• HABARI MPYA

    Saturday, October 18, 2014

    MRISHO NGASSA JINA KUBWA ‘KIGOLI KIMOJA TU’ MECHI ZA WATANI TANGU MWAKA 2007

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    HAPANA shaka Mrisho Khalfan Ngassa ni jina kubwa katika soka ya Tanzania hivi sasa- akiwa amekwishachezea timu zote kubwa, Simba na Yanga.
    Kwa sasa, Ngassa anavalia jezi za rangi ya kijani na njano na Yanga SC baada ya mwaka juzi kuchezea Simba SC, inayotumia ‘uzi’ wa rangi ya nyekundu na nyeupe.
    Na leo mahasimu hao wa jadi katika ya soka Tanzania, wanakutana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga SC ilimuuza Ngassa kwa Azam Mei 21, mwaka 2010 kwa dola za Kimarekani 40,000 baada ya kuchezea timu hiyo tangu mwaka 2007 alipojiunga nayo akitokea Kagera Sugar ya Bukoba.
    Mrisho Ngassa amefunga bao moja tu mechi za watani tangu aanze kuzicheza mwaka 2017

    Hata hivyo, Agosti mwaka juzi aliukera uongozi wa Azam FC kwa kwenda kubusu jezi ya Yanga SC baada ya kufunga bao la ushindi katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DRC, Uwanja wa Taifa.
    Baada ya kuiwezesha Azam, kutinga fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa 2-1, uongozi ulimuamuru kocha Stewart Hall asimpange mchezaji huyo kwenye fainali dhidi ya Yanga SC, lakini akakaidi na kumpanga na timu ikafungwa.
    Kilichofuatia, Azam FC iliamua kutangaza kumuuza mchezaji huyo kwa mkopo na Simba SC wakashinda tenda hiyo, wakati Stewart alifukuzwa na kwenda Sofapaka ya Kenya, kabla ya kurejea Azam na kufanya kazi kwa mwaka mmoja, kisha akajiuzulu mwenyewe Desemba mwaka jana.
    Ngassa aligoma kuuzwa bila idhini yake, lakini Simba SC wakaketi naye mezani na kufikia makubaliano, kabla ya kumtangaza rasmi kujiunga na klabu hiyo. Alipomaliza mwaka, Ngassa akaenda kusaini Yanga.
    Simba SC ikasema ilimuongezea Mkataba mchezaji huyo na kumpa Sh. Milioni 30, wakati yeye mwenyewe akasema alipewa fedha hizo, ili akubali kucheza kwa mkopo.
    Enzi za Msimbazi; Wachezaji wa Yanga SC, Didier Kavumbangu kulia (amehamia Azam FC) na Haruna Niyonzuma kushoto wakimdhibiti Mrisho Ngassa wakati akichezea Simba SC

    Hata hivyo, TFF ikabaini mchezaji huyo alisaini Simba SC pia hivyo kumfungia mechi sita na kumtaka arejeshe Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15. 
    Kumbuka katika kipindi chote ambacho Ngassa alicheza Yanga kabla ya kwenda Azam, hakuwahi kutikisa nyavu za Simba SC zaidi ya kutoa pasi za mabao tu. Na hata akiwa Simba SC hakuifunga Yanga. 
    Lakini baada ya kurejea Yanga SC mwaka jana, Ngassa alifunga kwa mara ya kwanza kwenye mechi za watani, katika sare ya 3-3 Oktoba 20, 2013. Ngassa alianza kuifungia Yanga SC dakika ya 15 kabla ya Mganda Hamisi Kiiza kuongeza mawili dakika ya 36 na 45
    Kipindi cha pili, Simba SC ikasawazisha mabao hayo kupitia kwa Betram Mombeki dakika ya 54, Mganda Joseph Owino dakika ya 58 na Mrundi Gilbert Kaze dakika ya 85.
    Shabiki mtoto wa Yanga SC, akiwa ameandika jina la Ngassa kichwani

    Ngassa akacheza mechi ya Nani Mtani Jembe Desemba 31, mwaka jana Yanga SC ikichapwa 3-1 na akacheza mechi ya mzunguko mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, timu hizo zikitoka saare ya 1-1, na hakufunga bao kwenye mechi zote hizo.
    Kweli Mrisho Ngassa ni jina kubwa katika soka ya Tanzania, lakini hadi sasa bado hana kubwa la kujivunia kwenye mechi za watani zaidi ya bao moja alilofunga mwaka jana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MRISHO NGASSA JINA KUBWA ‘KIGOLI KIMOJA TU’ MECHI ZA WATANI TANGU MWAKA 2007 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top