• HABARI MPYA

    Friday, October 03, 2014

    TBL YAONGEZA UHONDO NA VIONJO SIMBA NA YANGA NANI MTANI JEMBE, KAMPENI KUZINDULIWA RASMI KESHO

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MSIMU wa pili wa kampeni ya Nani Mtani Jembe umezinduliwa leo kwa Waandishi wa Habari wakati uzinduzi rasmi kwa wapenzi wa Simba na Yanga utafanyika viwanja vya Leaders Club, Dar es salaam na utajulikana kama Nani Mtani Jembe 2.
    Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari leo ukumbi wa Serengeti ndani ya hoteli ya JB Belmonte, Dar es Salaam, Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe amesema, “Dhumuni la kampeni yetu ya pili ya Nani Mtani Jembe ni kuisogeza Kilimanjaro Premium Lager karibu na wateja wake na wananchi na kuhamasisha ushindani kati ya mashabiki wa Simba na Yanga kwa kushindanisha mamilioni ya mashabiki wa  klabu hizi nchi nzima kwa kipindi cha wiki kumi kuanzia Oktoba hadi Disemba.

    Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George  Kavishe   akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar s Salaam  jana wakati akizungumzia uzinduzi wa Kampeni ya Nani Mtani Jembe 2

    Alisema, “kampeni hii itazinduliwa  na mlolongo wa matukio ambapo tukio la pili litakuwa ni uzinduzi rasmi kwa wadau jijini Dar es salaam ambapo Nani Mtani Jembe 2 itatambulishwa kwa wadau na mashabiki wa Simba na Yanga. Uzinduzi huu utafuatiwa na hafla fupi za kuzindua kampeni hii katika viwanda vyote vya  bia ya TBL nchini katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Moshi na Arusha lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa wafanyakazi wa TBL kuhusu Nani Mtani Jembe 2 ili waweze kuwa mabalozi wazuri. Pamoja na kampeni hiyo, tutakuwa na uzinduzi wa kipindi cha  televisheni  kiitwacho “Kili Chat ”ambacho kitarushwa hewani kwa muda wa wiki kumi kikijumuisha watu maarufu nchini ili kuitangaza Nani Mtani Jembe 2 zaidi na kuhakikisha  uwanja wa Taifa unajaa  siku ya mechi. ”  
    Akieleza utaratibu wa kampeni hiyo, Kavishe alisema kampeni hiyo itahusisha mashabiki wa Simba na Yanga ambapo jumla ya shilingi milioni 100 zitatolewa na kugawanywa katika makundi mawili.
    "Shilingi Milioni 20 itakuwa zawadi ya fedha kwa ajili ya mechi ya Nani Mtani Jembe 2, ambapo timu itakayoshinda itaondoka na kitita cha shillingi milioni 15 na shillingi milioni 5 zitatolewa kwa timu itakayofungwa mechi. 
    "Kampeni hiyo itaendeshwa kwa njia ya sms ambapo mashabiki watapiga kura kwa njia ya sms na shilingi milioni 80 zitagawanywa kati ya timu hizo mbili. Kwa hiyo kila timu itaanza na shillingi milioni 40 kwenye benki maalum  mtandaoni kwa ajili ya shindano,"amesema.
    Kavishe ameongeza kwamba, kwa kila bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye ujazo wa  500ml mnunuzi atakuta namba maalum chini ya kizibo cha bia hiyo, namba hizo atazitumia kutuma  sms kwenda kwenye namba maalum 15415.
    Amesema ni lazima mnunuzi aandike kwenye sms kuwa yeye ni shabiki wa timu ipi kwa kuandika neno SIMBA au YANGA ikifuatiwa na namba zilizopo chini ya kizibo, na anapotuma sms ataweza kupunguza shilling 10,000 kwenye benki ya timu pinzani na kuweka kiasi hicho kwenye timu yake.
    "Mwisho wa kampeni hiyo kila klabu itakuwa imeongeza au kupoteza kiasi cha fedha kwa timu pinzani, kulingana na jinsi mashabiki walivyopiga kura. Kwa mfano, kama mashabiki wa Simba watapiga kura zaidi ya mashabiki wa Yanga itamaanisha kwamba Simba itashinda na kupata fedha zaidi kutoka kwenye kiasi cha milioni 80, hivyo hivyo kwa mashabiki wa Yanga kama watapiga kura zaidi kuliko mashabiki wa Simba itamaanisha Yanga itapata fedha zaidi,"ameongeza.
    Kampeni hizo zinatarajiwa kuongeza chachu ya ushindani kati ya mashabiki wa Simba na Yanga kwa kuwapa fursa mashabiki kuonyesha mapenzi yao kwa timu zao na pia zitafungua milango ya  Kili kuendelea kuwa karibu zaidi na mashabiki na vilevile itazisaidia klabu hizi kuongeza idadi ya mashabiki na kuimarisha ushabiki na mapenzi kwa timu zao.  
    Mbali na kampeni ya sms, Nani Mtani Jembe 2 itahusisha mashabiki wa klabu za Simba na Yanga katika  promosheni mbalimbali na kuwawezesha kushinda zawadi mbalimbali kila wiki pamoja na fedha taslimu. Kampeni hii itafika kileleni mwezi Disemba ambapo itahitimishwa na mechi ya Nani Mtani Jembe 2 kati ya Simba na Yanga katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam mbele ya mashabiki wa timu hizo. IIi timu ziweze kujiandaa vizuri, kila timu itapata kiasi cha shilingi milioni 30 kwa ajili ya maadalizi ya mechi hiyo zikiwa ni ongezeko kutoka shilingi milioni 20 za mwaka jana. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TBL YAONGEZA UHONDO NA VIONJO SIMBA NA YANGA NANI MTANI JEMBE, KAMPENI KUZINDULIWA RASMI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top