• HABARI MPYA

    Thursday, April 25, 2013

    LADY JAYDEE YUPO JUU HATA KITUO CHA REDIO KIKISUSA KUCHEZA NYIMBO ZAKE, WATANZANIA WANAMKUBALI

    Yuko Juu; Lady Jaydee anafanya vizuri, hata vituo vingine vikisusa kucheza nyimbo zake

    Na Mahmoud Zubeiry
    WATANZANIA wa leo, wengi wao ni waelewa na ndiyo maana wanakosoa mtu au au taasisi bila kujali ukubwa wake, iwapo watabaini mapungufu.
    Vyombo vya Habari vinatambulika kama njia ya kufikisha ujumbe kwa jamii, kwa maana ya kuhabarisha, lakini kuelimisha na siku hizi, kuburudisha pia.
    Inapotokea chombo cha habari kikayumba katika haya, japo kwa maslahi yake binafasi, basi Watanzania wengi wataelewa na huo utakuwa mwanzo wa chombo husika kupoteza heshima yake.
    Na Watanzania wanapenda vile vitu ambavyo vinafanya vizuri au kwa namna moja au nyingine, vinateka hisia za watu. Watanzania wanampenda Lady Jaydee, ni mwanamuziki mzuri na siku zote yupo juu.
    Kazi zake ni nzuri. Wimbo wake mpya, Joto Hasira ni mzuri, tena nadiriki kusema sana na unawakuna wengi, kwa ala zake, mpangilio wa sauti, mtiririko wa mashairi na ujumbe wenyewe. 
    ‘Ameua’ zaidi pale alipomshirikisha MC wa ukweli, Profesa Jay, kijana aliyefanya mapinduzi makubwa katika muziki wa kizazi kipya, kutoka kuonekana wa kihuni, hadi wa heshima kiasi fulani.
    Jamani, joto linatia hasira, kwani uongo? Na foleni je? Saluti kwake Jide. Ajabu leo kituo cha Radio kinagoma kucheza wimbo huo mzuri, yaani kinajifanya kama kipo Msumbiji hakijui kinachoendelea katika tasniya ya muziki Tanzania. Hii ni aibu yao wenyewe.
    Hicho kituo hicho, lazima kijue kinajishushia heshima kwa jamii ya Watanzania na kupoteza imani kwa wasikilizaji wake.
    Kimekwishagombana na wasanii kibao jamani, tena kwa sababu zile zile. Kama wale wa zamani walikuwa ‘wanafiki’ na huyu Jide je, ambaye amekitumikia na ametumiwa na wamiliki wake kama mtambo wa kuwatengenezea fedha, nchi inajua. 
    Kwani ile Smooth Vibes ilikuwa ni ya nani? Sina uhakika labda ya Reginald Mengi au Anthony Diallo.  Lakini huko ndiko alikotokea Jide katika albamu ya Asubuhi ya 2001, iliyoshirikisha na wengine kama akina D. Rob (marehemu), Terrence, Fina Mango na wengineo.
    Watu wanajua sana, kama msanii gani, gazeti gani, blog gani na ya aina gani inafanya vizuri- wewe ukiwadanganya wanakujua ni muongo. Na wataacha kukuheshimu. Utakaa studio unapiga kelele unadhani watu wanakusikiliza kumbe, muda mrefu tu wamekwishahamia stesheni nyingine baada ya kukuona wewe na Redio yako ni waongo.
    Unawaambia Watanzania eti Azam FC ni timu ya kwanza ya Tanzania kushinda mechi Magharibi mwa Afrika baada ya kuifunga Barack Young Controllers 2-1 Liberia, na Simba ilipoifunga Hearts Of Oak ya Ghana 2-0 mabao ya Adam Sabu (marehemu) na Abdallah Kibadeni, ilikuwa ya Kenya?
    Msingi mkubwa wa chombo cha habari ni kutenda haki kwa kuripoti ukweli na kuzingatia usahihi, unapopoteza sifa kama hizi elewa unaelekea kizani na huna heshima tena.
    Kuibeba chuki kama sera kuu ya mapambano ni kujimaliza mwenyewe- na mbaya zaidi pale unapoonea wanyonge. Wasanii wa Tanzania ni wanyonge tu na wanahitaji sana msadaa wa vyombo vya habari, lakini inapotokea chombo cha habari ndiyo kinakuwa mstari wa mbele kuwanyanyasa, inauma sana.
    Mtu anajipendekeza kwa Mheshimiwa Rais, anajifanya mtetezi wa haki za wasanii, kumbe ndiye mnyonyaji na mnyanyasaji mkubwa. Huu sasa ndio unafiki. 
    Yako wapi yale matamasha ya uzinduzi wa albamu za wasanii wa Bongo Fleva kwa awamu, tena kwa ziara nchi nzima chini ya udhamini mnono wa makampuni makubwa nchini na bado kila sehemu ‘nyomi ya kufa mtu’?
    Hizi sasa ndizo dalili za laana ya kuwanyanyasa wasanii na wanyonge. Na bado. Lady Jaydee mwanamuziki mzuri tu hata kituo kimoja kisipocheza nyimbo zake.  Yuko juu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: LADY JAYDEE YUPO JUU HATA KITUO CHA REDIO KIKISUSA KUCHEZA NYIMBO ZAKE, WATANZANIA WANAMKUBALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top