• HABARI MPYA

    Sunday, October 28, 2012

    PRISONS WATAKA MECHI YAO NA RUVU PIA IAHIRISHWE

    Wachezaji wa Prisons

    Na Mashaka Mhando,Tanga
    UONGOZI wa klabu ya Tanzania Prison, umeliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuahirisha mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani inayotakiwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 31, kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi, Pwani.
    Katibu Mkuu wa timu hiyo, Sadiq Jumbe alisema wanaishukuru TFF kwa kuahirisha mchezo wao uliopita dhidi ya Mgambo JKT uliokuwa upigwe kwenye Uwanja wa Mkwakwani jana (Oktoba 27), kufuatia ajali ambayo timu yake ilipata jana.
    Alisema sababu kubwa ya kutaka mchezo huo nao uahirishwe ni kutokana na wachezaji wake tegemeo kutokuwa katika hali nzuri, baada ya ajali hiyo.
    "Kwa kweli ajali tuliyoipata ni kubwa, kila mtu mawazo yake hayapo, achilia mbali wachezaji walioumia, tunatakiwa tukae muda kutafakari na kuwapa nafasi wachezi walioumia kupumzika na kocha wetu aandae wachezaji watakaochukua namba za waliopata ajali, sasa tunaomba TFF wauahirishe pia mchezo wetu unaofuata dhidi ya Ruvu Shooting," alisema Jumbe.
    Wachezaji sita wa Prison waliopata ajali ya basi usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita katika eneo la Hale wilayani Korogwe na kulazwa katika hospitali ya Teule iliyopo wilayani Muheza mkoani Tanga na kisha kuhamishiwa katika hospitali ya mkoa Bombo, wameruhusiwa na hali zao zinaendelea vizuri.
    Ajali hiyo ilitokea katika eneo hilo baada ya basi dogo, aina ya Coasta lililowabeba wachezaji na viongozi wa timu hiyo wapatao 21 kuacha njia na kupinduka wakati likiwa njiani kwenda Jijini Tanga.
    Hiyo ilifuatia dereva wa gari hilo kushindwa kuumudu usukani, baada ya kumulikwa na mwanga mkali wa taa za lori ambalo lilikuwa mbele yake huku kukiwa na lori lingine pembeni ya barabara limepaki.
    Katibu huyo alisema wanamshukuru Mungu kwa kupata nafuuu kwa wachezaji wake na hatimaye kuweza kuruhusiwa kutoka hospitalini ingawa bado wanakabiliwa na majeraha waliyoyapata katika miili yao.
    Jumbe ambaye naye aliumia sehemu ya kifuani katika ajali hiyo aliwataja wachezaji walioumia na kukimbizwa hospitalini kabla ya kuruhusiwa ni Issa Mwantika, Lugano  Mwangama, Khalid Fungabreki, Daudi Masungwe ambaye alikuwa amepoteza fahamu na Misango Magai.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: PRISONS WATAKA MECHI YAO NA RUVU PIA IAHIRISHWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top