• HABARI MPYA

    Sunday, May 15, 2016

    MASHALI AMTWANGA MWARABU NA KUTWAA UBINGWA WA DUNIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BONDIA Francis Mashali amefanikiwa kutwaa ubingwa wa dunia wa UBO uzito wa Super Middle baada ya kumshinda kwa pointi Sajad Mehrabi wa Iran usiku wa Jumamosi Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mashali anayekwenda kwa jina la utani la Simba, alipewa ushindi huo na majaji wote watatu katika pambano hilo kali na la kusisimua liliodumu kwa raundi 12.
    Mehrabi alionekana ni bondia bora zaidi ulingoni, lakini staili ya kupigana kwa kutafuta ushindi wa Knockout (KO) ilimponza kupoteza pambano hilo kwa pointi.
    Mashali alilianza vizuri pambano hilo akipigana kwa tahadhari na kukwepa kabisa mtego wa kupigwa kwa KO na mpinzani mwenye ngumi nzito kutoka bara Asia.
    Bondia Francis Mashali (kulia) akimchapa konde mpinzani wake, Sajad Mehrabi wa Iran usiku wa Jumamosi Uwanja wa Ndani wa Taifa
    Mashabiki wakiwa wamembeba Mashali baada ya pambano hilo
    Refa Anthony Rutta akimuinua mkono Mashali kumtangaza mshindi wa pambano
    Mgeni rasmi akimvalisha mkanda wa ubingwa wa dunia wa UBO Mashali baada ya ushindi wake
    Akiongozwa na bondia nyota wa zamani nchini, Rashid Matumla, Mashali alionekana kupigana kwa utulivu, umakini na kujiamini jambo ambalo liliwafanya mamia waliojitokeza kushuhudia mchezo huo kumshangilia tangu mwanzo.
    Baada ya raundi saba, Mehrabi alionekana kama kuanza kuchoka na kasi yake kupungua na Mashali akafanya vizuri zaidi katika raundi ya saba hadi ya tisa.
    Hata hivyo, katika raundi ya 10, Mehrabi alirudi na kasi mpya na kufanikiwa kumtandika makonde mazito mfululizo Mashali alIyepepesuka hadi kwenye kamba.
    Mashali alirejea mchezoni baada ya refa Anthony Rutta kusimamisha pambano kwa muda kumsikilizia, lakini hakuweza kumalizia vizuri raundi hiyo, 
    Katika raundi ya 11, Mehrabi aliingia na moto tena, lakini safari hiyo Mashali alirudi kwa tahadhari na kufanikiwa kumpunguza kasi mpinzani wake huyo.
    Raundi ya 12 mabondia wote walipigana sawa ingawa kwa ujumla ngumi za Mehrabi zilionekana kuwa nzito kuliko za Mashali.
    Mehrabi hakuwa na malalamiko baada ya pambano zaidi ya kumkumbatia mpinzani wake na kumpongeza kwa ushindi huo.
    Katika mapambano ya utangulizi, bondia mwingine nyota wa Tanzania, Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ alimshinda Ben Sajjabi wa Uganda kwa KO raundi ya pili pambano la uzito wa Super Bantam.
    Mtanzania mwingine, Nassib Ramadhani alimshinda kwa pointi Reemy Iga wa Uganda pia pambano la uzito wa Super Bantam.
    Allan Kamote wa Tanzania alitoka sare na Salim Chazama wa Malawi katika pambano la uzito wa Light raundi sita.
    Ramadhani Shauri wa Tanzania alimshinda kwa pointi Osgood Kayuni wa Malawi pambano la uzito wa Welter raundi sita.
    Saleh Mkalekwa alitwaa taji la UBO uzito wa Welter baada ya kumshinda James Onyango wa Kenya kwa pointi pambano la raundi 10, wakati Twaha Kiduku alimshinda kwa KO raundi ya kwanza Fred Nyakesa wa Kenya pambano la uzito wa Light Heavy raundi sita lisilo la ubingwa.
    Bondia wa kike, Lulu Kayage alitoshana nguvu na Chiedza Hamakoma wa Malawi katika pambano la raundi nne uzito wa Welter na Dickson Mwakisopile alimshinda kwa pointi Mtanzania mwenzake, Ramadhani Ally katika pambano la uzito wa juu raundi nne.
    Shaaban Kaoneka alimshinda Mtanzania mwenzake, Hassan Mwakinyo kwa KO raundi ya tano, wakati Issa Nampepeche hakutokea kupigana na Baina Mazola katika pambano la uzito wa Super Feather raundi sita.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MASHALI AMTWANGA MWARABU NA KUTWAA UBINGWA WA DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top