• HABARI MPYA

  Wednesday, October 24, 2012

  YANGA NA POLISI TAIFA, AZAM YAWANIA USUKANI CHAMAZI MBELE YA RUVU SHOOTING LEO

  Yanga SC

  Na Mahmoud Zubeiry
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mechi nne za raundi ya tisa huku Azam ikiusaka usukani wa ligi hiyo ikiwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
  Kipre Herman Tchetche, tegemeo la Azam
  Mechi hiyo namba 60 ambayo kama Azam itashinda itafikisha pointi 20, hivyo kuwa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom itakayochezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, viingilio vyake vitakuwa ni Sh. 3,000 kwa sh. 10,000.
  Lakini macho na masikio ya wengi yatakuwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao Yanga wataikaribisha Polisi Morogoro, wanaoshika mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
  Katika mechi hiyo ambayo viingilio vitakuwa Sh. 5,000, Sh. 8,000, Sh. 15,000 na Sh. 20,000, refa Alex Mahagi kutoka Mwanza ndiye atakayepuliza filimbi kwenye mechi hiyo namba 62, akisaidiwa na Frank Komba na Michael Mkongwa, wote kutoka Iringa wakati mwamuzi msaidizi ni Oden Mbaga anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) wa Dar es Salaam.
  Katika mechi hiyo, Yanga itawakosa mabeki wake wa kati, Job Ibrahim, Kevin Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi ambao ni majeruhi.
  Job, ambaye amekuwa beki wa akiba tangu mwanzoni mwa msimu, aliumia kifundo cha mguu mazoezini mwishoni mwa wiki na juzi hakufanya mazoezi kabisa, wakati Yondan na Bahanuzi wanaendelea na programu ya mazoezi mepesi, chini ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts.
  Kwa sababu hiyo, Mbuyu Twite ataendelea kucheza pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika beki ya kati, wakati Jerry Tegete ataendelea kucheza na Didier Kavumbangu katika safu ya ushambuliaji.
  ‘Dogo’ Simon Msuva amemaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa Oktoba 3, mwaka huu katika mechi dhidi ya Simba na ilikuwa aanze kucheza tangu Jumamosi, ila kutokana na kiwango duni cha Hamisi Kiiza alichoonyesha kwenye mechi na Ruvu Shooting Jumamosi, leo kinda huyo anaweza kurudishwa uwanjani.
  Kiiza aliichezea Yanga kwa mara ya kwanza siku hiyo akitokea benchi kipindi cha pili, tangu atolewe kipindi cha kwanza katika mechi dhidi ya Simba, Oktoba 3, mwaka huu. Kiiza alikuwa kwao, Uganda, alipokwenda kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes katika mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini.
  Uganda ilitolewa na Zambia kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda nyumbani 1-0 na Uganda wakashinda kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
  Yanga imeweka kambi katika hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam huku ikiendelea kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
  Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu, wakati Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Oktoba 8, mwaka huu.
  Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
  Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
  Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 14, baada ya kucheza nane, kushinda nne, sare mbili na kufungwa mbili. Simba iliyocheza mechi tisa, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 19, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 17, iliyocheza mechi saba.
  Kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, wenyeji Coastal Union wataikaribisha African Lyon ya Dar es Salaam, wakati Mtibwa Sugar itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko kwenye mashamba ya miwa Turiani mkoani Morogoro.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA NA POLISI TAIFA, AZAM YAWANIA USUKANI CHAMAZI MBELE YA RUVU SHOOTING LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top