• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 21, 2013

  MAZEMBE YAPIGWA 3-1, SAMATTA AKOSA BAO HILO HUWEZI KUAMINI

  Mfungaji wa bao la kwanza la Pirates, Onyekachi Okonkwo

  Na Prince Akbar
  MSHAMBULIAJI Collins Mbesuma jana alifunga mabao mawili akiiwezesha Orlando Pirates kushinda 3-1 nyumbani dhidi ya TP Mazembe ya DRC mjini Johannesburg katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Kwa matokeo hayo, Mazembe italazimika kushinda 2-0 ili kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini, wakati Pirates watakwenda kupigania sare kwenye mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo ili kusonga mbele.
  Pirates ilipata bao lake la kwanza dakika ya pili tu ya mchezo kupitia kwa Onyekachi Okonkwo, baada ya kiungo huyo wa Nigeria kufumua shuti la umbali wa mita 30.
  Dakika saba baadaye, mshambuliaji wa Mazembe, Mtanzania Mbwana Samatta alikosa bao la wazi baada ya kupiga kichwa kilichopaa juu ya lango.
  Pirates ilikaribia kufunga tena kama si shuti la Mbesuma kuokolewa na kipa wa Mazembe, Muteba Kidiaba.
  Lakini Pirates walijikuta katika wakati mgumu baada ya Mazembe kupata bao la kusawazisha dakika moja kabla ya mapumziko kupitia kwa mshambuliaji Patou Kabangu.
  Kipindi cha pili, Mazembe walirudi na moto tena na dakika ya 50, Rainford Kalaba alipiga shuti kali juu ya lango.
  Pirates ilizinduka baada ya kushambuliwa mara mbili tatu na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 57 kupitia kwa Mbesuma, aliyemalizia kazi nzuri ya Khethowakhe Masuku.
  Mbesuma akafunga tena katika daikika za majeruhi na kufanya ushindi wa 3-1, hivyo kuisogeza Pirates karibu na hatua ya makundi ya michuano hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MAZEMBE YAPIGWA 3-1, SAMATTA AKOSA BAO HILO HUWEZI KUAMINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top