• HABARI MPYA

  Jumatano, Aprili 24, 2013

  BAYERN MUNICH INATAKA NINI KWA KOCHA ZAIDI YA MATOKEO MAZURI?


  “Bayern Munich 4-0 Barcelona”. Hivyo ndivyo ubao wa matokeo ulikuwa unasomeka baada ya dakika 90 na ushei za Nusu Fainali ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Allianz Arena, Munich, Ujerumani.
  Kama itashindikana kukutana naye, basi hata kuzungumza naye japo kwenye simu baada ya matokeo haya, basi mtu ambaye Josef ‘Jupp’ Heynckes angemtaka sana anaweza kuwa yule mwandishi aliyemuuliza kama amewasiliana na Pep Guadriola kabla ya kucheza na Barca ili ampe mbinu? 
  Aliuliza hivyo mara baada ya kupangwa kwa droo ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa, Bayern ikipangwa na Barcelona na Heynckes alimjibu; “Niheshimu mimi na kazi yangu. Sijawahi kumfuata yeyote au kuomba ushauri. Sihitaji msaada wa yeyote kumsoma mpinzani,". 

  Hili lilikuwa swali zuri kwa upande wangu, kwa sababu lisingetokea, wengi tungedhani kuna mchango wa Pep katika matokeo ya jana- lakini sasa tunaweza kuamini hakuna alichochangia.
  Mwanzoni mwa mwezi huu niliandika, Pep Guardiola anakwenda kufanya nini Bayern Munich, chini ya  Jupp Heynckes tayari timu imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani kwa pointi 20 zaidi na ipo Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa.
  Leo nikirudia kuuliza Pep wa nini Bayern, timu ipo mguu mmoja Fainali chini ya Josef ‘Jupp’ Heynckes, mmoja kati ya makocha ninaowakubali sana kwa kazi yao nzuri.
  Una shaka yoyote kuhusu kiwango cha uchezaji cha Bayern Munich na aina ya uchezaji wake? Inacheza soka safi ya kuvutia na japo haina wachezaji wa kuingia tatu bora ya Ballon d’Or, lakini ina wachezaji wazuri ambao hawaterereki kwa misimu kadhaa sasa.
  Mabadiliko katika benchi la ufundi ya nini Bayern? Hilo ni swali ambalo mtu yeyote anaweza kujiuliza. Anakwenda Pep kwa sababu ya jina na umaarufu wake, au kwa sababu klabu inahitaji kocha mwingine?
  Kocha wa sasa amefanya kazi nzuri Bayern. Hakuna sababu ya mabadiliko katika benchi la ufundi, lakini tayari inafahamika tangu Januari mwaka huu kwamba mwishoni mwa msimu Jupp Heynckes atapunga mkono kuaga mashabiki, akimuachia ofisi Pep.
  Narudia tena, inawezekana watu hawamjui vizuri Jupp Heynckes ambaye Mei 9, mwaka huu atafikisha miaka 68. Huyu ni mshambuliaji wa zamani wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi. 
  Enzi zake anacheza, alitamba sana katika klabu ya Borussia Monchengladbach miaka ya 1960 na 1970, ambako alishinda mataji kibao na vikombe, likiwemo Kombe la UEFA. 
  Alikuwepo kwenye kikosi cha Ujerumani Magharibi kilichotwaa ubingwa wa Ulaya na Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza na akiwa kocha, ameshinda mataji matatu ya ubingwa wa Ujerumani akiwa na hiyo hiyo Bayern Munich wakati msimu wa 1997–98 aliiwezesha Real Madrid kutwaa taji la kwanza la Ligi ya Mabingwa baada ya zaidi ya miaka 30.
  Huyu ni kocha mzoefu, akiwa ameifundisha Bayern kwa vipindi vitatu tofauti, 1987 na 1991, 2009 na 2011 hadi leo. Amefundisha pia Borussia Monchengladbach, Athletic Bilbao, Eintracht Frankfurt, Tenerife, Real Madrid, Benfica, Schalke 04 na Bayer Leverkusen.
  Pep aliondolewa Barcelona msimu uliopita, baada ya timu kupoteza taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa na kuanza kuwa laini kwa wapinzani wao, Real Madrid. Kwa matokeo hayo, nani atastaajabu, timu ina wachezaji bora wa dunia kama Iniesta, Xavi, Pedro, Messi na wengine, inakosa taji?    
  Jose Mourinho aliwahi kusema; “Unaweza kuwa na nyota wa kiwango cha juu wa kuteka hisia, unaweza kuwa na uwanja mzuri, unaweza kuwa na vifaa vizuri, unaweza kuwa na miradi mizuri kama ya masoko na kila aina ya kitu. Lakini kama haushindi... ni kazi bure,”.
  Camp Nou ni Uwanja mzuri, akina Messi ni wachezaji wazuri na timu ina vifaa vizuri vya mazoezi na miradi pia mizuri, hadi sisi huku Afrika tunanunua bidhaa zenye nembo ya Barca- lakini nani atamuheshimu Messi na wenzake kama Barca inapigwa 4-0 na Bayern?
  Sasa ajabu, kocha anayeshinda mataji Bayern anaondolewa. Ni kocha ambaye ameitengeneza timu ya sasa, inaishi kwa falsafa na mifumo yake ambayo ndiyo siri ya mafanikio yake kwa sasa.
  Ni rafiki wa wachezaji wote na wanafanya kazi kwa ushirikiano na upendo wa hali ya juu. Yote hayo hayazingatiwi, anaondolewa. Ataondoka tu, hata abebe taji la Ligi ya Mabingwa pia, tayari Pep amesaini mkataba na klabu kuanza kazi msimu ujao, Jupp Heynckes ataondoka tu.
  Ni uamuzi uliofikiwa chini ya uongozi wa timu, wa mpira haswa. Bayern ni klabu ya watu wa mpia haswa. Rais wake, Ulrich ‘Uli’ Hoeneb (61) ni mtu wa mpira haswa.
  Huyo ni mshambuliaji wa zamani wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, ambaye amecheza Fainali moja ya Kombe la Dunia na mbili za Mataifa ya Ulaya, akishinda taji moja moja kati ya yote.
  Uongozi wa Bayern umesheheni watu wa mpira pia akina Herbert Hainer, Makamu wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Adidas AG, Rupert Stadler, Makamu wa Pili wa Rais na Mwenyekiti wa Audi na Wajumbe Helmut Markwort, Dieter Rampl, Karl Hopfner, Dk. Edmund Stoiber ambaye ni Waziri na Rais wa zamani wa Bavaria, Timotheus Hottges, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Telekom AG na Profesa. Dk. Martin Winterkorn, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Volkswagen AG.
  Bodi ya Ukurugenzi pia inaundwa na watu wa mpira, chini ya Mwenyekiti Karl-Heinz Rummenigge, Makamu wake Jan-Christian Dreesen, Mkurugenzi wa Michezo, Matthias Sammer na Andreas Jung Deputy Mjumbe.
  Kwa hivyo, haya ni maamuzi yaliyochukuliwa na watu wenye kujua nini wanachokifanya na nini wanachokihitaji. Ni maamuzi ya kuheshimu, lakini bado narudia kujiuliza, Pep anakwenda kufanya nini Bayern inayoikung’uta Barca 4-0 chini ya Josef ‘Jupp’ Heynckes? Kwani wanataka nini zaidi ya matokeo mazuri kama haya?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: BAYERN MUNICH INATAKA NINI KWA KOCHA ZAIDI YA MATOKEO MAZURI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top