• HABARI MPYA

  Saturday, July 06, 2019

  MTIBWA, KAGERA SUGAR TIMU NYINGINE KONGWE LIGI KUU, ILA...

  Na Dominick Salamba, DAR ES SALAAM
  KUNA siku nilikuwa napita mahali fulani nikamuona mtoto mmoja anacheza niliamua kumsogelea kuona zaidi kilicho nifanya nisogee ni vile alivyokuaanacheza,alikuwa anajenga nyumba ya miti kwa kuipanga afu akimaliza anaanza kuruka kwa kufurahi na kujikuta anaikanyaga kwa bahati mbaya ile nyumba na kuifanya ianguke na kumfanya aanze kulia huku akianza kuijenga tena.
  Nilijifunza kitu kuwa alitamani sana nyumba yake idumu pale ila pengine hakujua kama yeye ndiye sababu za kuifanya nyumba ile walau idumu lakini pia isingeweza kudumu kwa muda maana hata upepo ungeiangusha tu hivyo angelijua angeanza kuzuia mazingira yake ili aweze kuilinda furaha yake.
  Niliamua kuondoka taratibu huku nikitafakari na kupata kitu kumbe kuna wakati unaweza kujitengenezea  furaha ya mda mchache halafu baada ya muda ukajichukia na kujiona hauna maana uku ukiwa hujajua kuwa sababu ya kutoweka furaha yako ni wewe mwenyewe.
  Sawa tuachane na mtoto maana watoto wanamengi nirudi kwa mada yangu hii kwa siku ya leo.
  Kwanza nianze kueleza kwanini Mtibwa Sukari na Kagera Sukari kwakua ni miongoni mwa timu kongwe kwenye ligi kuu soka Tanzania bara ukitoa wale jamaa wawili wa Kariakoo,lakini pia wamedumu muda mrefu wakiwa kwenye ligi itakuchukua muda ukianza kutafuta kujua kama toka wamepanda ligi daraja la kwanza ikiitwa kabla ya mwaka 1996 hadi ligi kuu pale ilipotimu mwaka 1998,ila siyo hivyo tu ni miongoni mwa timu ambazo zimekuwa na mwendelezo mzuri kwenye ligi na kutoa ushindani wa haja sana na pia wachezaji ambao wametoka kwenye vilabu hivyo waligeuka kuwa lulu kwenye hizi timu kubwa za hapa Tanzania kuna mifano kadhaa watu kama Mrisho Ngasa,Shabani Kado,Said Bahanuzi,Monja Liseki,Zuberi Katwila,Mexime,Shabani Nditi na wengine kibao ambao walitikisa soka na Tanzania kwa umahiri wao ndani ya kiwanja.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli akiwasabahi wachezaji wa Kagera Sugar Mei 19,mwaka 2018 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya wenyeji, Simba SC

