• HABARI MPYA

  Tuesday, January 06, 2015

  KOPUNOVIC: MECHI MBILI BILA KURUHUSU BAO HII NDIYO SIMBA SC NINAYOITAKA

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  KOCHA mpya wa Simba SC, Goran Kopunovic raia wa Seribia amesema kwamba amefurahi kushinda mechi ya pili mfululizo tangu aanze kazi, lakini kilichomfurahisha zaidi ni kucheza mechi zote hizo bila kuruhusu nyavu zao kuguswa hata mara moja.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Uwanja wa Amaan, Zanzibar baada ya mechi dhidi ya JKU, Kopunovic amesema kwamba kutofungwa bao katika mechi hizo ni jambo lililomfurahisha.
  Mserbia huyo ameiongoza Simba SC kushinda 1-0 mara mbili tangu aanze kazi dhidi ya Mafunzo na JKU na hatimaye kutinga Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi kama kinara wa Kundi C.
  Goran Kopunovic amefurahi Simba SC kucheza mechi mbili bila kufungwa bao

  Kopunovic aliikuta Simba SC imekwishapoteza mchezo wa kwanza wa kundi hilo dhidi ya Mtibwa Sugar kwa kufungwa 1-0 chini ya kocha Msaidizi, Suleiman Matola lakini akarekebisha mambo na timu imezinduka.  
  Hata hivyo, Kopunovic amesema pamoja na ushindi wa mechi hizo mbili, baado kuna mambo ya kufanyia kazi ndani ya kikosi chake kwa haraka ili timu iwe bora.
  “Ni mambo ambayo siwezi kusema mbele ya vyombo vya Habari, bali nitazungumza na wachezaji wangu tu,”amesema.
  Beki wa Simba SC, Hassan Kessy kushoto ni kati ya wanaostahili sifa kwa uimara wa safu ya ulinzi ya Simba SC

  Amesema kwamba baada ya kuingia Robo Fainali, hawajui watakutana na timu gani, hivyo hawezi kuizungumzia timu yoyote kwa sasa, hadi hapo atakapomjua mpinzani wake wa hatua ijayo.
  Kwa kuongoza Kundi C, Simba SC itakutana na mshindi wa tatu bora namba mbili katika Robo Fainali kesho Uwanja wa Amaan, Zanzibar, ambaye anaweza kuwa kati ya JKU, KMKM, Polisi au Taifa Jang’ombe itategemea na matokeo ya mechi za mwisho leo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOPUNOVIC: MECHI MBILI BILA KURUHUSU BAO HII NDIYO SIMBA SC NINAYOITAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top