• HABARI MPYA

  Wednesday, January 07, 2015

  AMBAVYO FEDHA NI SUMU KWA WACHEZAJI WETU

  KUNA stori moja ya kizushi kuhusu Emmanuel Adebayor, kwamba baada ya kusajiliwa Arsenal Januari 13, mwaka 2006 kwa dau la Pauni Milioni 3 kutoka Monaco ya Ufaransa, alitaka kuacha soka.
  Stori hiyo inasema Adebayor alitaka kuacha mpira mara baada ya kupokea mshahara wake wa kwanza wa wiki Arsenal- zilikuwa fedha nyingi ambazo zilimtosha kufanya mambo makubwa nyumbani kwao Togo, ikiwemo kumjengea mama yake nyumba.
  Lakini watu wakamuweka chini na kumshauri, naye akatuliza kichwa na kuendelea kucheza soka, kuendelea kupokea fedha nyingi kila wiki.

  Huwezi kutaja wanasoka wa Afrika wenye mafanikio Ulaya, ukamuacha Adebayor- akiwa amecheza klabu kubwa kama Monaco, Arsenal, Real Madrid, Manchester City na sasa Tottenham Hotspur, huyu ni mchezaji mkubwa.
  Lakini pamoja na yote, ili kufikia mafanikio hayo makubwa alilazimika kuushinda mtihani wa kulewa fedha na badala yake kurudisha akili yake mchezoni.
  Nchini Tanzania wachezaji wengi wa sasa wanashindwa kuushinda mtihani wa kulewa fedha, na matokeo yake wanaua viwango vyao mapema na kuondoka kwenye soka haraka.
  Vijana wanajibidiisha sana wakati wana hali dunia ya kimaisha. Wanafanya mazoezi mengi na kucheza kwa juhudi, ili kukuza thamani zao, hatimaye wasajiliwe na timu zenye kulipa vizuri.
  Hapo unazungumzia, Azam FC, Simba na Yanga SC- hizo ndizo timu ambazo zinalipwa fedha nyingi wacheaji Tanzania.
  Lakini, wachezaji wengi baada ya kufikia kusajiliwa kwa mamilioni ya fedha na ama Azam, Simba au Yanga na kupewa mishahara minono ya mwezi, ufundi wao huhamia kwenye anasa.
  Pombe kwa wingi, ngono sana na kukesha kwenye klabu za usiku na sehemu nyingine za starehe.
  Yale mazoezi mengi ambayo ndiyo yaliwainua kisoka wanayapuuza, na matokeo yake viwango vinaanza kushuka kwa kasi.
  Wakati viwango vinashuka, hawafikirii kwamba kuzembea mazoezi na kuendekeza anasa ni chanzo cha kuporomoka kwake, bali wanaanza kuingiza imani za kishirikina, labda wachezaji wenzao wanawaloga.
  Na kwa imani hiyo, wanapoteza fedha nyingi na muda pia kwa ajili ya waganga, na kusahau kabisa kuhusu bidii ya mazoezi na anasa.
  Soka inazidi kuwakimbia na mwisho wa siku hata hizo klabu kubwa zinaamua kuachana nao- na huo unakuwa mwanzo wa kuporomoka kwao hadi kimaisha.
  Mifano ipo mingi ya wachezaji ambao viwango vilishuka kwa kasi baada ya kupatiwa fedha nyingi za usajili- kwa sababu ufundi wote ulihamia kwenye anasa.
  Vijana wakicheza mpira kwa maslahi duni, wanasikitika sana, lakini wanapoanza kupata fedha, nazo  zinawalevya na kuua vipaji vyao.
  Tazama jinsi gani fedha ni simu kwa wachezaji wetu, lakini kwa nini wasipate fedha kama wanacheza soka ya kisasa, ambayo wenzao Ulaya wanapata nzuri zaidi.
  Jambo kubwa hapa ni wachezaji hawa kupata mwongozo juu ya maisha ili waweze kujitambua- hatimaye waweze kupokea fedha na kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu.
  Hata klabu zinaweza kutusaidia katika hili, kwa kuwa na wataalamu maalum wa kuwashauri wachezaji hao, lakini kwa sasa ni fedha ni simu kwa wachezaji wetu. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AMBAVYO FEDHA NI SUMU KWA WACHEZAJI WETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top