• HABARI MPYA

  Alhamisi, Oktoba 25, 2012

  TAIFA CUP KIKAPU OKTOBA 29 TANGA, WAMAREKANI WAJA KUFUNDISHA TIMU ZA TAIFA

  Magesa

  Na Princess Asia
  MASHINDANO ya mpira wa Kikapu ya kombe la Taifa, yanatarajiwa kufanyika mjini Tanga kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 4, mwaka huu.
  Makamu wa rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Phares Magesa ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mashindano haya ya Kombe la Taifa kwa kawaida ndio hutumika kuchagua timu zetu za Taifa, hvyo ni muhimu kwa mikoa yote kushiriki ili kuwapa nafasi wanamichezo kutoka mikoa yao kuonekana katika ngazi ya Taifa.
  Ameitaja mikoa iliyothibitisha hadi sasa ni Iringa, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Singida, Mara, Dodoma, Pemba, Unguja, Tanga, Mtwara, Lindi na Dar Es Salaam.
  “Bado nafasi ya kuthibitisha kushiriki ipo kwa wanaopenda kushiriki katika mashindano haya na ratiba ya mashindano itapangwa tarehe 28/10/2012 katika kikao ambacho wawakilishi wa mikoa yote lazima wawepo na ndo itakuwa mwisho wa kuthibitisha kushiriki,”alisema.
  Akizungumzia makocha wa timu yaifa kutoka Marekani, Magesa alisema Kocha Mkuu atakuwa Albert Sokaitis mwenye uzoefu wa miaka 24, ambaye kwa sasa anafundisha timu ya Chuo Kikuu cha Post, Marekani katika jimbo la Connecticut, ambaye pia amewahi kufundisha timu na kuendesha mafunzo nchi za Uchina, Lebanon, Ugiriki na Japan.
  Amesema Sokaitis atasaidiwa na Jocquis L. Sconiers mwenye uzoefu wa miaka mingi, ambaye kwa sasa ni Kocha Msaidizi wa timu ya Chuo Kikuu cha Post huko Marekani katika jimbo la Connecticut.
  “Walimu wote hawa wana shahada za juu kutoka vyuo vikuu  mbali mbali vya Marekani na katika utekelezaji wa mpango huo katika awamu ya kwanza Kocha Sconiers anatarajiwa kuwasili nchini  Oktoba 30 na ataelekea Tanga siku inayofuata katika Kombe la Taifa ili kuchagua wachezaji wa timu za taifa (wanawake na wanaume) na baada ya hapo ataanza kazi rasmi kwa timu zote Novemba 5,”alisema.
  Alisema awamu hii ya kwanza ya mpango wa mafunzo unadhaminiwa na watu wa Marekani kupitia ubalozi wao hapa Tanzania na kwamba wanawashukuru kwa msaada huo.
  Aidha, Magesa alisema kama mipango yote ikienda vizuri, wanatarajia kuwa wenyeji wa mashindano ya kanda ya Tano ya FIBA, yanayotarajiwa kufanyika mjini Dar es Salaam kuanzia Desemba 15 hadi 22, mwaka huu.
  “Hivyo basi Kocha huyo atatumia nafasi hii kuanza maandalizi ya timu zetu za Taifa kuziandaa kwa mashindano haya yanayotarajiwa kushirikisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Eritrea, Somalia, Djibouti, Misri Sudan na Sudani ya kusini,”alisema.
  Kuhusu Mkutano Mkuu wa TBF, alisema wanatarajia utafanyika Novemba 1 hadi 2, mwaka huu na amewataka viongozi wote wa Mikoa na wawakilishi wachezaji, vyama shiriki kushiriki bila kukosa katika mkutano huu utakaofanyika Tanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: TAIFA CUP KIKAPU OKTOBA 29 TANGA, WAMAREKANI WAJA KUFUNDISHA TIMU ZA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top