• HABARI MPYA

  Tuesday, January 06, 2015

  MESSI ATOA YA MOYONI; “SIYO KILA SIKU…”

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  WINGA Ramadhani Singano ‘Messi’ jana amefunga bao lililoivusha Simba SC Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi na akasema si wakati wote mchezaji huwa anacheza vizuri.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Amaan, Zanzibar baada ya mechi na JKU ambayo Simba SC ilishinda 1-0, Messi alisema kwamba viongozi wa klabu wanapaswa kutambua si wakati wote mchezaji atakuwa anacheza vizuri.
  “Hata hao akina Ronaldo (Cristiano) na Messi (Lionel) kuna wakati vile vile hawachezi vizuri. Lakini huku (Tanzania) usipocheza vizuri mechi moja maneno yanakuwa mengi sana,”amesema.
  Ramadhani Singano 'Messi' amesema mchezaji hawezi kucheza vizuri wakati wote

  Winga huyo aliyeibuliwa kutoka timu ya vijana ya Simba SC, maarufu kama Simba B amesema kwamba hakuna mchezaji anayependa kuingia uwanjani kuharibu, bali inatokea tu bahati mbaya kuna siku mchezo unamkataa.
  “Kila mtu anapenda kuingia uwanjani na kufanya vizuri. Lakini kuna siku unaingia uwanjani na unashindwa kuisaidia timu. Haimaanishi wewe ni mchezaji mbaya, ni hali ya kimchezo tu,”amesema.
  Messi jana alicheza vizuri na kufunga bao zuri kutokana na haswa na jitihada, maarifa na ubunifu wake na kuiwezesaha Simba SC kumaliza kileleni mwa Kundi C, kwa pointi sita zilizotokana na ushindi wa mechi mbili.
  Simba SC ilianza vibaya mashindano haya baada ya kufungwa 1-0 na Mtibwa Sugar, lakini ikazinduka katika mchezo wa pili na kushinda 1-0 dhidi ya Mafunzo, bao pekee la Said Hamisi Ndemla kabla ya jana pia kushinda 1-0 dhidi ya JKU.
  Na kwa matokeo hayo, Simba SC itakutana na mshindi wa tatu bora namba mbili katika Robo Fainali kesho Uwanja wa Amaan, Zanzibar.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MESSI ATOA YA MOYONI; “SIYO KILA SIKU…” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top