• HABARI MPYA

    Saturday, October 04, 2014

    RWANDA WABOMOA TIMU YA TAIFA, MAKANJANJA WOTE WATIMULIWA, WAMO NA MEDDIE KAGERE, KAGABO NA JEROME SINA

    Na Mwandishi Wetu, KIGALI
    KATIKA jitihada za kujenga upya misingi imara ya soka ya nchi yake, Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA), limeamua kuwatema wachezaji wote wa timu ya taifa ambao si wazaliwa wa nchi hiyo.
    Uamuzi huo unafuatia Rwanda kuenguliwa katika hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2015 Agosti mwaka huu, baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuifungia Amavubi kwa kumtumia mchezaji mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tady Etekiama Agiti ambaye kwa Rwanda anafahamika kama Dady Birori.
    Birori anayechezea AS Vita ya DRC pia amefungiwa na CAF kwa miaka miwili kwa kitendo cha kumiliki pasi mbili za kusafiri za nchi mbili tofauti na majina tofauti.
    Meddie Kagere ameenguliwa Amavubi kwa sababu ni Mganda 

    Kocha Mkuu wa Amavubi, Stephen Constantine  amesema kwamba wamechukua maamuzi magumu kuachana na wachezaji wote ambao si wazaliwa wa Rwanda, ili kuepuka kurudia makosa.
    Mshambuliaji mzaliwa wa Uganda, Meddie Kagere aliyejiunga na FK Tirana ya Albania miezi miwili iliyopita sasa hataichezea tena Amavubi, licha ya kuifungia mabao 29 tangu aanze kuichezea mwaka 2011.
    Jimmy Mbaraga na Peter Kagabo ambao wanachezea Polisi FC ya Ligi Kuu ya Rwanda pamoja na nyota wa Rayon Sport, Jerome Sina pia wameambiwa hawataichezea tena Amavubi.
    “Tunafahamu tuna pengo kubwa, kwa sababu wanne kati yao walikuwa ni washambuliaji. Ni jambo zito tunaposema kuhusu washambuliaji, ni kitu ambacho tutakwenda kukifanyia kazi kuziba mapengo,” amesema Constantine.
    Muingereza huyo aliyeanza kazi Amavubi Mei mwaka huu anavutiwa na mafanikio ya wachezaji hao, lakini amesema sasa ni wakati wa kuanza kufanya kitu sahihi.
    Amefafanua, “Ikiwa tulikuwa tuna kundi la wacheaji 30 kuteua kati yao, sasa tumebaki na 25. Tunatakiwa kuanza kuinua wachezaji wachanga na uamuzi sahihi ni kutumia wachezaji wazawa tu,”.
    Sasa wachezaji hao wote wanatarajiwa kurejesha pasipoti za Rwanda Idara ya Uhamiaji ili wapewe pasipoti zao halisi za nchi walizozaliwa.
    Maana yake Kagere na Kagabo, watarejeshewa utaifa wao wa Uganda na ikibidi kubadilisha majina, itafanyika hivyo.
    Kagabo anatarajiwa kurudia kutumia jina lake halisi, ambalo ni Peter Otema wakati Sina anatarajiwa kurudishiwa pasipoti yake ya Kongo na jina halisi Jerome Sena Abedi.
    Rais wa FERWAFA, Vincent Degaule Nzamwita amesema; “Tunafanya kazi kwa karibu na Shirikisho la Soka la DRC kuhakikisha tunaepuka wachezaji kuwa na uraia wa nchi mbili baina yetu na pia kupambana na wachezaji ambao wanacheza ligi za nchi zote (Rwanda na DRC) kwa majina tofauti,”
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RWANDA WABOMOA TIMU YA TAIFA, MAKANJANJA WOTE WATIMULIWA, WAMO NA MEDDIE KAGERE, KAGABO NA JEROME SINA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top