• HABARI MPYA

    Thursday, October 02, 2014

    KIPI SAMATTA HAJAFANYA TP MAZEMBE, NA AENDELEE KUSUBIRI NINI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NDOTO za mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta kushinda taji la Afrika na klabu yake, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa mara nyingine ziliyeyuka mwishoni mwa wiki.
    Hiyo ilifuatia Tout Puissant Mazembe kutolewa na ES Setif ya Algeria katika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao ya ugenini baada ya sare jumla ya 4-4.
    Setif walishinda 2-1 katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita na Mazembe wakashinda 3-2 katika mchezo wa marudiano mwishoni mwa wiki mjini Lubumbashi.
    Setif sasa wanakwenda kukutana na AS Vita ya DRC pia katika fainali baadaye mwezi huu, wakati Mazembe wanasubiri mwakani kuanza upya kusaka taji la tano la Ligi ya Mabingwa.
    Kilio; Mbwana Samatta akilia baada ya Tanania kutolewa na Msumbiji katika AFCON Julai mwaka huu 

    Samatta alilia na kumwaga machozi baada ya Mazembe kufungwa katika fainali ya Kombe la Shirikisho na CS Sfaxien ya Tunisia na hali hiyo imejirudia mwaka huu wakitolewa katika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa.
    Kwa mwaka huu, Samatta analia kwa mara ya pili, baada ya awali kububujikwa machozi kufuatia Tanzania kutolewa na Msumbiji katika mechi za kufuzu AFCON.
    Hautakuwa mwaka mzuri kwake 2014 na akionekana mchezaji mwenye malengo dhahiri Samatta anajisikia vibaya. Mafanikio yoyote yaliyotangulia kwa sasa si kitu kwake akiwa na kiu ya mafanikio zaidi.
    Huyo ni aina ya mchezaji tofauti na wachezaji wengi wa hapa Tanzania- akiwa analipwa zaidi ya Sh. Milioni 16 za Kitanzania kwa mwezi DRC, analipiwa nyumba na kupata posho na huduma nzuri kwa ujumla, hajabweteka.
    Wakati fulani mwaka jana katika mahojiano na BIN ZUBEIRY, Samatta alisema kwamba anajuta kusaini Mkataba mrefu TP Mazembe (miaka minne) ambao unambana kwa sasa.
    Samatta alisema kila anaposoma habari za wachezaji wengine namna wanavyolipwa Ulaya na akilinganisha uwezo wao na wa kwake, huwa anaumia sana.
    Samatta akiwatoka wachezaji wa Setif mwishoni mwa wiki


    Miezi miwili iliyopita alipokuja nchini kwa ajili ya mechi za Taifa Stars, Samatta alisema kwamba anaweza kuondoka Mazembe baada ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.
    Alisema hayo ni makubaliano yake na mmiliki wa Mazembe bilionea Moise Katumbi, ambaye amemuahidi kumtia sokoni baada ya Ligi ya Mabingwa.
    Na kwa sababu tayari Mazembe iko nje ya michuano hiyo, tutarajie mchezaji huyo wa zamani wa Mbagala Market atakuwa sokoni katika dirisha dogo Januari mwakani.
    Tayari klabu kadhaa kubwa za Kaskazini mwa Afrika, Afrika Kusini na Ulaya zimeonyesha nia ya kumnunua mpachika mabao huyo na hakuna kingine kinachowavutia zaidi ya uwezo wake mkubwa.
    Januari 7, mwakani Samatta atatimiza umri wa miaka 23  na hapana shaka ni wakati mzuri tu kuhamia Ulaya, iwapo Mungu atamjaalia bahati hiyo.
    Samatta kwa uwezo wake wa sasa anaweza kucheza klabu za Ulaya na akapata mafanikio ambayo siku moja yanaweza kuifanya Tanzania itajwe kwenye michuano mikubwa ya UEFA.
    Kitu ambacho anapaswa kuomba kwa sasa Mbwana ni bahati ya kupata nafasi ya kuingia Ulaya, baada ya hapo kwa uwezo wake kocha yeyote mtaka mafanikio atampa nafasi. Na akipata nafasi, si rahisi Samatta kuichezea.
    Wakati wote Samatta ni mchezaji mwenye kiu, mwenye kujitambua na ameonyesha dalili za kuwa na bahati kwa mafanikio yake ya awali.
    Samatta alitokea Simba SC kwenda TP Mazembe

