• HABARI MPYA

    Tuesday, April 23, 2013

    BEKI TEGEMEO AZAM APEWA MAPUMZIKO MAALUM, AGGREY MORRIS KUANZA TENA KAZI IJUMAA MKWAKWANI

    Mapumzikoni; Joackins Atudo hatagusa mpira hadi Morocco

    Na Mahmoud Zubeiry
    BEKI tegemeo wa Azam FC, Joackins Atudo Otieno ataendelea kuwa nje ya Uwanja hadi timu hiyo itakapofika Morocco wiki ijayo tayari kwa mchezo wa marudiano, Raundi ya Tatu Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji FAR Rabat. 
    Mkenya huyo aliumia bega katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Pwani Machi 30, mwaka huu, lakini akaendelea na kazi.
    Kwa bahati mbaya, Jumamosi katika mchezo wa kwanza na Rabat, Uwanja wa Taifa, Atudo alitonesha bega hilo na kushindwa kuendelea na mechi dakika ya saba tu akimpisha Luckson Kakolaki.
    Kwa sababu hiyo, kocha Muingereza Stewart Hall ameamua Atudo akae nje na asiguse kabisa mpira hadi timu itakapofika Morocco, ili kulipa mapumziko bega hilo lipone sawa sawa.
    Kwa kupumzishwa Atudo, Stewart atamtumia beki Aggrey Morris Ambroce katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union Ijumaa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Aggrey ni kati ya wachezaji wanne wa Azam FC waliokuwa wamesimamishwa kupisha uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kupokea rushwa wahujumu timu hiyo ilipocheza na Simba katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu mwishoni mwa mwaka jana.
    Hata hivyo, baada ya TAKUKURU kukamilisha uchunguzi wake na kubaini nyota hao hawakuhusika, Aggrey na wenzake, Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni na Said Mourad wamerusishwa kazini.
    Azam, inayokimbizana na Yanga SC kuwania ubingwa wa Ligi Kuu itaondoka Dar es Salaam kesho tayari kwa mchezo huo wa Ijumaa ambao lazima washinde ili kuweka hai matumaini ya ubingwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BEKI TEGEMEO AZAM APEWA MAPUMZIKO MAALUM, AGGREY MORRIS KUANZA TENA KAZI IJUMAA MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top