• HABARI MPYA

    Thursday, April 18, 2013

    LIGI KUU BARA MSIMU HUU WE ACHA TU, JKT RUVU INAPUMUA KWA MSAADA WA MASHINE!

    Shomary Kapombe wa Simba SC akichuana na David Mwantika wa Azam kushoto katika mechi iliyoisha kwa sare ya 2-2

    Na Mahmoud Zubeiry
    SARE ya 1-1 kati ya Yanga SC na Mgambo JKT jana imeongeza urefu wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na sasa inawezekana bingwa akapatikana katika siku ya mwisho kabisa, Mei 18 au ikiwa mapema mechi za pili kuelekea mwishoni mwa ligi.
    Baada ya Simba SC kuibana kwa sare ya 2-2 Azam FC, ilitarajiwa Yanga ingetangaza ubingwa ndani ya dakika 180, lakini kwa kuambulia pointi moja jana, sasa wanahitaji dakika 180 zaidi kujihakikishia taji hilo.
    Lakini inaweza ikawa mapema zaidi ya hapo, iwapo Azam itapoteza mechi zake zijazo na Yanga itashinda.
    Yanga SC ina pointi 53 na imebakiza mechi tatu, wakati Azam yenye mechi tatu pia, ina pointi 47. Azam inaweza kufikisha pointi 56 tu ikishinda mechi zake zote zilizobaki, maana yake ikifungwa mechi moja inaweza kufikisha 53, ambazo tayari Yanga inazo.
    Haruna Niyonzima wa Yanga kushoto akichuana na beki wa Mgambo katika mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1
    MSIMAMO WA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA:
                                   P W D L GF GA GD   Pts
    1 Yanga SC 23 16 5 2 41 13 28 53
    2 Azam FC 23 14 5 4 41 19 22 47
    3 Kagera Sugar 23 11 7 5 25 18 7 40
    4 Simba SC 22 9 9 4 32 21 11 36
    5 Mtibwa Sugar 24 9 9 6 27 23 4 36
    6 Coastal Union 23 8 9 6 23 20 3 33
    7 Ruvu Shooting 22 8 6 8 21 21 0 30
    8 JKT Oljoro 24 7 7 10 22 27 -5 28
    9 Prisons 24 6 8 10 14 21 -7 26
    10 Mgambo JKT 23 7 4 12 16 23 -7 25
    11 JKT Ruvu 22 6 5 11 19 34 -15 23
    12 Toto African 25 4 10 11 22 34 -12 22
    13 Polisi Moro 23 3 10 10 12 22 -10 19
    14 African Lyon 23 5 4 14 16 35 -19 19

    MECHI ZILIZOBAKI…
    Aprili 21, 2013
    JKT Ruvu Vs Yanga SC
    Aprili 24, 2013
    African Lyon Vs JKT Ruvu
    Aprili 25, 2013
    Ruvu Shooting Vs Simba SC
    African Lyon Vs JKT Ruvu
    Aprili 27, 2013
    Coastal Union Vs Azam FC
    Aprili 28, 2013
    Simba SC Vs Polisi Moro
    Mei 1, 2013
    Mtibwa Sugar Vs African Lyon
    Yanga SC Vs Coastal Union
    JKT Ruvu Vs TZ Prisons
    Polisi Moro Vs Kagera Sugar
    Ruvu Shooting Vs JKT Oljoro
    Mei 8, 2013
    Simba SC Vs Mgambo JKT
    Mei 11, 2013
    Azam FC Vs Mgambo JKT
    Kagera Sugar Vs Ruvu Shooting
    Mei 18, 2013
    Toto Africans Vs Ruvu Shooting
    Mgambo JKT Vs African Lyon
    JKT Ruvu Vs Mtibwa Sugar
    TZ Prisons Vs Kagera Sugar
    Simba SC Vs Yanga SC
    JKT Oljoro Vs Azam FC
    Polisi Moro Vs Coastal Union

    Maana yake, kama Azam itapoteza mechi ijayo na Yanga ikishinda, Watoto wa Jangwani watahitaji pointi moja katika mchezo wake ufuatao ili kujihakikishia ubingwa, hivyo mfalme mpya wa Ligi Kuu kupatikana mechi ya pili kuelekea mwishoni mwa ligi hiyo.
    Lakini kulingana na kasi ya Ligi Kuu sasa na ikizingatiwa wawania ubingwa hao wote watacheza mechi zao zilizobaki Dar es Salaam, kuna uwezekano bingwa akapatikana mwishoni kabisa mwa Ligi Kuu.

    NAFASI YA PILI:
    Wakati Azam FC inawania ubingwa, lakini pia inaweza kujikuta ikikosa hata nafasi ya pili, kutokana na kasi ya Kagera Sugar nyuma yao.
    Kagera wana pointi 40 sasa baada ya kucheza mechi 23 pia na wanaweza kufikisha pointi 49. Hivyo Azam ili kujihakikishia tiketi ya kucheza michuano ya Afrika mwakani, inahitaji kushinda mechi moja zaidi ili kufikisha pointi 50.
    Simba SC wenye pointi 36 baada ya kucheza mechi 22 wanaweza kutimiza pointi 48 hadi mwisho wakishinda mechi zao zote.
    Vichwa chini; Wachezaji wa JKT Ruvu

    Maana yake, kama Azam itashinda mechi moja tu ijayo, Simba SC rasmi watakuwa hawamo katika michuano ya Afrika mwakani. Watacheza michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita, basi.

    MKIANI: 
    Kuanzia timu iliyo katika nafasi ya nane hadi mkiani kabisa, 14 yoyote kati yao inaweza kuingia kwenye orodha ya timu tatu za kushuka Daraja, kuzipisha Mbeya City, Ashanti United na Rhino zilizopanda. 
    Hali ni mbaya zaidi kwa timu za jeshi, kwani JKT Oljoro, JKT Mgambo, JKT Ruvu na Polisi Morogoro zote zinachungulia kaburi. Hadi sasa ni timu moja tu ambayo unaweza kusema tayari imeipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu, ni Toto African ya Mwanza yenye pointi 22 na imebakiza mechi moja.
    Safari ya kurudi Nyamagana; Kikosi cha Toto Africans ambacho kimeaga Ligi Kuu

    JKT Oljoro iliyo katika nafasi ya nane ina pointi 28, ambazo Polisi na African Lyon zilizo mkiani kabisa zinaweza kuzifikisha zikishinda mechi zao zote tatu tatu zilizobaki. Maana yake hawako salama sawa tu na Prisons yenye pointi 26 katika nafasi ya tisa, Mgambo JKT pointi 25 nafasi ya 10 na JKT Ruvu pointi 23 nafasi ya 11.
    Kwa kiasi fulani tunashuhudia ligi yenye ushindani msimu huu, farasi wawili Yanga SC na Azam FC wakifukuzana kileleni na huko mkiani ni patashika ambayo huwezi kuamini kwamba timu kama JKT Ruvu inapumua kwa taabu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: LIGI KUU BARA MSIMU HUU WE ACHA TU, JKT RUVU INAPUMUA KWA MSAADA WA MASHINE! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top