• HABARI MPYA

    Sunday, September 01, 2013

    YANGA SC SASA WACHEZE BILA MASHABIKI UWANJANI, HIYO NDIYO ADHABU INAYOWAFAA

    IMEWEKWA SEPTEMBA 1, 2013 SAA 12:15 ASUBUHI
    WAHENGA wamenena, samaki mkunje angali mbichi- lakini pia tuna usemi mwingine; tahadhari ni bora kabla ya hatari. Haya sijui yana maana gani mbele ya viongozi wetu wa soka kwa ujumla, kuanzia klabu, vyama vya wilaya, mikoa na shirikisho la taifa (TFF).
    Maana wamekuwa wakinyamazia matukio yenye dalili za kuleta athari kubwa zaidi mbele, jambo ambalo hakika si zuri.
    Kwa mara nyingine, Jumatano wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam uligeuka kilinge cha mapambano na damu kumwagika, kufuatia mashabiki wa Yanga SC kulishambulia basi la wachezaji wa Coastal Union ya Tanga na kujeruhi mmoja wa wachezaji wa timu hiyo.

    Hayo yalitokea baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, timu hizo zikitoka sare ya 1-1, Coastal Union wakisawazisha kwa penalti dakika ya 90.  Sikuwepo Uwanja wa Taifa na hadi naandika makala haya sijabahatika hata kuiona mechi hiyo, kwa sababu Jumatano hiyo nilikuwa Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora ambako kulikuwa kuna mchezo mwingine wa Ligi Kuu kati ya Azam FC na wenyeji Rhino.
    Kwa sababu hiyo siwezi kuzungumzia malalamiko ya Yanga kuonewa na refa- lakini kitu ambacho ninalaani kwa nguvu zangu zote ni vurugu walizofanya mashabiki wa timu hiyo na ninaona, wakati umefika sasa TFF ichukue maamuzi magumu dhidi ya klabu hiyo, ili iwe fundisho.
    Hii si mara ya kwanza kwa mashabiki wa Yanga kufanya fujo uwanjani na kusababisha uharibifu wa mali na hata kujeruhi na kwa ujumla kuhatarisha amani. Wenye soka yao, FIFA wanauita mchezo wa kiungwana- hawataki uhuni hata kidogo na TFF kama wasimamizi wakuu wa soka nchini, wanapaswa kulizingatia hilo.
    Lakini tatizo kubwa, TFF wanashindwa kuchukua adhabu ambazo zitakuwa fundisho kwa mashabiki wa Yanga na wengine wote, kwa sababu wameweka mbele fedha kuliko utu na thamani ya mchezo wenyewe.
    Wakati umefika sasa, Yanga ipewe adhabu ya kucheza mechi bila mashabiki uwanjani, japo tatu tu na bila shaka baada ya kukosa fedha, viongozi wake wataona umuhimu wa kuwasihi mashabiki wao wawe wastaarabu.
    Lakini kama tutaendelea na ile desturi ya faini Sh. 500,000 na kutakiwa kufidia gharama za uharibifu na tiba za waliojeruhiwa, hakika iko siku litakuja kutokea kubwa kutokana na mashabiki hawa wa Yanga.
    Rejea Machi 31, 2002 wakati Simba SC inaifunga Yanga 4-1 katika Fainali ya iliyokuwa michuano ya Kombe la Tusker, mabao ya Mark Sirengo dakika ya tatu na 76, Madaraka Selemani dakika ya 32 na Emanuel Gabriel dakika 83 upande wa Simba na Sekilojo Chambua wa Yanga dakika ya 16.
    Mbele ya mgeni rasmi, rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu mechi hiyo ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa aweze kupiga. 
    Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa na mashabiki wa Yanga. 
    Refa wa mchezo huo, Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. 
    Baada ya hapo, adhabu waliyopewa Yanga ni faini na Tarimba alifungiwa kwa sababu alionekana chanzo cha vurugu zilizotokea. Lakini Yanga wamerudia, na wameendelea tena kuhatarisha amani viwanjani, na unaweza kuona wazi kwa adhabu wanazopewa, hawataacha na wataendelea.
    Wazi, kama tunataka kuivusha soka yetu katika hatua nyingine, lazima kwanza tukubali kujivua ushabiki na kuchukua hatua ambazo moja kwa moja zitalenga maslahi na ustawi wa mchezo huu nchini. 
    Wakati umefika sasa, tuondoe dhana kwamba Yanga chini ya utawala Leodegar Tenga na Athumani Nyamlani haiwezi kuchukuliwa hatua kali hata ikifanya kosa kubwa kiasi gani, kwa sababu viongozi wote hao wawili ni Yanga wazuri. Si sahihi.
    Tunakumbuka, wakati fulani mashabiki wa Ashanti walifanya vurugu katika mechi dhidi ya Yanga SC na wakafungiwa kucheza Uwanja wa Taifa. Lakini ni mara ngapi Yanga wamefanya vurugu na wamechukuliwa hatua kama hiyo angalau, au ilionewa Ashanti tu?  
    Ndiyo, Ashanti haina mashabiki wa kuingiza hata Milioni 1 na mchezo mmoja wa Ligi Kuu wa Yanga wenye kiwango kidogo kabisa cha fedha ni Sh. Milioni 40, sasa bila shaka hili nalo linachangia kwa kiasi kikubwa, lakini kwa nini tuweke fedha mbele kuliko utu na thamani ya mchezo wenyewe?
    Ajabu tangu yametokea maafa hayo Jumatano, hadi leo si kiongozi wa TFF wala Yanga aliyelaani tu- na kitakachofuata, Boniface Wambura atatoa taarifa siku mbili hizi ikisema Yanga wametozawa faini na kupewa onyo kali. Angekufa mchezaji wa Coastal? Alamsiki waungwana.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA SC SASA WACHEZE BILA MASHABIKI UWANJANI, HIYO NDIYO ADHABU INAYOWAFAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top