    SAFARI YA SAMATTA HADI TP MAZEMBE
    Baada ya vigogo wa DRC kuitoa Simba SC katika hatua ya 32 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2011, ikawasilisha maombi ya kununua wachezaji wawili, Mganda Patrick Ochan na dogo huyo wa Tanzania, wakati huo akiwa na umri wa miaka 20 tu.
    Simba SC ilimsajili Samatta mwanzoni mwa msimu wa 2010/2011 kutoka African Lyon ambayo ilikuwa inabadilishwa kutoka kwenye umiliki wa Mohamed Dewji hadi Rahim Kangezi.
    Hata hivyo, Samatta aligoma kuanza kazi Simba SC hadi atimiziwe ahadi alizopewa ambazo ni Sh. Milioni 2 na gari aina ya Toyota GX100. Awali, Simba SC walimpuuza, lakini baadaye wakashituka na Desemba 2010 wakamalizana naye, hatimaye akaanza kazi Msimbazi.
    Kocha Patrick Phiri hakuwa akimpa nafasi mchezaji huyo mwanzoni, lakini mambo yalipokuwa magumu alianza kumtolea benchi kuingia uwanjani, naye akaanza kufanya vitu.
    Simba SC ililazimishwa sare ya bila kufungana na Elan Mitsoudje nchini Comoro katika mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na katika mchezo wa marudiano, dakika 45 za kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana 1-1.
    Madaha Mohammed alitangulia kuwafungia Elan Mitsoudje dakika ya 43, lakini kipa Youssouf Ahamada akajifunga katika harakati za kuokoa dakika ya 45 kuipatia Simba SC bao la kusawazisha.
    Kocha Phiri, akamuinua Samatta kipindi cha pili na alipoingia tu akamsetia Ochan kuwafungia Wekundu hao wa Msimbazi bao la pili dakika ya 47 kabla ya yeye mwenyewe kufunga la tatu dakika ya 56 na Amri Kiemba la nne dakika ya 71. Bao lingine la Elan lilifungwa na Abdulkarim Sandjema dakika ya 63.
    Wakati mwafaka sasa Samatta kuondoka TP Mazembe akakutane na changamoto nyinigne

    Simba SC ikatinga 32 Bora, mchezo wa kwanza ikafungwa 3-1 na TP Mazembe mjini Lubumbashi na marudiano, wakafungwa tena 3-2 Dar es Salaam, mabao ya Wekundu wa Msimbazi yakifungwa na Shijja Mkinna dakika ya 58 na Samatta dakika ya 70.
    Huo ukawa mwisho wa Samatta Simba SC, kwani alinunuliwa Mazembe kwa pamoja na Ochan.
    Simba ilirudishwa mashindanoni baada ya kushinda rufaa waliyomkatia beki wa Mazembe, Janvier Besala Bokungu, aliyevunja mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia na ikacheza mechi ya mkondo mmoja na Wydad Casablanca ya Morocco mjini Cairo, Misri na kufungwa 3-0, hivyo kuangukia kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa mabao 2-1. 
    Samatta akaanza kuichezea Mazembe Juni 2011 katika Ligi Kuu ya DRC na katika msimu wake wa kwanza akatwaa taji hilo na klabu yake hiyo mpya. Mwaka 2012 Samatta akang’ara katika Ligi ya Mabingwa Afrika akifunga mabao sita dhidi ya vigogo Al Ahly, Zamalek, Berekum Chelsea, Power Dynamos na Al-Merrikh.
    Mazembe ilitolewa katika Nusu Fainali mwaka huo na mwaka jana wakatolewa hatua ya 16 Bora na kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho ambako walifika fainali- mwaka huu wametolewa Nusu Fainali.
    Lakini katika miaka yake mitatu ya kufanya kazi Mazembe, Samatta amevaa Medali ya Fedha ya Kombe la Shirikisho mwaka 2013, ametwaa taji la Super Cup la DRC mara mbili mfululizo 2013 na 2014, ubingwa wa Ligi Kuu DRC mara zote nne, 2011, 2012, 2013 na 2014. 
    Mafanikio binafsi kwa Samatta katika Ligi ya DRC ni kuwa mfungaji bora msimu wa 2012/2013. Ameshinda mataji sita na TP Mazembe katika miaka minne, amecheza Nusu Fainali mara mbili Ligi ya Mabingwa Afrika na amecheza Fainali moja ya Kombe la Shirikisho. 
    Samatta hajashinda taji la Afrika tu na klabu hiyo, lakini pamoja na hayo ni wakati mwafaka kwake kuondoka akapambane na changamoto mpya katika ulimwengu wa soka angali kijana mdogo. Kila la heri Poppa, au Sama Goals kama wamuitavyo Lubumbashi. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPI SAMATTA HAJAFANYA TP MAZEMBE, NA AENDELEE KUSUBIRI NINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top