• HABARI MPYA

    Wednesday, November 05, 2014

    AZAM FC WAINGIA KAMBINI LEO KUJIPANGA KWA AJILI YA COASTAL UNION JUMAMOSI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MABINGWA wa Tanzania Bara, Azam FC wanaingia kambini jioni ya leo katika hosteli za Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ya Tanga Jumamosi.
    Azam itashuka dimbani Jumamosi katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wakitoka kupoteza mechi mbili mfululizo, nyumbani na ugenini.
    Azam FC imefungwa mechi mbili mfululizo nyumbani na ugenini
    Azam FC ilifungwa 1-0 na JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam wiki iliyopita kabla ya mwishoni mwa wiki kufungwa tena 1-0 na wenyeji Ndanda FC mjini Mtwara. 
    Tovuti ya Azam FC imeandika kwamba, kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog baada ya matokeo hayo, wiki hii amekuwa bize na kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwenye michezo hiyo miwili, kuhakikisha matokeo mabaya hayajirudii.
    Beki Erasto Nyoni, aliyepata ajali juzi baada ya gari lake kugongana na mwendesha pikipiki, maarufu kama bodaboda anatarajiwa kuanza mazoezi jioni ya leo, baada ya kumaliza kesi yake Polisi.
    Azam FC itaendelea kumkosa mshambuliaji Kipre Tchetche aliyekwenda nyumbani kwao, Ivory Coast kwa matatizo ya kifamilia, wakati beki Gardiel Michael ameanza mazoezi baada ya kukosa mechi dhidi ya Ndanda kwa kuwa majeruhi.
    Kwa ujumla, kuelekea mchezo na Coastal, mshikamano ni mkubwa ndani ya timu kuanzia Wakurugenzi, uongozi, benchi la Ufundi na wachezaji kuhakikisha matokeo mazuri yanapatikana.
    Lengo la Azam FC bado ni kutetea ubingwa wake msimu huu, licha ya kupoteza pointi nane hadi sasa kwa sare moja na kufungwa mechi mbili- ikiwa inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Mtibwa Sugar pointi 14 na Coastal Union pointi 11.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC WAINGIA KAMBINI LEO KUJIPANGA KWA AJILI YA COASTAL UNION JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top