  Pia ni miongoni mwa timu ambazo zinajimudu ni kwa maana vya uwezo wa kuwahudumia wachezaji kwa kuwapatia mahitaji ya msingi na kumudu gharama za uendeshwaji wa timu hizo ni vigumu kusikia migomo ya wachezaji wa timu hizi kisa posho,msharaha au pesa ya usajili na si hivyo tu hata viwanja vyao kwa maana ya sehemu ya kuchezea ni bora sana kwa mazingira yetu ya Tanzania.
  Lakini kubwa zaidi ni uwezo wao wa kuvumbua vipaja na kuvitambulisha katika soka la Tanzania.
  Pamoja na sifa lukuki nilizowapa bado kuna jambo natamani kuwaeleza kwani kwa mbali nikiwakumbuka namkumbuka yule mtoto niliye mtolea mfano hapo awali kwani ninajua kabisa wanajitahidi sana kuzalisha vipaji ndani ya Tanzania ila walitakiwa waende mbali wasiwe nusunusu kama wameamua kufanya biashara ya soka kwa maana ya kuuza wachezaji ni bora wawekeze kweli kweli juzi tu hapa timu ya mtibwa sukari chini ya miaka 17 imetwaa ubingwa tena kwa kandanda safi sana ila hawa vijana kwanini wasiwatafutie soko nje ya nchi?kwanini wasiingie ubia na timu mbalimbali duniani ili wao wawe ni kiwanda cha kuzalisha vijana kama wanavyozalisha sukari?uzuri wa hizi timu hazina presha hivyo zinaweza kuwa na malengo ya muda mrefu na yakafikika bila shaka.
  Kwa nguvu ya uchumi waliyonayo kwanini hawajaamua kuwekeza kwenye miundombinu ya kuchezea,kujenga hostel na mambo mengine kwa kuendeleza soka la vijana sidhani kama hawajui faida yake na kwa kufanya hivyo watakua wamesaidia maisha ya vijana wengi ambao mpira ndio kitu pekee kinachoweza kuwafanya wafikie ndoto zao.
  Sawa tunajua wanaongoza kuuza wachezaji waliowazalisha hapa nchini lakini kuwauza Simba na Yanga bado si mafanikio makubwa ni kujichekesha wenyewe maana mwisho wao unakuwa kurudi tena Mtibwa au Kagera sukari kitu ambacho siyo afya badala yake wangewekeza kweli wakatoa vijana walioiva leo tungekuwa tunashuhudia vijana wakija timu ya Taifa wakiwa  chimbuko la timu hizi mbili.
  Sawa pengine inaweza kua sio kipaumbele chao ila kuna wakati mahitaji ya jamii yanakufanya ubadili mtazamo na kulifata soka sidhani kwamba wanafanya haya wakiwa hawatarajii mrejesho chanya wa kiuchumi hapana..Najua kabisa malengo ya kua mabingwa wa nchi ni magumu kulingana na uwepo wa timu hizi mbili za Kariakoo ambazo ubingwa wanaweza kuupata kwa namna yeyote ile,lakini bado nafasi ya kuwa miongoni mwa timu kubwa na zenye mafanikio inawezekana leo kuna timu ambazo zinaheshima kubwa Duniani si kwa kuchukua ubingwa wa Ulaya hapa bali kutokana na kutoa vipaji vikubwa vya soka duniani timu kama Ajax,Dortmund,Sevila,Basel,na nyingine nyingi ambozo zimefanikiwa kupitia biashara ya soka.
  Uwezo mlionao na viongozi mliona pia kama mtaamua kuwekeza kwenye soka la vijana lenye mwendelezo hapana shaka Tanzania itajivunia kupitia vilabu vyenu tunaweza kuwa na akina Samatta wengi wapya walio kulia kwenye vituo vyenu jambo ambalo ni heshima iliyotukuka sana sana kwa maendeleo ya soka letu.
  Siyo lazima muanze kwa mkupuo mana kama kuanza tayari mmeanza ila kikubwa ni kutanua wingo katika uwekezaji wenu na kujikita zaidi kuona mnavuka mipaka ya Tanzania huku silaha kubwa ikiwa ni utulivu mlio nao kwani hakuna presha kutoka mahali popote hakuna kugombea madaraka,hakuna migogoro sijui timu ziendeshwaje hakuna makundi mara ya asili na ya kisasa mmetulia sana na nina imani hata Serikali itaunga mkono juhudi zenu kwa maendeleo ya soka letu.
  Ni heshima yangu kwenu kuwaona mkitutoa hapa tulipo na kusaidia vijana wetu wengi ambao wapo gizani hawaoni mwanga kupitia soka.
  Dah nadhani imetosha ngoja nikapashe maana naona kitambi kinakuja bila kupiga hodi kama vipi wakati mwingine.

  (Mwandishi wa makala haya, unaweza kumfollow kupitia @dominicksalamba au kuwasiliana naye kwa namba  +255713942770)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MTIBWA, KAGERA SUGAR TIMU NYINGINE KONGWE LIGI KUU, ILA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top