• HABARI MPYA

  Tuesday, January 06, 2015

  SHERMAN: TANZANIA KUNA VIPAJI VINGI

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  MSHAMBULIAJI Mliberia wa Yanga SC, Kpah Sean Sherman amesema kwamba kwa muda mfupi aliocheza Tanzania, amegundua nchi hii ina vipaji vingi.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana visiwani japa, Sherman amesema kwamba wachezaji wa Tanzania wana uwezo sana na anashangaa kwa nini hawafiki mbali kisoka.
  “Rasmi niliijua Tanzania baada ya mpango wa kuja kucheza Yanga SC, nilikuwa sijui lolote kuhusu nchi hii. Nikaanza kuingia kwenye intaneti kusoma ndiyo nikapta kidogo kujua,”amesema.
  Mchezaji huyo mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kasi na kufunga mabao, amesema baada ya kufika hapa alianza kujionea maajabu ndani ya timu yake kutokana na uwezo mkubwa wa baadhi ya wachezaji.
  Kpah Sherman amesema Tanzania kuna vipaji vingi

  Amesema baada ya kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Simba SC katika Nani Mtani Jembe akagundua zaidi kwamba Tanzania kuna vipaji vingi.
  “Tulipocheza na Azam (katika Ligi Kuu), nikasema basi hii ni nchi ya soka. Zaidi navutiwa na mashabiki wanapenda sana timu zao, wanakuja kwa wingi uwanjani na wanatoa sapoti ya kutosha. Ni nchi nzuri kucheza,”amesema.
  Mliberia huyo ameongeza kwamba baada ya kufika Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, pamoja na Yanga SC kushinda 4-0 mara mbili dhidi ya Taifa ya Jang’ombe na Polisi, lakini walicheza dhidi ya timu zenye wachezaji wenye vipaji.
  Sherman amejiunga na Yanga SC Desemba mwaka jana akitokea klabu ya Ligi Kuu ya Cyprus Kaskazini, Cetinkaya FC, ambayo alikuwa anaichezea kwa mkopo kutoka Aries FC ya kwao Liberia.
  Hadi sasa, Mliberia huyo amecheza mechi nne Yanga SC na kufunga mabao mawili wakati leo anatarajiwa kuiongoza katika mchezo wa mwisho wa Kundi A Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtende.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SHERMAN: TANZANIA KUNA VIPAJI VINGI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top