi Kuu juzi dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga iliyoisha kwa sare ya 1-1 akiwapumzisha wachezaji wake kadhaa wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya mechi na FAR Rabat.
  Wakati mabeki Waziri Salum, Joackins Atudo, viungo Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Balou na mshambuliaji Kipre Tchetche hawakukanyaga kabisa nyasi za Uwanja wa Mkwakwani juzi, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alicheza kwa dakika 15 tu za mwisho- ili kuhakikisha wanakuwa vizuri Jumapili mjini Rabat.
  Kutoka kikosi cha kwanza cha sasa cha Azam waliocheza dakika zote juzi ni kipa Mwadini Ally, kiungo aliyehamishiwa beki ya kulia, Himid Mao, beki David Mwantika, kiungo Humphrey Mieno na washambuliaji Brian Umony na John Bocco ‘Adebayor’.
  Azam, itakuwa Rabat kwa wiki nzima hadi Jumapili itakapocheza mechi na imejipanga vema kuhakikisha inavuka hatua hii. Safari njema wawakilishi wetu. Kila la heri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: DEGE LA ARSENAL LAWABEBA AZAM FC KUFUATA TIKETI YA KUSONGA MBELE KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top