• HABARI MPYA

    Thursday, August 09, 2018

    RAIS MAGUFULI AMLILIA KING MAJUTO, ASEMA ALIKUWA KIELELEZO CHA SAFARI NDEFU YA SANAA KATIKA NCHI YETU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha msanii nguli wa filamu, maigizo na uchekeshaji Tanzania, Amri Athumani maarufu kama King Majuto.
    Katika salamu zake kufuatia msiba huo wa usiku wa jana, Rais Magufuli amesema King Majuto atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi za chama na Serikali katika kuhimiza maendeleo.
    “King Majuto alikuwa kielelezo cha safari ndefu ya sanaa kwa nchi yetu, kwa muda wote amedhihirisha kipaji, ujuzi na uwezo wa hali ya juu katika uigizaji na uchekeshaji na hivyo kuwa kipenzi cha Watanzania na wasanii wenzake, hatutasahau ucheshi wake, upendo na uzalendo kwa nchi yake wakati wote wa uhai wake," amesema Rais Magufuli.
    Rais Dk John Magufuli (kulia) alikwenda kumjulia hali King Majuto Januari 31 mwaka huu Muhimbili
    Mzee Majuto alikuwemo kwenye tamasha la SZIFF Aprili 1, mwaka huu

    Kiongozi huyo wa nchi alimjulia hali msanii King Majuto alipokuwa amelazwa katika hospitali ya Tumaini jijini Dar es Salaam Januari 31, mwaka huu kabla hajasafirishwa India Mei mwaka huu kwa matibabu zaidi.
    King Majuto amefariki dunia Saa 1:30 usiku wa jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili mjini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa matibabu kufuatia hali yake kubadilika na kuwa mbaya wiki iliyopita.
    King Majuto alianza kusumbuliwa na maradhi mwaka jana na Mei 4 mwaka huu akapelekwa India kwa matibabu kabla ya kurejea Juni 22 mwaka huu na kutangaza rasmi kustaagu shughuli zote za sanaa kwa sababu za Kiafya.
    Alirejea anasukumwa kwenye kiti maalum kuashiria kwamba pamoja na matibabu yake nje ya nchi, bado afya haikuwa njema sana. 
    Na wiki iliyopita alikimbizwa tena katika hospitali ya Muhimbili baada ya hali kubadilika ghafla na kuwa mbaya tena, ambako alilazwa ICU kabla ya usiku wa jana kuaga dunia.
    King Majuto Alizaliwa mwaka 1948 jijini Tanga na kusoma shule ya Msambwini mkoani humo na hadi anafariki amecheza zaidi ya filamu 1,000.
    Hizo ni pamoja na; Lolita, Sio Sawa, Mama Ntilie, Nahama,Gumzo, Mrithi Wangu, Rent House, Ndoa ya Utata, Daladala, Nimekuchoka, Mbegu, Zebra, Shikamoo Mzee, Tabia, Utani, Tikisa, Trouble Maker, Gundu, Kizungunguzu, Shoe Shine, Street Girl, Faithful, Mtego wa Panya, Boss, Back with Tears, Sikukuu ya Wajinga, Nyumba Nne, Chips Kuku, Kitu Bomba, Ndoto ya Tamaa, Lakuchumpa, ATM, Bishoo, Tupo Wangapi, Moto Bati, Varangati, Out Side, Pusi na Paku, Juu kwa Juu, Swagger, Oh Mama, Jazba, Mke wa Mtu Sumu, Mbugila, Kidumu, Mkali Mo, Mpela Mpela, Utanibeba, Babatan, Mjomba, Msela wa Manzese, Karaha, Mpango Sio Matumizi, Mume Bwege, Shuga Mammy, Embe Dodo, Nakwenda Kwa Mwanangu, Seaman, Naja Leo Naondoka Leo Tanga, Mgeni Njoo, Kuwadi, Kulipa Tabu, Uso wa Mbuzi, Machimbo, Fundi Feni, Mwizi wa Kuku, Mtu Mzima Hovyo, Wake Up, Vituko Show Vol. 10, Bettery Low, Brothers, Alosto, Back from New York, Kipofu, Koziman Vol 21, After Money, Talaka Yangu, Gereji, Welcome Back, Mshamba, Pedeshee, Waiter, Inye Plus, Inye Gwedegwede na Inye Vol.1.
    Inasemekana King Majuto ndiye muigizaji wa kwanza kuandaa kazi zake katika mikanda na kuuza huku akifanya kazi na shirika la filamu Tanzania (Tanzania Film Company-TFC). 
    Alianza kuigiza mwaka 1958 akiwa na umri wa miaka tisa kuanzia shuleni kabla ya kujiunga na DDC kibisa mwaka 1983 ambacho ndicho kilimpatia umaarufu mkubwa. 
    Baadaye alijiunga na Muungano Culture Troupe chini ya Dk, Norbet Chenga, Tanzania One Theatre (TOT) chini ya Kapteni John Komba (marehemu) kabla ya kuamua kufanya zake binafsi.  King Majuto atabaki kuwa msanii mkubwa kwenye historia ya sanaa za filamu na uchekeshaji Tanzania. Buriani Mzee Majuto. Umeyamaliza yako ya duniani. Nenda kwa mola wako. Na Mola akupumzishe kwa amani. Amin. 

    UTARATIBU WA KUMUAGA MZEE WETU KING MAJUTO. 
    Mwili wa Marehemu Mzee wetu Majuto utaswaliwa na kuagwa katika Msikiti ulipo pale ndani Muhimbili wakti wa Swalat Dhuhr ( Swala ya Mchana). 
    BAADA YA HAPO MWILI UTAAGWA VIWANJA VYA KARIMJEE. 
    HIVYO, Kuanzia saa nane Mchana Wanafamilia wote, ndugu, jamaa na marafiki, Wapenzi na Wadau mbali mbali tunatakiwa tukutane  pale kwa ajili ya Kusoma Dua na Kumuaga Mzee wetu. 
    Baada ya Swalat L'laasir (Swala ya Alasiri ) Mwili wa Marehemu Mzee wetu Majuto utasafirishwa kwenda Mkoani Tanga na Maziko ni Ijumaa baada ya Swalat Dhuhr ( Swala ya Mchana ) Tanga Mjini.
    Pia kutakuwa na Usafiri maalum kwa ajili ya Wasanii. 
    Wote mnaotarajia kusafiri Mnaelekezwa kujiorodhesha kwa Afisa Habari wa TDFAA Kinondoni Bw. Masoud Kaftany. 
    Michango yote itakusanywa na Kamati ya Matukio na Uratibu. 
    By. Chiki Mchoma. 

    Mwenyekiti/Uratibu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS MAGUFULI AMLILIA KING MAJUTO, ASEMA ALIKUWA KIELELEZO CHA SAFARI NDEFU YA SANAA KATIKA NCHI YETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top